Hatua ya Jaji Mutungi, imekuja siku chache baada ya CCM kumtumia Balozi wa China, Dk. Lu Youping katika shughuli za kisiasa mkoani Shinyanga wiki iliyopita.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, ilisema suala la ushiriki wa raia wa kigeni ikijumuisha wanadiplomasia katika shughuli za kisiasa nchini, halikubaliki.
Alisema ofisi yake, inaunga mkono kwa dhati hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo.
"Tamko la Serikali limezingatia sheria na wajibu wa wanadiplomasia, wakati wa uwepo wao hapa nchini, mimi nikiwa mlezi wa vyama vya siasa, ninakemea kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi wa China katika shughuli za kisiasa," alisema Jaji Mutungi.
Alisema katika tukio hilo, CCM kuruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake ni dhahiri limezua hali ya taharuki kwa wananchi, japo sheria ya vyama vya siasa kwa upande wake iko kimya katika suala hilo.
"Naviasa vyama vya siasa kwa ujumla wake, kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
"Napenda kuujulisha umma kwamba, ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa wakati huu ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya sheria husika ya vyama vya siasa, ambayo imebainika kuwa na upungufu....lengo ni kukabiliana na changamoto zilizopo likiwemo suala hili," alisema Msajili, Jaji Mutungi katika taarifa yake.
Jaji Mutungi, aliongeza sasa hivi ofisi yake inaendelea kukusanya maoni ya wadau katika jitihada za kufanikisha marekebisho ya sheria hiyo.
Suala la CCM kumshirikisha Balozi wa China katika masuala ya kisiasa, lilizua mjadala mkubwa hali iliyosababisha CHADEMA kutoa tamko na kuandika barua ya malalamiko UN wakitaka aondolewe kwa kupoteza sifa za kuwa balozi, baada ya kuvunja mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1961 unaosimamia nchi na nchi.
CHADEMA waliandika barua nyingine kwenda Serikali ya China na Tanzania, wakitaka msimamo na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya balozi huyo kuvunja mkataba huo ibara ya 41(1-3), kinachokataza balozi kujihusisha na siasa katika Taifa ambalo yuko.
Chadema imesema inalaani kitendo hicho na itachukua hatua kwenda Umoja wa Mataifa na pia kupata maelezo toka Serikali ya China kama imemtuma balozi huyo kujihusisha na mambo ya siasa za ndani za vyama au kuiwakilisha nchi.
Akijibu tuhuma hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alichofanya balozi huyo ni kitendo cha kuungwa mkono, maana alikuwepo kwa nia ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa zao la Pamba katika Mkoa wa Shinyanga.
Alisema uwekezaji kutoka China, utasaidia kuondoa tatizo sugu la ajira, kupanda kwa bei ya zao la pamba ambacho kimekuwa kilio kikubwa cha wakulima pamoja na ujengwaji wa viwanda vya nguo na kuchuja mafuta.
Hivyo ni vema kumpongeza balozi huyo na kuunga juhudi za CCM za kuwatafuta wawekezaji wa nje, badala ya kusingizia uvunjaji wa Mkataba wa Vienna ili kupata umaarufu wa kisiasa. Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment