Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 15, 2013

HII KUBWA KULIKO:.MBUNGE BONGO ASAKWA KWA WIZI WA GARI YA WAZIRI, SOMA MKASA MZIMA HAPA


Bifu zito lipo hivi sasa kati ya Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani. Makalla anamtuhumu Ngonyani a.k.a Profesa Maji Marefu kuwa alichukua gari lake aina ya BMW X5 kisha akatokomea nalo kisha akawa anampigia simu hapokei na hata akimtumia SMS hajibu. Kutokana na malalamiko hayo, hivi sasa Maji Marefu anasakwa na polisi wa Kituo cha Kati (Central), Dar es Salaam, tuhuma zikiwa ni wizi wa kuaminiwa, shauri lipo kwenye kitabu cha ripoti za polisi (Report Book ‘RB’) kwa namba CD/RB/13336/2013. NYEUPE NA NYEUSI YA TUHUMA ZENYEWE
Nyeupe na nyeusi (black and white) ya tuhuma hizo, inawekwa wazi na ‘sosi’ wetu ambaye aliliibia siri gazeti hili kwamba sakata kati ya Maji Marefu na Makalla lilianza tangu Julai, mwaka huu wakati waheshimiwa hao walipokuwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
“Maji Marefu aliomba gari la Makalla ili alitumie kwa mizunguko ya siku moja tu lakini hakurudisha,” kilisema chanzo chetu. “Mgogoro mkubwa ulianza kuibuka kuanzia hapo na mpaka leo waheshimiwa hao hawazungumzi kwa salamu wala kutakiana heri.” Chanzo chetu kiliendelea kusema: “Siku ya kwanza tu ilipopita, Makalla alimpigia simu Maji Marefu akawa hapokei, akimtumia SMS hajibu. Kwa kifupi Makalla alipoteza mawasiliano na Maji Marefu lakini aliendelea kusubiri kwa sababu anajua ni mtu wake.” Habari zaidi zinasema kuwa kilipita kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja bila ya Makalla kumpata Maji Marefu kwenye simu lakini walikutana katika Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioketi kati ya Agosti 27 hadi Septemba 13, mwaka huu, Dodoma. “Walipokutana Makalla alimuuliza Maji Marefu gari lake lipo wapi? Maji Marefu alimjibu alilikabidhi Lamada Hotel, Dar es Salaam,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza: “Unajua makabidhiano ya lile gari yalifanyika Lamada Hotel, kwamba angelirudisha baadaye lakini ikawa kimya. “Hata hivyo, Makalla aliona siyo kesi kubwa, akafuatilia Lamada Hotel, menejimenti ya hoteli hiyo ilijibu kuwa gari hilo halijapelekwa pale. Vilevile baada ya kuzungumza siku hiyo, Maji Marefu alitoweka na bungeni hakuonekana tena. “Baada ya kupata majibu hayo kutoka kwa Profesa Maji Marefu na Lamada, Makalla alifungua mashitaka Central, akidai kuibiwa gari lake na Maji Marefu.” MAKALLA AFUNGUKA
Makalla ambaye ni Mbunge wa Mvomero (CCM) alipozungumza na mwandishi wetu alikubali kila kitu kisha akafunguka: “Niliomba polisi wanisaidie maana kwa hali iliyokuwepo ni kama nilikuwa nimeshatapeliwa. Vilevile niliripoti kwa Kamanda Mohamed Mpinga (mkuu wa kikosi cha usalama  barabarani) ili naye awaambie vijana wake wanisaidie kunitafutia gari langu.
“Nilimpa alama zote, rangi na namba za usajili. Oktoba Mosi, mwaka huu, ikiwa ni karibu miezi mitatu imepita tangu nimpe gari, polisi Tanga waliliona gari langu likiwa linaendeshwa na mheshimiwa Ngonyani (Maji Marefu) kwenye msafara wa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal. “Nilimtumia SMS kumwambia kuwa gari langu ameonekana nalo katika msafara wa makamu wa rais. Polisi Tanga walitaka kumkamata lakini nikaomba aachwe kwanza, kukamatwa katika msafara wa makamu wa rais angeona amedhalilishwa. “Nilimuomba baada ya msafara akalikabidhi gari kwa RPC Tanga kwa sababu linatafutwa na polisi. Akaniambia hawezi kulipeleka polisi kwa sababu tulikabidhiana vizuri. Nikamwambia sitaki kwa sababu alikuwa ananizungusha sana kunirudishia gari langu, mara aseme amelipeleka Lamada kumbe bado analo na wakati huohuo hapokei simu wala hajibu SMS zangu.” USHAHIDI WA SMS
