Akizungumza na waandishi wa habaari Dar es Salaam, Mratibu wa Usimamizi wa Misitu ya Asili, Florian Mkeya alisema mwaka 1990 hadi 2005 hekta milioni nne za misitu zimepotea ambazo ni karibu asilimia 11 ya eneo lote la misitu nchini.
Mkeya alisema uharibifu mkubwa wa misitu unachangiwa na umasikini wa wananchi walio wengi ambao hutegemea rasilimali ya misitu katika kuendesha maisha yao.
"Ongezeko la watu wakiwamo wahamiaji haramu na ukosefu wa rasilimali mbadala kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi, pia vinachangia kwa kiwango kikubwa katika uharibifu wa misitu," alisema Mkeya.
Alieleza kuwa misitu ya Tanzania haina ubora kutokana na utumiaji holela wa misitu hivyo kusababisha ukosefu wa vyanzo vya maji.
Kutokana na na changamoto hizo TFS ina wajibu wa kuendelea kusimamia maeneo yote ya misitu chini ya mamlaka hiyo, alisema.
Alisema baadhi ya juhudi zilizofanywa ni kuendeleza kupanua maeneo ya hifadhi na kuhamasisha wananchi kuendelea kupanda miti.
"Ni wajibu wa wadau wote kwa uwezo walionao kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo ili kunusuru misitu hiyo isiangamizwe kwa kuwa athari zake ni kubwa," alisema Mkeya. Chanzo:mtanzania
No comments:
Post a Comment