Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 29, 2013

TEMESA NA TBA ZATAHADHARISHWA

Picha_1_d2c43.jpg
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya (watatu kutoka kulia) wakiwa pamoja na viongozi wengine mbali mbali wakiwa katika mkutano wa pamoja na wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi mkoani Kigoma.
Picha_2_72096.jpg
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Eng. Dr. William Nshama (aliyesimama) akitoa maelezo katika mkutano wa pamoja wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi mkoani Kigoma.
Picha_3_0071c.jpg
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TEMESA Brigedia Generali Mstaafu Berth-Rafa Mashauri (aliyesimama) akitoa maelezo katika mkutano wa pamoja wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi mkoani Kigoma.
Picha_4_48496.jpg
Wawakilishi kutoka Tanroads, TEMESA na TBA wakiwa katika mkutano wa pamoja wa Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake katika mkoa wa Kigoma.
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) pamoja na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) zimetahadharishwa kubadili mfumo wake wa kujiendesha vinginevyo zitaendelea kukosa kuaminika kwa wateja wao. Hayo yameelezwa katika kikao ambacho Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya walipokutana na Wafanyakazi kutoka Taasisi zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi mkoani Kigoma.
Katika kikao hicho ilielezwa kuwa kukosa ubunifu na mawasiliano yasiyo mazuri na wateja wao kumesababisha baadhi ya taasisi za umma kuamua kutumia taratibu zisizo rasmi kwa ajili ya kupata huduma ambazo zingestahili kutolewa na wakala hizo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizotolewa na mameneja wa wakala hizo mbili mkoani Kigoma, Mkurugenzi wa Ufundi na Umeme wa Wizara ya Ujenzi Dkt. William Nshama alibainisha kuwa, ipo mikoa ambayo imejijengea jina zuri kiasi cha kutumiwa hata na sekta binafsi. Akitolea mfano wa TEMESA ameelezea kuwa karakana za wakala huo katika mikoa ya Pwani na Kagera zimekuwa zikifanya vizuri kiasi cha kuweza kujendesha zenyewe kwa kutoa huduma zenye viwango bora.
Kati ya changamoto zilizojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na taasisi nyingi kutolipa madeni yake kwa wakati kwani zipo taasisi zipo ambazo zimebainika kuwa na madeni ya kuanzia mwaka 2002. Eneo jingine lililojadiliwa katika kikao hicho ni taasisi za umma kuanza kutafuta huduma mbali mbali kutoka vyanzo visivyo rasmi ikiwa ni pamoja na kutengeneza magari katika gereji binafsi bila ya kufuata utaratibu, matumizi ya watendaji wasiosajiliwa ambao wamekuwa wakiingia mikataba kama makandarasi au wasimamizi wa miradi.
Hali hiyo ya ukiukwaji wa sheria ilielezewa kuchangiwa pia na taasisi za fedha zinazopitisha malipo huku zikitambua wazi kuwa taratibu hazijafuatwa. "Inashangaza kuona malipo yanafanyika tena kwa kutoa kipaumbele kwa huduma ambayo imefanyika nje ya utaratibu na kulimbikiza madeni kwa taasisi stahili zenye madai makubwa kama TEMESA" alibainisha Brigedia Generali Mstaafu Berth-Rafa Mashauri aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya TEMESA katika kikao hicho.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, Msajili wa Bodi ya Wahandisi Eng. Steven Mlote pamoja na Msajili wa Bodi ya Makandarasi Eng. Boniface Muhegi walibainisha wazi kuwa, kwa mujibu wa Sheria Namba 15, 16 na 17 za mwaka 1997 imeelezwa bayana kwamba ni kinyume cha sheria kwa mtu asiyesajiliwa chini ya sheria hizo kufanya kazi za uhandisi au kandarasi na yeyote anayetoa kazi kwa mtu au kampuni ambayo haijasajiliwa pia ni mvunjaji wa sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Mheshimiwa Issa Machibya, amempongeza Waziri wa Ujenzi kwa utekelezaji wa majukumu yake na hasa kwa upande wa mkoa wa Kigoma ambako miradi mingi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa. "Kwa kweli jitihada hizi ni za kuungwa mkono na mimi kwa upande wangu nitafuatilia malimbikizo hayo ya madeni kutoka kwa wahusika ili taasisi hizi muhimu zisikwamishwe katika utekelezaji wa majukumu yake" aliahidi Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Machibya.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa aliwasilisha ombi rasmi kwa Waziri wa Ujenzi kuiimarisha karakana ya TEMESA mkoani Kigoma ili iweze kuwa kitovu cha huduma katika ukanda wa magharibi wa nchi yetu.
Akihitimisha kikao hicho Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliendelea kuipongeza Tanroads kwa utekelezaji wa majumuyake vizuri. Kwa upande mwingine aliwataka TBA na TEMESA kuhakikisha kuwa wanabadilika na kurejesha imani kwa wateja wao.
"Hapa ninachokiona ni kutokuwepo kwa uwajibikaji, hamjitumi na sio wabunifu, ninataka kuona hali hii inabadilika mapema vinginevyo tutalazimika kutafuta watendaji wengine watakaoweza kusimamia kazi hizi kwa umakini zaidi" alisisitiza Waziri Magufuli.
Akizungumzia ombi la Mkuu wa Mkoa, Waziri Magufuli alimhakikishia kuwa wizara yake itaufanyia kazi ushauri huo na kuhakikisha kuwa karakana ya Kigoma inapatiwa nyenzo muhimu kuimarisha utendaji wake.

No comments:

Post a Comment