Getrude Lwakatare |
WAMO DEWJI,
LWAKATARE, RUTABANZIBWA
WABUNGE Mohamed Dewji wa Singida mjini na
Mchungaji Getrude Lwakatare wote wa CCM pamoja na mfanyabiashara maarufu jijini
Dar es Salaam Robery Mugishagwe wametajwa kuwa vinara wa uvamizi na uuzaji wa
viwanja jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, naye ametajwa kumkingia kifua mmoja
wa wavamizi wa viwanja kwa kumuwekea dhamana alipofikishwa polisi.
Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais,
Dk. Tereza Huviza ndiye aliyewataja vigogo hao jana jijini Dar es Salaam,
alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maliasili,
Ardhi na Mazingira, iliyokwenda kutembelea ofisi za Baraza la Mazingira
(NEMC).
Huvisa alikuwa akihofia kutaja majina ya vigogo
hao, lakini Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, alimkasirikia na kumhoji
ni nani hapa nchini aliye juu ya sheria kiasi cha kumfanya aogope kumtaja licha
ya kuvunja sheria.
Lembeli alimtaka Waziri Huvisa kuyataja majina
hayo kwani akiendelea kuwahofia watu wa aina hiyo, wataendelea na uvamizi huo na
watakapofika 100 wenye tabia hizo nchi haitatawalika.
“Huna sababu ya kuogopa kuwataja watu waovu,
kamati hii ina mamlaka kisheria…usihofie chochote, wataje tujue namna ya
kuwashughulikia,” alisema Lembeli.
Shinikizo hilo la Lembeli liliungwa mkono na
wajumbe wote wa kamati hiyo waliomuhakikishia usalama Waziri Huvisa aliyeonekana
kuwa na hofu wakati akiulizwa maswali.
Baada ya kuhakikishiwa usalama, alianza kumtaja
Dewji ambaye alisema anashinikiza kupewa eneo la ufukwe karibu na zilipo ofisi
za ubalozi wa Urusi hapa nchini huku akijua ni kinyume cha sheria.
Waziri huyo alisema vielelezo walivyonavyo
wizarani vinaonyesha kwamba Dewji alikinunua kiwanja hicho mwaka 1995, lakini
kwa kuwa eneo hilo liligundulika kuwa na mikoko, Rais Benjamin Mkapa alifuta
rasmi hati yake mwaka 1998.
Alibainisha kuwa baada ya kufutwa kwa hati ya
kiwanja hicho, mbunge huyo alipeleka maombi tena wizarani ambako alikumbushwa
namna kilivyotenguliwa, lakini bado akawa king’ang’anizi kwa kumtumia watu na
baadhi ya wabunge.
Waziri Huvisa alisema miongoni mwa wabunge
waliotumika kushawishi Dewji arejeshewe kiwanja hicho ni pamoja na Diana Chilolo
(Viti Maalumu - CCM). Hata hivyo hadi sasa hawajafanikiwa.
“Mimi nimeendelea na msimamo wa kumkatalia
Dewji. Kiukweli ndugu zangu wenye watu wenye nguvu kifedha na madaraka ndio
wanaochangia mambo kutokwenda sawa kwenye sekta ya ardhi,” alisema.
Nyumba ya Lwakatare
Katika mkutano huo, pia suala la kubomolewa kwa
nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum, Mchungaji Lwakatare lilizusha majadala mkubwa.
Wajumbe wa kamati hiyo walimbana Waziri Huvisa ili azungumze kwanini
hajabomolewa.
Hata hivyo, Waziri Huvisa alisema hawezi
kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa kesi yake ipo mahakamani na anashangazwa na
danadana za kesi hiyo kila inapotajwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM),
alisema kuwa jengo la mbunge Lwakatare limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa
kutobomolewa hali inayotoa tafsiri ya upendeleo wa kimatabaka.
Wengine watajwa
Waziri Huvisa pia alimtaja mfanyabiashara
maarufu Mugishagwe, aliyetakiwa kubomolewa jumba lake maeneo ya Kawe, lakini
kushindikana baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Rutabanzigwa, kuingilia kati na kumuwekea dhamana.
Alisema wizara yake imeshindwa kubomoa nyumba
ya mfanyabiashara huyo kwa kuwa alipokamatwa na polisi, Rutabanzibwa alimwekea
dhamana jambo lililozua utata.
Waziri huyo alisema kutokana na dhamana hiyo,
hivi sasa anafanya taratibu za kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Anna Tibaijuka walizungumze.
Alisema kutobomolewa kwa nyumba ya Mugishagwe
kumesababisha malalamiko kwa wananchi ambao nyumba zao zilibomolewa katika
maeneo kama aliyojenga mfanyabiashara huyo.
Wataka mahakama za mazingira
Wajumbe wa kamati hiyo wakichangia hoja
mbalimbali za kuboresha uendeshaji wa NEMC, walitaka kuanzishwa kwa mahakama ya
mazingira kwa kuwa sheria zinaonekana kukinzana inapotokea kesi ya
mazingira.
“Hadi sasa tayari tuna Mahakama ya Ardhi na ile
ya Kazi, kwa nini tusione ni wakati wa kuwa na Mahakama ya Mazingira ili
kuepusha mlolongo wa kuendesha kesi zinazohusu mazingira?” alihoji Mbunge wa
Magomeni Zanzibar, Mohamed Amour Chomboh.
Mbunge Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (CHADEMA)
alisema rushwa miongoni mwa watendaji wa serikali imekuwa kikwazo cha utunzaji
wa mazingira na kushauri kwamba ili kujenga kizazi kitakachothamini mazingira,
elimu itolewe kuanzia shule za awali.
Naye Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Boniveture Baya,
alizitaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na kutoeleweka
vizuri kwa usimamizi wa sheria kwa watendaji na wananchi.
Alisema wakati mwingine wamekuwa wakishindwa
kesi kutokana na watendaji wao kukurupuka kutoa uamuzi kwa sababu ya
kutozifahamu vizuri sheria.
Aliitaja changamoto nyingine ni mwingiliano wa
sheria na wizara ambazo wamekuwa wakifanya nazo kazi, ambako kila moja inatoa
kibali kwa wakati wao hivyo inapokuja suala la mazingira unakuta linawadondokea
wao.
Rasilimali fedha nayo imetaja kuwa kikwazo kwao
kwani hii huwafanya kushindwa kwenda kufanya ukaguzi maeneo mbalimbali na
kubomoa majengo ambayo yamejengwa kinyume na taratibu ikiwemo hoteli ya Coco
Beach, ambayo hadi sasa ipo kutokana na kokosa fedha za kuibomoa.
Pia alionekana kukerwa na kutokuwepo kwa mfumo
mahususi kwa ajili ya utupaji wa taka ngumu za viwandani hususani katika Jiji la
Dar es Salaam ambako kutokana na kujisimamia wenyewe kwa sasa wamekuwa wakikiuka
sheria za mazingira.
Chanzo Tanzania
daima
No comments:
Post a Comment