ASKARI
wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza, ameonekana shujaa
katika tukio la uvamizi lililotokea katika jengo la maduka la Westgate
jijini Nairobi Kenya baada ya kufanikiwa kuokoa watu 100 waliokuwa ndani ya jengo hilo.Baadhi ya wakenya waliopoteza jamaa zao katika shambulizi la Westgate.
Askari
huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa
ni sababu za kiusalama, wakati wavamizi hao wanavamia jengo hilo siku
ya Jumamosi, naye alikuwemo ndani ya jengo hilo akinywa kahawa.
Kwenye
baadhi ya mitandao, askari huyo ameonekana akiwasaidia wanawake wawili
huku akiwa ameweka bastola kwenye suruali yake, ingawa sura yake
imefichwa.
Habari
zinasema kuwa, askari huyo ameonekana shujaa kwani licha ya hali tete
iliyokuwa ndani ya jengo hilo, aliweza kuingia na kutoka zaidi ya mara
12 akiwaokoa baadhi ya watu waliokwama ndani ya jengo hilo lenye maduka
na migahawa mbalimbali.
“Alichofanya ni kitendo cha kishujaa sana, alikuwa akinywa kahawa na baadhi ya rafiki zake wakati wavamizi walivyoingia.
Alirudi
ndani mara 12 na kufanikiwa kuokoa zaidi ya watu 100. Fikiria kuthubutu
kurudi ndani huku akijua kabisa jinsi hali ilivyo ndani ya hilo jengo,”
baadhi ya mashuhuda walinukuliwa.
Habari
zaidi zinaeleza kuwa, askari huyo wa Uingereza anafanya zaidi shughuli
zake Kenya na nje ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia raia wa
nchi yake wanaojishughulisha na mambo mbalimbali.
Agosti
mwaka huu, gazeti la Daily Mirror liliripoti kuwa kikosi maalumu cha
SAS na askari maalumu wa kupambana na ugaidi, wameanza kumtafuta
Samantha Lewthwaite, Mwanamke anayetajwa kuwa ni raia wa Uingereza
anayedaiwa kuwa gaidi ambaye pia anashirikiana na kundi la Al-Shabaab.
Mwanamke huyu mjane anayetajwa kuwa ni gaidi, inasemekana pia alishiriki kupanga na kutekeleza uvamizi mjini Nairobi.
Kikosi
hicho cha SAS, kinaelezwa kuwa kinafanya kazi kwa ukaribu na vikosi vya
ulinzi vya Uingereza, Kenya na vile vya nchi nyingine za Afrika
Mashariki.
Habari
juu ya askari huyo zimekuja wakati milio ya risasi ikizidi kusikika
ndani ya jengo hilo, huku maofisa wa usalama wa nchi hiyo wakisema kuwa
wamedhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, bado
zaidi ya watu 10 wanashikiliwa ndani ya jengo hilo kama mateka.
‘Tumeshadhibiti
sehemu yote ya jengo, tuko hapa kuhakikisha tunawaadhibu vya kutosha
hawa watekaji,” Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Kenya, IGP David Kimaiyo
aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter. BBC