Huyu si mwingine bali ni Mark Paulo Kishiwa
ambaye kitaaluma ni daktari, aliyewahi kufanya kazi Hospitali za Kasulu,
mkoani Kigoma na Bugando mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua
humwishia akiwa maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona mara kadhaa utamkuta akiimba nyimbo
zisizo rahisi kuzielewa kutokana na hali anayonekana kuwa nayo ya
matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa, hugeuka kuwa msaada kwa wengi;
madaktari wa MNH ambao huomba ushauri kwake, wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na wagonjwa ambao hutaka ushauri
pia.
Dk Kishiwa anasema: “Naikumbuka Aprili 26, 1981,
ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, ndipo nilianza kuugua. Nilijikuta nikifanya
vitu visivyo vya kawaida.
Nilimwaga maji ovyo ndani, nilimwaga nguo na vitu
mbalimbali, kila kitu kilikuwa ovyo. Baada ya muda niligundua kufanya
vitu siyo vya kawaida…Hivyo ndivyo nilivyoanza kuchanganyikiwa na hali
hii imenitokea mara kwa mara.”
Aliongeza: “Yaliponitokea hayo, nilikuwa nikifanya
kazi mkoani Kigoma katika hospitali iliyopo wilayani Kasulu (hakuitaja
jina) ndipo kilikuwa kituo changu cha kazi.”
Pamoja na Dk Kishiwa kuwa na matatizo ya akili,
imethibitika kuwa baadhi ya madaktari wa MNH wamekuwa wakikimbilia kwake
kupata ushauri, lakini kubwa ni lile la kufundisha masomo ya ziada kwa
baadhi ya wanafunzi MUHAS.
Pia amekuwa akifuatwa na watu wanaomfahamu hasa
wanawake wakimwomba ushauri hata kuwaandikia dawa kutokana na maradhi
waliyonayo. Mwandishi wa habari hii ni mmoja wa waliopata ushauri wa
kitabibu kutoka kwa Dk Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi wa wiki kadhaa katika eneo la MNH,
nyumbani kwake Chamazi na hata katika familia yake, umethibitisha kwamba
Dk Kishiwa licha ya kuwa mgonjwa wa akili bado ni msaada mkubwa kwa
watu wengi.
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza
mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu
wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo,
hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa wakati fulani, Dk
Kishiwa anakuwa katika hali ya kawaida na kuweza kutoa ushauri, hata
kutibu kwa kuwaandikia dawa wagonjwa akiwa eneo hilo la Muhimbili.
No comments:
Post a Comment