MAKALLA: “Mhe. pamoja na kutopokea simu na kutojibu meseji zangu, nakujulisha leo Oktoba Mosi, umeonekana na gari langu kwenye msafara wa makamu wa rais. Polisi walitaka wakukamate nikashauri wasubiri umalize mkutano. Kwa meseji hii naomba kesho asubuhi ukakabidhi gari langu kwa RPC Tanga, bila kukosa. Utamkuta ndugu Rajabu alipokee gari hilo baada ya ukaguzi mbele ya RPC.”
MAJI MAREFU: “Sawa nimekuelewa, yote ni makosa yangu na hii ni mali yako ila gari hatukupeana polisi, ungeniambia ulipo nikuletee.” MAKALLA: “Sitaki umenizungusha sana, nilikukabidhi kwa heshima lakini umegeuka adui, hupokei simu huu ni mwezi wa tatu.” MAJI MAREFU: “Ok nitafanya hivyo.” MAKALLA ANAENDELEA “Hakupeleka gari kwa RPC Tanga kama nilivyomtaka. Zilipita kama siku tatu, ndipo mtu mmoja akaenda kulitelekeza gari langu Lamada Hotel usiku. Walinzi walimuuliza yule mtu aliyetekeleza lile gari kwa nini anaacha gari na anakimbia? Hakujibu, akarukia kwenye pikipiki ambayo ilikuwa inalifuata lile gari kwa nyuma kisha akatoweka. “Uongozi wa Lamada baada ya kuliona gari langu walinipigia simu, wakanijulisha nami nikapiga simu polisi, wakaenda kulichukua. Mpaka sasa gari lipo polisi central, wanasubiri kumkamata Mhe. Ngonyani ili kesi iendelee mbele.” KAZI YA UWAZI
Gazeti hili baada ya kuzungumza na Makalla, lilikwenda kufanya upekuzi wake central na kubaini kwamba kesi hiyi ipo na madai yapo kama yalivyoelezwa.
Baada ya hapo, mwandishi wetu alimpigia simu Maji Marefu ambaye alipokea akiwa Nairobi, Kenya, na aliposomewa tuhuma dhidi yake, alijibu: “Subiri nirudi Dar, nitaeleza kila kitu.” Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo; MWANDISHI: Kuna madai kwamba ulichukua gari la Mheshimiwa Makalla, umekaa nalo miezi mitatu, kipindi chote hicho simu ulikuwa hupokei wala hujibu SMS zake.
MAJI MAREFU: Siyo kweli.
MWANDISHI: Labda ukweli ni upi.
MAJI MAREFU: Labda kwa sababu sipo Dar, nisubiri nirudi tutakaa tuzungumze.
MWANDISHI: Ungeniambia kwa kifupi tu ni kwa nini Makalla akushitaki, maana hii kesi ipo polisi, RB ipo na unatafutwa kwa tuhuma za wizi wa kuaminiwa.
MAJI MAREFU: Polisi wananitafuta mimi?
MWANDISHI: Ndiyo wanakutafuta wewe.
MAJI MAREFU: Kwa vile nipo Nairobi na wewe upo Dar, naomba usubiri tukutane kwanza ndipo nitaweza kueleza ukweli halafu ndipo mtaamua kuendelea mbele.
MWANDISHI: Sawa mheshimiwa, swali lingine wewe una ugomvi na Mheshimiwa Makalla?
MAJI MAREFU: Aah, ndiyo nikasema tukikutana ndiyo italeta picha nzuri. Kama natafutwa au kuna tukio lolote nitaeleza.
MWANDISHI: Sawa mheshimiwa, basi nijibu swali hili, wewe una ugomvi na Makalla?
MAJI MAREFU: Sina ugomvi naye.
MWANDISHI: Sasa kwa nini akushtaki kwa wizi wa gari lake?
MAREFU: Naomba tukutane nikirudi nitaongea tu.
MWANDISHI: Inasemekana hilo gari uliwahi kumwambia Makalla kwamba uliliacha Lamada Hotel lakini baadaye ukaonekana nalo kwenye msafara wa makamu wa rais Tanga. Hili limekaaje?
MAJI MAREFU: Mimi nina magari zaidi ya 15, nitakupeleka uone kama mimi nina shida ya gari. Nyumbani kwangu kuna magari ya kila aina.
MWANDISHI: Ni kweli Makalla alikukabidhi gari?
MAJI MAREFU: Subiri nirudi Dar nitaongelea hilo.
MWANDISHI: Nijibu tu hilo moja tu, alikupa au hakukupa?
MAJI MAREFU: Kwani yeye anasema nilimnyang’anya au alinipa?
MWANDISHI: Anasema alikupa.
MAJI MAREFU: Sasa subiri nirudi nitaeleza ukweli wangu.
MWANDISHI: Kwani mheshimiwa inashindikana nini kunijibu swali hili moja tu? Alikupa au hakukupa?
MAJI MAREFU: Ukweli mtaupata nikisharudi Dar.
POLISI NAKO
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alipoulizwa kuhusu kesi hiyo, kwanza alisema hajapata taarifa yoyote kuhusu sakata hilo mpaka afuatilie.
Siku iliyofuata, Kova alipigiwa tena simu akaulizwa kuhusu sakata hilo, akajibu: “Kuna mtu wa Uwazi alinipigia simu jana kuhusu hii kesi, unajua mimi ni kamishna, hii kesi ni ndogo na siyo kila kesi lazima nijibu mimi.

No comments:

Post a Comment