KUKITHIRI kwa
rushwa miongoni mwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi nchini,
kumesababisha silaha ndogondogo hususan bastola kumilikiwa na watu wasio
na sifa nchini.
Uchunguzi wa kina wa gazeti hili katika mikoa mbalimbali nchini
ikiwamo iliyopo mipakani inaonyesha kuwa, bastola zinamilikiwa na watu
bila ya kufuata taratibu na nyingine zikitumika kwa ajili ya kufanyia
uhalifu.
Hivi sasa hata vibaka ambao awali walikuwa wakitumia visu na mbao za
misumari kupora mali za watu, sasa wanafanya uhalifu huo kwa kutumia
bastola. Mbali ya vibaka kumiliki bastola, wahamiaji haramu walioko
ndani ya mipaka ya Tanzania inayopakana na Rwanda, Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, wanadaiwa kuingiza silaha nzito, ambazo
zinatumika kwa ajili ya matukio ya kihalifu.
Jinsi silaha zinavyopatikana
Uchunguzi unaonyesha moja ya njia ambayo imekuwa ikitumika watu
wasiokuwa na sifa kupata bastola au bunduki ni kutumia mawakala au
baadhi ya maofisa polisi, waliopo katika mikoa mbalimbali ambao
huwatafutia vibali vya kumiliki. Utaratibu wa kawaida ni kwamba waombaji
wanaotaka kumiliki silaha ni lazima wajadiliwe katika kamati za ulinzi
na usalama za mtaa au kijiji, wilaya na mkoa na kuhojiwa ili
kujiridhisha kama mwombaji ana sifa.
Mkoa wa Kilimanjaro
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya vijana wadogo
wakiwamo wafanyabiashara, wana vibali vya kumiliki bastola mkoani
Kilimanjaro na hawakupitia mchakato huo.
“Unataka kibali cha kumiliki bastola? Una milioni moja na nusu
nikuunganishe na jamaa Dar anakufanyia process (mchakato) zote
anakuletea kitabu,”alisema kijana mmoja jina tunalihifadhi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, baadhi ya maofisa wa Jeshi la
Polisi makao makuu na wale waliopo mikoani, wamegeuza suala la
kumilikisha watu silaha kama mradi wa kujitajirisha.
“Tatizo la nchi hii ni corruption (rushwa) kwa sababu unajiuliza hivi
hawa vijana wadogo kabisa wanamiliki bastola na hawakujadiliwa kwenye
kikao chochote,”alidokeza mfanyabiashara mmoja.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wapo wanaojiita wafanyabiashara, lakini
ni matapeli wa kimataifa nao wamepewa vibali vya kumiliki bastola na
wakati mwingine huzionyesha waziwazi wakiwa baa.
“Ufyatuaji wa risasi siku hizi umekuwa holela…ninavyofahamu ukifyatua
hata risasi moja, lazima uandikishe maelezo polisi ulifyatua kwa sababu
zipi siku hizi lakini hilo halifanyiki,” ilidokezwa.
Inadaiwa kuwa kutokana na kuwapo kwa ulegevu wa vyombo vya dola
hususan Polisi, baadhi ya wamiliki wa bastola hizo wamekuwa
wakizikodisha kwa majambazi ambao huzitumia katika uporaji.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ulegevu huo katika kudhibiti matumizi ya
silaha, kumetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki kukodisha bastola zao na
kurudishiwa baada ya matukio pasipo kugunduliwa.
Dar es Salaam
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa kuongezeka kwa idadi
ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria jijini Dar es Salaam,
kumeongeza matukio ya uhalifu. Baadhi ya watu ambao wapo karibu na
maofisa wa polisi makao makuu wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwatafutia
watu vibali vya kumiliki silaha.
Watu hao wamekuwa wakijipatia Sh600,000 hadi Sh900,000 kwa kibali kimoja cha kumiliki silaha.
Hali hiyo imesababisha wahalifu wengi wakiwamo vibaka mitaani kumiliki silaha ambazo wanazitumia kupora watu mitaani.
Mussa Radhamn Mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam anasema hali ni
mbaya, hivi sasa hata vijana wasiokuwa na kazi wanamiliki silaha.
Alisema hivi sasa huwezi kupita uchochoroni kuanzia saa 4:00 usiku,
lazima utakutana na vibaka wakiwa na bastola.
Wahamiaji haramu
Mkoa wa Kagera
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wakazi wa
Wilaya ya Ngara alisema kuwa silaha nyingi hasa bunduki za rashasha (sub
machine gun) zinanunuliwa nchini Burundi.
“Wakati kambi za wakimbizi za Lukole zikifanya kazi, silaha zilikuwa
zikipatikana kwa wingi, lakini kwa sasa kwa kuwa wakimbizi hao
wameondoka, silaha zinafuatwa hukohuko,” alisema na kuongeza:
“Kuna watu wana uhusiano na wenyeji wa Burundi, basi wanaziagiza tu…
bunduki moja ya SMG ni kama Sh200,000 wanakuletea. Unajua kule kwa sasa
kuna njaa kali kwa hiyo yale makundi ya waasi yalikuwa na silaha nyingi
hayana jinsi ila kuziuza ili kujikimu kimaisha.”
