Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema
kuwa anatafakari iwapo awanie urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,
kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea
nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba
ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: "Kwanza ni
kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana walioko
nje na ndani ya chama, wanataaluma, baadhi ya wazee na watu wengine iwe
kwa makundi au mtu mmoja mmoja wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa
muda sasa."
Aliongeza:
"Mwanzoni sikuona uzito sana, yaani sikuzingatia sana, lakini kwa
kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo
niseme ni jambo ambalo sasa ninalitafakari kwa kina".
Alisema ikiwa
ataamua kuwania urais, atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia
utaratibu utakaowekwa na chama hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati
wake. Makamba alikuwa akijibu hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi
wake kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka
urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Gazeti
hili lilidokezwa kuwa hatua yake hiyo imemwingiza katika mvutano usio
rasmi na wanasiasa ambao tayari wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo
ya juu ya uongozi nchini, wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa
akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali
iliaminika kuwa Makamba alikuwa katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa masuala ya kisisa wanasema 'katika
siku za karibuni mwenendo wake unaashiria kwamba si mmoja wa wanaomuunga
mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye mipango yake binafsi ya
kisiasa".
Habari
ambazo Mwananchi imezipata zinasema mwenendo wa Makamba umewakasirisha
baadhi ya wanasiasa hususan wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa
wamesikika hadharani wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata
hivyo, Makamba katika maelezo yake anasema hajawahi kuwa katika kundi
lolote la kumuunga mkono mtu yeyote kwani yeye haamini katika makundi.
"Ninaamini katika kundi moja, nalo ni CCM," alisema.
Aliongeza:
"Kwa hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa sababu zozote zile za kisiasa
nitamshangaa maana sijawahi mahali popote na kwa namna yoyote
kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi fulani, au kundi la mtu
yeyote."
Sababu za mashaka
Miongoni
mwa nyedo zinazotiliwa shaka za mwanasiasa huyo ni hatua yake ya
kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)
uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na mambo mengine aligawa simu zaidi
ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika
kwamba mpango huo ulikuwa ni wake binafsi na haukuwashirikisha
waliokuwa wakiamini kwamba wako naye katika harakati za kumuunga mkono
Lowassa.
Tukio
jingine ni lile la vijana waliojitambulisha kuwa viongozi wa vyuo vikuu
nchini kutangaza katika mkutano wao mjini Morogoro kwamba watamwomba
Makamba awanie urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, kutokana na kile
walichodai kwamba ni matokeo ya kura walizopiga baina ya kiongozi huyo
na viongozi wengine vijana; John Mnyika na Zitto Kabwe wa Chadema.
Wapinzani
wake wanaamini kwamba tamko la vijana hao zilikuwa mbinu binafsi za
Makamba kutaka kuonyesha kwamba naye anakubalika na pengine maandalizi
ya kujiengua rasmi kutoka katika kambi yake ya awali.
Wakati wa
maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, Makamba alikuwa Butiama mkoani Mara ambako mbali na kushiriki
Ibada ya kumwombea Baba wa Taifa, pia alikuwa mgeni rasmi katika
kongamano la kumuenzi kiongozi huyo.
Kuhusu
baadhi ya makada wenzake kukasirishwa na mwenendo wake kisiasa, Makamba
alisema: "Hata mimi nimesikia kama wewe unavyosema umesikia, inawezekana
wanakasirishwa na mvumo maana ndani ya chama chetu watu wanazungumza
sana, tena hadharani kwa hiyo katika mazingira hayo taarifa zinaweza
kumfikia yeyote kama zilivyokufikia wewe".
Alitetea
hatua yake ya kugawa simu kwenye mkutano wa UVCCM akisema alikuwa
akitimiza ahadi aliyoitoa wakati wa semina ya vijana hao Februari mwaka
huu mjini Dodoma, pale walipomuomba kuwasaidia ili waweze kutekeleza
matakwa ya ushauri wake wa kukitetea CCM katika mitandao ya kijamii.
"Mimi kwa
nafasi yangu nikiwa Naibu Waziri wa masuala ya teknolojia, nikiombwa
kusaidia lolote katika eneo langu ndani ya chama sioni tatizo ilimradi
niwe na uwezo nalo, kwa hiyo nilitimiza ahadi yangu tena kwa uwazi
sikufanya kwa kificho,"alisisitiza.
Makamba
ni mwanasiasa wa tatu kijana kutajwa kuwa huenda akawania urais, wengine
wakiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine
ambao wameishaonyesha nia ya kuutaka urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta na Lowassa.
Vita ya
urais imekuwa ikikiumiza CCM, ambapo Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania
Bara), Philip Mangula aliwahi kukaririwa akiwaonya makada wa chama hicho
ambao wameanza kupiga mbio za kuusaka uongozi huo kuwa hawatavumiliwa,
kwani harakati hizo zimekuwa kichocheo cha mgawanyiko ndani ya chama.
No comments:
Post a Comment