Kugunduliwa kwa gesi nchini kulionekana ni neema kubwa kwa Tanzania ambayo inaogelea kwenye lindi la umasikini. Lakini sasa mtazamo ni tofauti kwani wazawa wanahofu ya kutofaidika na gesi hiyo kutokana na masharti ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali.
Hofu ya Watanzania ilianza kujionyesha muda mrefu
baada ya wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuandamana kupinga gesi
inayotoka kwenye mikoa hiyo kusafirishwa jijini Dar es Salaam badala ya
kutumika huko huko kwa lengo la kuwaletea utajiri.
Baada ya Serikali kuyazima maandamano hayo, sasa
utata umeigubika sekta binafsi inayohusisha Watanzania wenye mitaji
mikubwa na Serikali ambayo imeweka masharti magumu ya uwekezaji
yanayofanana na yale ya wawekezaji wa nje.
Akizindua awamu ya nne ya ugawaji wa vitalu vinane
vya gesi vilivyopo katika ukanda wa kina kirefu baharini na ukanda wa
Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais
Jakaya Kikwete ametoa tahadhari akisema gharama za kuwekeza katika
utafiti na uchimbaji ni kubwa.
“Mwekezaji akishatumia gharama zake kwenye
utafiti, zitarudi endapo atapata gesi anayotafuta, lakini akikosa
hatumrudishii, nani anaweza kuingia kwenye kazi hiyo,” anasema Rais
Kikwete.
Anasema nafasi nzuri ya Watanzania kushiriki
kwenye uwekezaji wa gesi ni kununua hisa kupitia Shirika la Petroli
Tanzania (TPDC).
“Kwa sekta binafsi au mtu mmoja mmoja kuwekeza
kwenye gesi haiwezekani kwani gharama ya kuchimba kisima kimoja ni Dola
100 milioni.
“Unaweza kutafuta gesi kwa gharama kubwa, lakini
usipate na ukajikuta umeingia hasara, ndio maana Serikali ikatoa nafasi
ya TPDC kushiriki kwenye uwekezaji.
Rais Kikwete anasema sheria, mfumo na mikataba iliyopo kwa sasa hairuhusu kupata hasara.
“ Lakini baada ya wawekezaji kujirudishia gharama zao za utafiti, Serikali itakuwa inapata asilimia 75 ya faida,” anasema.
Pamoja na kauli hiyo Rais Kikwete anasema milango iko wazi kwa yeyote anayetaka ushindani wa vigezo vilivyopo.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment