-Mkurugenzi
wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii toka Wizara ya Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Bw. George Lauwo(kushoto) Akifafanua kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani) kuhusu mchakato kuelekea matumizi ya mfumo
mmoja wa fedha, wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa idara ya
habari(MAELEZO) leo Jijini Dar Es Salaam.Kulia ni Mkurugenzi wa
Siasa,Ulinzi na Usalama Bw. Steven Mbundi.
Mkuu
wa kitengo cha mawasiliano toka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Bi. Vedastina Justinian(kushoto) akieleza kwa waandishi wa
habari(Hawapo pichani)kuhusu Mikutano ya utatu kati ya Nchi za Kenya,
Uganda na Rwanda,wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa idara ya
habari(MAELEZO) leo Jijini Dar Es Salaam. Kulia ni Afisa Habari wa Idara
ya Habari(MAELEZO) Fatma Salum.
……………………………………………………………………………..
Hivi
karibuni wananchi wengi wamekuwa wakifuatilia na kuulizia kuhusu
taarifa mbali mbali zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya hatua ya
baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Kenya,
Uganda na Rwanda kufanya mikutano ya utatu kujadili masuala ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki pasipo kuzishirikisha nchi za Tanzania na
Burundi. Mikutano hiyo inaandaliwa kupitia utaratibu wa Ushirikiano wa
nchi hizo tatu kupitia Wizara za Mambo ya Nje ya Nchi zao na sio kupitia
mfumo wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kulingana
na taarifa zilizotolewa kwa vyombo ya habari mara baada ya kukamilika
kwa mkutano wa wakuu wa nchi hizo tatu uliofanyika tarehe 24-25 Juni,
2013 huko Entebbe Uganda. Masuala yaliyojadiliwa na kutolewa maamuzi na
mwongozo wa utekelezaji ni pamoja na:
- Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Mombasa-Kampala– Kigali Km 2,784;
- Ujenzi wa Bomba la Mafuta South Sudan-Kampala-Kenya;
- Ujenzi mitambo ya kusafisha mafuta Uganda;
- Kuongeza upatikanaji wa Umeme;
- Kuanzisha Himaya Moja ya Forodha; (single customs Territory)
- Kuharakisha Shirikisho la Kisiasa;
- Vitambulisho vya Kitaifa kutumika kama Hati ya Kusafiria; na
- Visa ya Pamoja ya Utalii.
UFAFANUZI
Pamoja na kuwa Ibara ya 7(1)
(e) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
inaruhusu nchi wanachama kuwa na Ubia (Bi-lateral or Tri-lateral
agreements), ni lazima suala linaloenda kutekelezwa chini ya mfumo huo
liwe limejadiliwa na kukubalika na nchi zote wanachama.
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 27 wa Baraza la Mawaziri la
Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Arusha tarehe 31 Agosti, 2013,
ilitaka kujua hatma ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tanzania ilitaka ufafanuzi kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mambo
ambayo nchi hizo zinayajadili na kuyatolea maamuzi, bado majadiliano
yake yanaendelea katika ngazi ya Jumuiya. Baraza la Mawaziri la Afrika
Mashariki lilimtaka Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri kutoa taarifa ya
kina kuhusu mikutano hii na athari zake katika Mkutano wa 28 wa Baraza
la Mawaziri unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2013.
Katika moja
ya mikutano hiyo, Wakuu wa Nchi za Kenya, Uganda na Rwanda
walikubaliana kuharakisha uundwaji wa Shirikisho la Kisiasa baina ya
nchi hizo tatu.
Ibara ya 5(2) ya
Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeainisha hatua
za mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa ni Umoja wa Forodha,
ukifuatiwa na Soko la Pamoja, kisha Umoja wa Fedha, na hatimaye
Shirikisho la Kisiasa.
Kuanzia
mwaka 2004 kumekuwa na jitihada mbali mbali za kutaka kuharakisha
uundwaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Hii pamoja na
hatua nyingine mbali mbali ilipelekea kuundwa kwa Timu za Kukusanya
Maoni ya Wananchi juu ya pendekezo hilo. Kwa upande wa Tanzania iliundwa
timu iliyokuwa na chini ya Uenyekiti wa Professa Samweli Wangwe na
matokeo yaliyoonyesha kuwa asilimia 79.4 ya watanzania hawataki
kuharakisha uundwaji wa shirikisho. Serikali ya Tanzania daima
inazingatia maoni haya ya wananchi.
Ili
kuwawezesha wananchi kujua aina ya shirikisho linalotarajiwa kuundwa,
Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya waliiagiza Serikali ya Jumuiya kuunda
Rasimu ya Modeli ya Shirikisho. Na kwa sasa nchi wanachama wanafanya
mashauriano ya ndani kuhusiana na rasimu iliyowasilishwa.
VITAMBULISHO VYA KITAIFA KUTUMIKA KAMA HATI YA KUSAFIRIA
Itifaki ya Soko la Pamoja Ibara ya 9(2) Nchi Wanachama zilikubaliana kutumia hati halali za kusafiria (Passport)
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati hizo ni Passport ya Nchi
Mwanachama na Passport ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha,
imekubalika pia kuwa Nchi Wanachama ambazo zipo tayari kutumia
vitambulisho vya uraia kama hati za kusafiria zinaweza kuendelea kwa
kufanya makubaliano baina yao ili mradi tu vitambulisho hivyo viwe machine readable.
KUANZISHA HIMAYA MOJA YA FORODHA
Mwaka 2012 Wakuu wa
Nchi Wanachama waliridhia uanzishwaji wa Himaya Moja ya Forodha
inayotaka bidhaa zinazopitia nchi moja kuelekea nchi nyingine mwanachama
kukaguliwa na kodi kukusanywa katika kituo cha forodha cha kwanza
bidhaa inapoingia katika Jumuiya. Masuala muhimu yanayojadiliwa ni
pamoja na kuondoa dhamana (bond) kwa mizigo iliyolipiwa kodi, na
matumizi ya njia ya kisasa ya ufuatiliaji wa misafara ya mizigo
(electronic cargo tracking system) kama njia mbadala ya matumizi ya
dhamana (bond); matumizi ya dhamana moja (single bond) kwa mizigo yote
inayosafirishwa kwenda nje ya Jumuiya na mizigo ambayo haijalipiwa kodi.
HITIMISHO
Tanzania
ni sehemu ya mtangamano na nia yetu ni kuhakikisha tunatekeleza
makubaliano yetu ya pamoja kulingana na matakwa ya Mkataba wa Uundwaji
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Imetolewa na:
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
No comments:
Post a Comment