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Uhamiaji katika mpaka wa
Rwanda na Tanzania (Rusumo), Mahirande Samuel alisema ni vigumu
kudhibiti wahamiaji haramu hasa katika mpaka wa Burundi kwani ni mkubwa
na uwezo ni mdogo. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip
Kalangi alisema wahamiaji hao wamekuwa wakishiriki katika matukio ya
uhalifu wakishirikiana na wenyeji.
“Wahamiaji haramu wamechangia sana katika matukio ya uhalifu.
Wanaharibu mazingira kwa kuchoma misitu, kuchoma mkaa, kupasua mbao na
ujangili. Tunafaya juhudi kutekeleza agizo la Rais la kuwaondoa nchini
na kazi inaendelea vizuri,” alisema na kuongeza:
“Hadi sasa tumeshakamata silaha aina ya bunduki za gobori 50 ambazo
zimesalimishwa, ila wanaosalimisha hatuwajui maana huzitupia kwa
viongozi wa vijiji na kukimbia. Silaha tulizokamata ni mbili ambazo ni
SMG ikiwa na risasi 70 na gobori moja.
Akizungumzia tukio la Juni 15, mwaka huu, ambapo mabasi mawili
yalitekwa na majambazi na kuwapora abiria katika pori la Kasindaga,
Kamana Kalangi alisema bado uchunguzi unafanyika, lakini kuna kuhusika
kwa wahamiaji haramu wakishirikiana na wenyeji.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Fabian Massawe alisema kuwa majeshi ya
Tanzania kwa sasa yanajipanga kwa ajili ya operesheni ya kuwaondoa
wahamiaji haramu mkoani humo.
Kwa sasa majeshi yetu yanajipanga kwa ajili ya operesheni, alisema na kuongeza:
Kama Serikali itasaidia tunataka operesheni hii iwe endelevu, ila
hatuwezi kuweka kambi za jeshi mipakani kwa sababu sheria za kimataifa
haziruhusu. Operesheni hii ni kwa wahamiaji wa nchi zote
zinazotuzunguka. Nashangaa Rwanda peke yao wanalalamika.
Mkoa wa Mwanza
Uchunguzi unaonyesha kuwa watu wengi wamepata silaha kwa njia ya
haramu. Baadhi ya watu wamenunua kutoka kwa wakimbizi na wengine
wakipata vibali vya kumiliki kupitia kwa mawakala au maofisa wa polisi
wasiokuwa waaminifu.
Lugwecha Makune Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, alisema kuwa hali ya
uhalifu mjini Mwanza hivi sasa inatisha. Alisema kuwa hivi sasa wahalifu
wengi wanatumia bastola kupora watu mitaani tofauti na zamani walikuwa
wakitumia mapanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alipotakiwa
kuzungumzia hali hiyo alisema yupo nje ya ofisi atalitolea ufafanuzi
baadaye. Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la kuwarudisha
makwao wahamiaji hao, huku idadi yao ikifikia zaidi ya 10,000 waliorudi
kati ya 50,000 wanaokadiriwa kuwepo nchini.
Wiki hii Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema operesheni ya
kuwandoa kwa nguvu wahamiaji waliobaki itakuwa ya kushtukiza.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa
kuzungumzia suala hilo, alisema atafutwe baadaye. Hata hivyo,
alipopigiwa simu alisema afuatwe ofisini kwake kulizungumzia, lakini
alipofuatwa alisema alikuwa na kazi nyingi.
Maoni ya watu mbalimbali
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa
Humprey Moshi alisema kuongezeka kwa matukio ya watu wanaotumia silaha,
ni matokeo ya ukosefu wa amani katika nchi za jirani ambao umesababisha
wahalifu kuingia nchini kwa njia za kificho wakiwa na silaha.
Moshi anasema ukiritimba katika upatikanaji silaha serikalini si
sababu ya watu kununua silaha kwa njia za siri, bali ukosefu wa ajira
kwa vijana na mmomonyoko wa maadili ndivyo vilivyoifikisha hali ya
kutokuwa na usalama mahali ilipo leo.
“Taratibu za upatikanaji wa silaha serikalini siyo tatizo, migogoro
katika nchi jirani ndiyo inayofanya silaha zipatikane kwenye mipaka
yetu,” anasema.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete
alisema suala la upatikanaji silaha haramu si la Tanzania peke yake,
nchi inapaswa kushirikiana na nchi zote na kushauri serikali za mitaa
kushirikiana na vyama vya siasa kudhibiti tatizo hilo.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence
Mpangala alisema upatikanaji wa silaha kiholela unatokana na kubadilika
kwa mfumo wa maisha na kwamba baadhi ya watu siku hizi wanamiliki silaha
kama njia mojawapo ya kujipatia fedha kwa njia za uhalifu.
“Kuna mianya mingi ya kumiliki silaha kinyume na sheria, Serikali imeweka sheria ambazo ni lazima zifuatwe,” alisema.
Chanzo: Gazeti Mwananchi
No comments:
Post a Comment