Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, November 25, 2013

Kigoma wapinga, Mbeya washangilia




Msanii wa kizazi kipya, Peter Msechu (aliyevaa miwani) akisikiliza kwa makini wakati aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam janaKigoma/Mbeya. Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mikoa ya Kigoma na Mbeya wametoa misimamo tofauti juu ya kuvuliwa uongozi kwa Zitto Kabwe.
Wakati wafuasi wa Tawi la Mwandiga, Kigoma wakifanya maandamano kupinga kitendo hicho, wenzao wa Mbeya wameunga mkono hatua hiyo.
Kigoma
Baadhi ya wanachama wa Mwandiga walichoma moto kadi, bendera na fulana za chama hicho kupinga uamuzi wa kuvuliwa uongozi kwa Zitto.
Wanadaiwa kufanya vurugu hizo baada ya maandamano ya umbali wa kilomita tisa kutoka Mwandiga hadi Kigoma. Pia wanadaiwa kubomoa ukuta unaotumika kubandika matangazo.
Wakizungumza katika eneo la Kituo cha Mabasi Mwandiga, wanachama hao walisema Chadema kimekuwa na desturi ya kufukuza viongozi wanaopigania haki na kupambana na ufisadi nchini hatua ambayo walisema ni sawa na kudhoofisha jitihada za kupambana na uovu nchini.
Akisoma tamko lao, mmoja wa wanachama wa tawi hilo, Rucha Bakari alisema wanachama wa Kigoma wamepokea kwa masikitiko uamuzi wa chama kumvua madaraka Zitto na kusema jambo hilo linaua harakati za Chadema kuingia Ikulu mwaka 2015.
“Chama kimemdhalilisha kiongozi wetu Zitto Kabwe. Viongozi wa Chadema wamezidi kuonyesha ubabe na umangimeza dhidi ya viongozi wanaopigania haki za kidemokrasia ndani ya chama na rasilimali za chama,” inasema sehemu mojawapo ya tamko hilo na kuongeza:
“Walianza kwa kumfukuza Dk Aman Kabourou, David Kafulila, Shaibu Akwilombe, Habibu Mchange, Juliana Shonza na Mtella Mwampamba na sasa wamehamishia ukatili huo kwa mwanademokrasia, Jemedari wa vita dhidi ya ufisadi, Zitto. Ili chama kiwe na amani tunataka ufanyike mwafaka wa kitaifa ndani ya chama, vinginevyo tutachukua uamuzi mgumu.”
Mmoja wa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Jimbo la Kigoma Kaskazini, Stumai Omari alisema anapinga uamuzi wa chama dhidi ya adhabu aliyopewa Zitto. Hata hivyo, alisema bado ataendelea kuwa mwanachama wa Chadema.
Tawi la Mwandiga ndiko alipozaliwa Zitto na kisiasa ndipo ilipo ngome kuu ya Chadema katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.

No comments:

Post a Comment