Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, October 11, 2013

Uvumbuzi: Teknolojia rahisi inavyookoa maisha ya mama na mtoto




Muuguzi akimfunga mama kifaa cha kuzuia kutokwa damu kwa wingi kiitwacho anti-garment shock. 
Ni saa 9.00 alfajiri katika Kijiji cha Sintale, wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa. Maumivu ya uchungu wa kujifungua yamemuanza binti aitwaye Naomi John.
Amewahishwa katika zahanati ya kijiji ambayo hata hivyo haina dawa wala vifaa zaidi ya mkunga wa zamu wa siku hiyo.
 Kwa kuwa hakuna usafiri wa ku mwahisha Naomi katika hospitali ya wilaya, mkunga anajaribu kumsaidia katika kujifungua, lakini baada tu ya kujifungua, dada huyu anatokwa na damu kwa wingi, lakini pia, kichanga kilichozaliwa kinashindwa kupumua na kwa bahati mbaya wote… wanapoteza maisha.
Roho za kinamama na watoto wengi zinapotea kila kukicha kutokana na ukosefu wa huduma za afya, jambo ambalo limesababisha idadi ya   vifo vya makundi haya kuwa  milioni 6.9 kwa mwaka.
Vifo vya mama na mtoto vinaepukika na katika kupunguza vifo hivyo wataalamu wa afya wamebuni teknolojia nyepesi na nafuu itakayowezesha wataalamu wa afya katika eneo lolote Kusini mwa Jangwa la Sahara kuokoa maisha ya   viumbe hawa muhimu duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa, uvumbuzi wa teknolojia rahisi  utaweza kuokoa maisha ya wanawake na watoto zaidi ya milioni 7.5 kwa mwaka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki- Moon amesema, uvumbuzi huo ni sehemu muhimu kwa kila mwanamke na kila mtoto duniani kwani ni miongoni mwa harakati za kuokoa maisha ya wanawake na watoto milioni 16 ifikapo mwaka 2015.
Kupunguza vifo vya wanawake na watoto ni miongoni mwa malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa, kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa nchini kila siku, 26 hufariki kwa sababu zinazoweza kuzuilika. Wasaidie watoto kupumua (Helping Baby Breath) ni teknolojia inayotumiwa na wataalamu wa afya sehemu yeyote ile kuwasaidia watoto wanaozaliwa na kushindwa kupumua.(birth asphyxia) Teknolojia hii imesaidia kupunguza asilimia 47 ya vifo vya watoto wanaozaliwa na tatizo la kupumua nchini.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Profesa Cyriel Massawe anasema, iwapo teknolojia zaidi zingevumbuliwa, basi vifo vya wanawake na watoto vingekwisha kabisa.
“Tatizo kubwa ni kuwawezesha wataalamu wa afya. Hata kama teknolojia hizi zitavumbuliwa bado wataalamu wanahitaji usafiri ili kuzifikisha vijijini ambako kuna vifo zaidi, ” anasema Profesa Massawe.
 Profesa Massawe anasema ni teknolojia rahisi kutumika kwani inafundisha mbinu za kumkausha mtoto pindi anapozaliwa na kumvalisha kifaa maalumu kinachomsaidia kupumua.
Wakunga nchini walipewa mafunzo hayo na jinsi ya kutumia kifaa aina ya ‘Neonatalie’ ambacho ni kifaa rahisi kutumiwa na mtaalamu yeyote hata mkunga wa jadi ili kumsaidia mtoto mwenye matatizo ya kupumua pindi tu anapozaliwa. Teknolojia nyingine inayofanana na HBB ni ‘Bubble CPAP,’ kifaa cha njia ya upumuaji ambacho  huwasaidia watoto waliopata matatizo ya mfumo wa upumuaji ikiwemo nimonia.CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment