Familia ya watu watatu akiwamo baba, mama na mtoto wa miezi
saba, wameuawa kikatili usiku wa kuamkia jana Kata ya Buhongwa, Kijiji
cha Ihila,Wilaya ya Nyamagana, mkoani hapa.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia miili ya
marehemu hao ikiwa sakafuni, huku imetapaa damu. Hadi sasa haijafahamika
sababu ya watu hao kuuawa.
Waliouawa ni Jonas Luhinga, Rusia Jonas na mtoto Eliud Jonas.
Akisimulia tukio hilo, mtoto wa marehemu, Debora
Jonas (12), alisema tofauti na baba, mama yake na mdogo wake ambao
wameuawa, kulikuwa na mgeni nyumbani kwao kwa muda siku tatu ambaye
asubuhi ya tukio alitoweka.
Debora alisem saa 10:00 usiku, akiwa amelala na
mdogo wake ghafla alianza kulia sana na kumbembeleza, baada ya muda
mgeni huyo aliingia chumbani kwake na kumwomba mtoto huyo ili ampeleke
chumbani kwa mama yake.
Alisema alimpatia mtoto huyo na yeye kulala mpaka
asubuhi na kwamba, aliamka kwenda kufungua mlango wa chumbani kwake na
kukuta umefungwa kwa nje ndipo alipoanza kuomba msaada kwa kupiga kelele
na majirani walikwenda kufungulia.
“Nilipofika mlangoni nilijaribu kuufungua bila mafanikio, baadaye niligundua umefungwa kwa nje,” alisema Debora.
Alisema baada ya kufunguliwa aliona maiti ya baba
yake ikiwa sebuleni, huku ikiwa imechinjwa na alikimbia chumbani kwa
mama yake na alimkuta amekufa na mdogo wake huyo wa miezi saba.
Pia, tukio hilo lilishuhudiwa na majirani waliokwenda kumfungulia mlango.
Debora alisema alikimbia chumbani kwa wazazi wake
moja kwa moja akiwa na majirani hao na kukuta miili ya mama na mdogo
wake ikiwa chini, hakukuwa na damu bali waliona kamba ikiwa pembeni yao
na kuhisi huenda ndiyo ilitumika kumnyongea mama na mtoto wake.
Kuhusu mgeni ambaye alikaa nyumbani kwao kwa siku
tatu, alisema alikuwa hamfahamu zaidi ya kumtambua kwa jina moja la
Lameck na kwamba, muda mwingi alikuwa akimwona anaongea na baba yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Erenst Mangu,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, polisi wanafuatilia
waliohusika na mauaji hayo.
-MWANANCHI
Akizungumza eneo la tukio, Ofisa Upelelezi Makosa ya Jina Mkoa
Mwanza, Joseph Konyo, alisema waliouawa ni familia ya Jonas Luhinga.
Konyo alisema ni mapema kwa polisi kuzungumzia mauaji hayo kwamba, watakapokuwa tayari watatoa taarifa.
Baadhi ya wananchi walisema hivi sasa upokeaji wa
wageni unatakiwa kuratibiwa kama ilivyokuwa zamani, mwenyeji akitakiwa
kutoa taarifa kwa mjumbe wa nyumba kumi.
Walidai inawezekana mgeni huyo akawa amehusika na muda aliokaa hapo alikuwa anasoma mazingira ya nyumbani.
Pia, walitaka ulinzi shirikishi kuimarishwa kwa
sababu inawezekana wakati mauaji hayo yalipokuwa yanafanyika, kungekuwa
na doria ingeweza kusaidia. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa
wakipinga kushiriki ulinzi shirikishi, huku wakidai kazi hiyo inatakiwa
kufanywa na polisi.
-MWANANCHI