Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 19, 2013

Ukatili: Mtoto wa miaka 11 aozeshwa kwa mbuzi 13


mkwasa 0c12d

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa
Katika hali ya kawaida, binti wa miaka 11 (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili), mkazi wa kijiji cha Kongogo, Wilayani Bahi mkoani Dodoma hivi karibuni aliolewa na binamu yake, kisha ndoa yake kuvunjwa na Serikali.
Hakuna taarifa nyingi za mabinti kuolewa katika umri mdogo katika wilaya hiyo mbali ya kuwepo kwa watoto wadogo ambao huondolewa katika masomo na wengine kushindwa kupata elimu kwa sababu wazazi wao huwapeleka migodini na wengine maeneo ya mijini kutumikishwa majumbani.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, anasema wilaya yake inaongoza mkoani hapa kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vitendo vya ukeketaji wa wanawake ikiwa nayo ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.
Lakini kwa tukio hilo, lililojitokeza katika moja ya familia ya wafugaji, kunaweza kukafanya umuhimu wa kujikita katika utafiti wa kina kuliangalia suala la kuolewa katika umri mdogo lina ukubwa gani mkoani hapa.
"Hazungumzi na mtu yeyote humu ndani na unaweza kumsemesha anakuangalia tu, ila anazungumza na mimi (Mkwasa), ama wasichana wawili tu wa hapa ndani ambao anashinda nao,"anasema Mkwasa ambaye sasa anamlea mtoto huyo.
Maneno hayo yanathibitishwa na mwandishi wa makala haya, aliyefika nyumbani kwa Mkwasa kwa nia ya kuzungumza naye baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa mtoto huyo.
Anapoitwa kwa nia ya kutambulishwa, anafika mlangoni na kubaki akiangalia tu huku wakati mwingine akiinamisha macho yake chini na hata anaposalimiwa haitikii, badala yake anaondoka na kwenda kujificha ndani.
Hali hii iliweka ugumu katika kufanya mahojiano naye, lakini kwa usiri mkubwa inatubidi kumtumia mmoja wa wasichana ambaye amekuwa muwazi kwake kusikia nini kilichotokea.
Si kwamba hazungumzi, la hasha binti huyu ni mzungumzaji mzuri na tunapotoka nje na kuwaacha wawili ndani ya sebule hiyo tunawasikia wakizungumza na hata kucheka kwa sauti.
Mkwasa anasema siku za mwanzoni binti huyo alikuwa haongei na mtu yoyote lakini baada ya kuhudumiwa na mwanasaikolojia ambaye hufika nyumbani kwake kila baada ya siku tatu, alianza kuongea.
Akisimulia tukio hilo, Mkwasa anasema mtoto huyo alikutwa akizubaa na akiwa amechoka katika kijiji cha Mindola baada ya kutoroka kwa mwanamume aliyeolewa naye.Anasema alipigiwa simu na viongozi wa kijiji hicho na kuagiza apelekwe katika kituo cha polisi.
"Nilikuwa kwenye kikao mjini, nikawaambia OCD (Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya), akae naye mtoto huyo hadi nitakaporejea, nilimwona mtoto. Hakuwa katika hali nzuri sana kwanza alikuwa mwoga, halafu hakuwa anaongea na mtu yeyote,"anasema.
Anasema polisi walimshauri kumpeleka mtoto huyo kwa daktari kwa ajili ya vipimo ambapo iligundulika kuwa ameshaingiliwa sana kimapenzi na kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
"Alipewa dawa na tukarudi nyumbani. Licha ya kulalamika kuwa anasikia maumivu, hata kaa yake pale nyumbani kwa siku za awali haikuwa nzuri,"anasema Mkwasa.
Anasema baada ya siku mbili mtoto huyo alionekana anajisaidia haja ndogo iliyochanganyika na damu, hali iliyomfanya kumrudisha tena hospitali alifanyiwa vipimo na kupewa dawa.
CHANZO MWANANCHI


No comments:

Post a Comment