UKIMUULIZA shabiki yeyote wa soka duniani, atakwambia kwa sasa kuna mwamuzi mmoja tu maarufu, Howard Webb.Sifa yake ni kuchezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi nchini Afrika Kusini mwaka 2010.
Pia hata mechi ngumu za Ligi Kuu England au Ligi
ya Mabingwa Ulaya amekuwa akipangwa kuchezesha. Sahau hilo la Webb.
Tanzania kuna mtu mmoja anaitwa Kipunje.
Huyu jamaa anaishi sehemu moja inaitwa Mwananyamala B, Mtaa wa Ujiji, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Unaweza ukashangaa, lakini huyo Kipunje ndiyo
mwamuzi ghali zaidi wa mechi za mchangani kwenye wilaya zote tatu za Dar
es Salaam ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni.
Ndiye mwamuzi pekee anayeweza kufanya kitu ambacho hata Webb au mwamuzi yeyote wa Fifa hawezi kuthubutu kukifanya.
Ndiye mwamuzi wa Dar es Salaam, ambaye ni maarufu
zaidi katika mechi za mchangani na anayechezesha mechi yoyote
iliyoshindikana kutokana na vurugu za mashabiki au wachezaji, haogopi
chochote ndiyo maana thamani yake ipo juu tofauti na wengine.
Ukikutana naye ana kwa ana mtaani huwezi kuamini
kwamba ndiye Kipunje anayeogopwa na wakorofi walioshindikana katika
Wilaya ya Kinondoni.
Unajua kwa nini anaogopwa? Ni hivi, anachezesha
mechi akiwa ametinga na silaha za jadi kiunoni ndani ya bukta yake.
Silaha hizo ni panga refu upande wa kushoto na shoka dogo upande wa
kulia.
Nani atamsogelea?
Anavyojiandaa
Anavaa jezi zake bukta, fulana, soksi na raba
kisha anafunga kamba ya katani kiunoni halafu anachomeka panga kushoto
kwake na shoka kulia.
Anachukua kadi zake ile ya njano anaweka mfuko wa
kushoto kifuani kwenye fulana yake na ile nyekundu anaichomeka kulia
ananyoosha viungo anaingia kazini.CHANZO GAZETI LA MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment