skip to main |
skip to sidebar
HISTORIA YA NENO MARANGU "ENEO LENYE MAJI YENYE MAAJABU"
Kihistoria
jina Marangu linatokana na neno Morangu neno la kichaga cha zamani
kabla ya kuchakachuliwa na usasa,maana halisi ya neno hili ni nchi yenye
maji mengi.
Kwa wageni wanaofika eneo hili ambalo lipo kwenye
mitelemko ya mlima Mashariki kitu cha kwanza kukiona ni msitu mzito wa
migomba na miti,cha pili ni madaraja yasio na idadi yanapita juu ya
mito na chemichemi nyingi zilizopo eneo hili ambapo pia ni makao makuu
ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Moja ya maeneo yenye maajabu ni kijiji cha Ashira ambacho ni maarufu
kutokana na kuwa karibu na Shule ya Sekondari ya Ashira ambayo kwa miaka
mingi mamia na mamia ya wataalamu wamepitia hapa.Ndani ya kijiji hiki
kuna msitu mkubwa uitwao Yenunyi ambao ni chanzo kikubwa sana cha maji
kwani kuna chemichemi nyingi zinazoanzia hapa.Maji ya chemichemi hizi ni
meupe na matamu na husambazwa kwa mfumo wa mabomba na mifereji kwenda
kwenye taasisi na vijiji vyote vya karibu.
Katikati ya msitu
huu ndipo yalipokuwa makazi ya Mkuu wa ukoo wa Mtui aliyeitwa
Kimori.Huyu aliishi wakati ule koo mbalimbali zilikuwa zinapigana
ilikuweza kupata ukoo wenye nguvu kuunda utawala yaani Umangi.
Hivyo kwa wakati ule kulikuwepo na ushindani mkubwa kati ya ukoo wa Mtui
na ule wa Lyimo,kila wakati wa vita watu wa Mshiri walikuwa
wanawachukua maiti na majeruhi wao nyumbani na siku ya pili watu hawa
walioonekana tena sokoni na mtaani wakiwa wazima kabisaa.
Jambo
hili lilitishia usalama wa ukoo wa Lyimo kwani kila mara kutokana na
kutoogopa kifo askari wa Mshiri walipigana kwa ari kubwa na kuwashinda
wenzao huku wakichukua mifugo na mateka wengi.
Ili kupata siri
ya jambo lile,viongozi wa ukoo wa Lyimo walimtuma mwanamke ambaye
alijifanya kafukuzwa na mumewe na aliomba hifadhi kwa ukoo wa Mtui.Kwa
sababu alikuwa amekwisha fundishwa baada ya kuolewa na mmoja wa watu wa
Mtui kama alivyofanya Delila naye alimlaghai mumewe mpaka akatoa siri.
Siri alioitoa ni kuwa Mkuu wa mzee Kimori alifuga Konokono mkubwa
aliejulikana kama Kikoru,huyu alikua na uwezo mkubwa wa kuponya majeraha
ya askari walioumia na kuwafufua maiti waliofia vitani tu.Alifanya
hivyo kwa kulamba miili yao na kila aliepitiwa na konokono huyu alipona
jeraha au kufufuka.
Baada ya kupata siri ile askari wa Lyimo
walifanya mashambulizi matatu ya nguvu,shambulizi la tatu ndipo jeshi la
Lyimo liliwazidi nguvu askari wa wa Mtui mpaka waakamfikia Kikoru.
Walimchoma kwa mikuki mingi na kumuua,kabla ya kufa alilia kwa sauti
kubwa ya kutisha iliyosikika eneo lote la Marangu huku akitoa damu
nyingi sana.Baadae damu ile iligeuka kuwa maji ambayo mpaka leo
inaaminika yanatoka sehemu hiyo.
Baada ya hapo ukoo wa mtui
uliwekwa chini ya ukoo wa Lyimo na kuwa mtawala wa eneo lote la Marangu
chini ya Mangi aliejulikana kama Kilamia yani Mkandamizaji.
Kwa msaada wa Maliasili Zetu
No comments:
Post a Comment