Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison
Mwakyembe, ametangaza rasmi kumalizika kwa fungate kwa watendaji wa serikali
mkoani Tanga ikiwamo Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Jeshi
la Polisi, kutokana na kuhusika moja kwa moja na mtandao wa magendo hasa
upitishaji wa dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa
bandari bubu 49 mkoani Tanga ambazo zimekuwa zikihusika na upitishaji wa bidhaa
kwa magendo ili kukwepa kodi, zikiwamo dawa za kulevya, wahamajia haramu na
pembe za ndovu.
Dk.
Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa TPA, TRA,
wafanyabiashara na wadau wanaotumia bandari ya Tanga muda mfupi tu baada ya
ziara ya ukaguzi katika wilaya ya Pangani na bandari ya Tanga.
Alisema ili kuthibitisha kauli yake
hiyo atawataja kwa majina wahusika na vinara wa mtandao huo nakwamba kuanzia
sasa anatangaza rasmi vita baina yao.
“Tunawajua kwa majina msione tumekaa
kimya tu na mitandao yenu tunaijua…jeshi la Polisi wanasaidia kuwasindikiza,
yaani Tanga imekuwa ni kituo cha kupokea bidhaa haramu…sasa honeymoon
(fungate), ndugu zangu imekwisha,” alisisitiza Waziri huyo.
Dk. Mwakyembe alieleza kutoridhishwa
kwake na utendaji kazi wa TRA mkoani hapa na kusema kuwa ataliwakilisha kwa
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa ili hatua za haraka zichukuliwe.
Awali, akizungumza katika mkutano
huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kipande Madeni, aliwataka watendaji wa
mamlaka hiyo mkoa wa Tanga kuendela kujituma katika utekelezaji wao ikiwamo
kufanya kazi kwa saa 24 kama wanavyofanya Dar es Salaam.
Naye
Kaimu Meneja wa TPA Mkoa wa Tanga, Freddy Liundi, alisema kuwa bandari hiyo
inatarajia kupokea vifaa aina ya Baji vyenye uwezo wa kupakua mzigo hadi wa
tani 3,500 kwa kontena 196 zenye urefu wa futi 20 mwezi Disemba, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment