Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, November 7, 2013

KUTOKA TABORA: WAFUGAJI WASEMA SERIKALI INAWAFANYA WAISHI KAMA WAKIMBIZI.

Mmoja wa jamii ya wafugaji akionesha jeraha mgongoni alilopata kutokana na kipigo cha askari wa maliasili wilayani Kaliua Tabora

**************
 
Na Hastin Liumba,Kaliua-Tabora yetu blog
TUMEFIKIA mahali  tunaishi katika ardhi ya nchi yetu kama wakimbizi,huku tukinyanyasika sana kwa kigezo cha sisi kuwa wafugaji mifugo, tunaelezwa mifugo yetu inaharibu vyanzo vya maji, mazingira na hifadhi za taifa.
Hayo ni maneno yaliyotamkwa na mfugaji Gunze Pamagi wakati akiongeza na mwandishi wa makala hii katika kijiji cha Lumbe wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
Pamagi anasema hatua hiyo imekuja na kuitamka kauli hiyo kwa uchungu hasa baada ya miaka mingi jamii ya wafugaji kunyanyasika ndani ya ardhi ya nchi yao kama vile hawana kwao ni kama wakimbizi.
Mfugaji huyo anasema wamejitahidi kufuata taratibu za hifadgi lakini kila wanaoonyeshwa maeneo ya kuchungia kunyweshea tena kwa vibali na mihutasari ya vikao na serikali ya vijiji bado wamekuwa wakikamatwa na mifugo yao na mara nyingine wamekuwa wakipigwa risasi ama mfugaji kufa kwa ugonjwa wa moyo baada ya kufikilisiwa.
“Pamoja na jamii ya wafugaji kuwa na mchango kwa taifa hili hasa mazao ya mifugo kama maziwa,nyama,uchangiaji shughuli za maendeleo na zao la ngozi bado tumekuwa wahamishwa kutwa kucha licha kulipa faini kwa kigezo cha kuchungia kwenye maeneo ya hifadhi.”aliongeza.
Anasema kinachowasikitisha sana ni jinsi wanavyoonyeshwa mipaka ya kuchungia na serikali za vijiji lakini ghafla baada ya siku chache wanakamatwa kwa mitutu ya bunduki na askari wa maliasili na kujulishwa wameingia kwenye hiafadhi.
Mapema jumapili ya mwezi oktoba 12 mwaka huu, ng`ombe 5,000 zilikamatwa na askari wa hifadhi na tukajulishwa kuwa wameingia kwenye vyanzo vya maji na hadi sasa tumeshindwa kuwakomboa kutokana na faini kuwa kubwa.
Pamagi anasema ndani yake wapo wafugaji kadhaa ambao ni Gunze Pamagi Mjanandege Doto ,Mulani Mabatula ,Lesio Nhumai.
Wengine ni Sitesheni Swila ,Mashilili Shija ,Lukalalila Jitungo ,Anthony Bahebhe ,Masanja Tama na Fungameza Lugulu.
Baada ya kukamatwa kwa ng`ombe wao.
Pamagi anasema baada ya kukamatwa kwa ng`ombe hao na kuelezwa kuwa wameingiza mifugo yao kwenye hifadhi ya vyanzo vya maji katika hifadhi ya Pori la akiba la Ugala,wametakiwa kulipa faini kila ng`ombe sh 180,000 faini ambayo haikuwahi kulipwa toka wameanza kufuga.
Anasema wanashangazwa na faini hiyo kwani wanachojua wao faini ya siku zote ni sh 10,000 japokuwa wamewaeleza watu wa hifadhi kuwa wapo tayari kulipa kila ng`ombe sh 30,000 lakini imeshindikana.
Anasema hatua hiyo iliwafanya kutafuta mwanasheria Moses Mahenge toka kampuni ya uwakili ya Tutashinda Legal and Centre ya Kisarawe kwani ukipiga hesabu ya faini ya sh 180,000 kwa kila ng`ombe maana yake zinatakiwa sh milioni 900 fedha ambazo hatuna.
Hali ilivyo kijiji cha Lumbe walikohifadhiwa ng`ombe hao.
Pamagi anasema hadi sasa kuna ng`ombe takribani ni zaidi ya 50 wakiwemo ng`ombe wakubwa na ndama wanaozaliwa eneo la tukio kutokana na kukosa malisho na maji.
Wamejitahidi sama kujadiliana na watu wa maliasili juu ya malisho kiasi cha kukubaliana wachungwe lakini wenzetu wamekuwa wakikaidi na kuwabadilikia kila mara tena kwa vitisho vikali.
Aidha anaongeza kuwa hadi sasa zipo taarifa kuwa kuna kundi la ng`ombe walionekana wakiswagwa huku nyama zikizagaa mitaani zikiuzwa bila kuelewa ni mifugo yao ama la na ndiyo maana wanaona kama wapo kwenye nchi isiyo ya kwao walipoazaliwa.
Kwa upande wake mfugaji mjanandege Doto anasema yeye binafsi ana ng`ombe 200 waliokamatwa akidaiwa waliingia kwenye chanzo cha maji.
Doto anasema anashangazwa na hatua ya mifugo yake kukamtwa kwani kuna muhutasari wa mwaka mwezi septemba 2,2009 ulihusisha serikali ya kijiji cha,wafugaji,diwani na katibu tarafa ukiruhusua wafugaji hao kuishi eneo hilo.
Anasema muhutasai huo unaonyesha makubaliano hayo kutokana na magizo ya mkuu wa wilaya kuhusiana na hifadhi na uchangiaji miradi ya maendeleo kama ujenzi wa sekondari nyumba za walimu na zahanati.
Aidha muhutasari huo unaonyesha serikali ya kijiji cha Lumbe kata ya Ukumbisiganga ilivyowapokea wafugaji watatu ambao ni Richard Nyanda Maduka mwenye ng`ombe 300,Amlani Matatula ng`ombe 300 na Redio Numai ng`ombe 400.
Anafafanua kuwa wafugaji wengine waliotuma maombi ya kuhamia kijiji cha Lumbe na kukubaliwa ni Stesheni Swila ng`ombe 150,Nganza Ngassa ng`ombe 300,Mashiri Shija ng`ombe 200,Kitungulu Lutamla ng`ombe 200 na Mjanandege Doto ng`mbe 200.
Akionyesha muhutasari unaonyesha aliyekuwa afisa maliasili marehemu Fedrick Yerenimo Nkolle kuwa kijiji kinatakiwa kiwe na ng`ombe 3000 tu na walielezwa moja ya masharti mwaka 2008 walichangia fedha za ujenzi wa majengo mawili ya shule ya msingi Lumbe na walianya hivyo.
Anasema makubaliano haya yapo kwenye muhutasari na zaidi wameweka sahihi na dole gumba kukukaliana na maelezo na masharti ya serikali ya kijiji sasa wanashangazwa na hali hii inayojitokeza na kuona kuwa wananyanyasika kwenye ardhi ya nchi yao.
Anasema hadi kufikia leo mwezi oktoba 22 2013 bado watu wa maliasili wameng`ang`ani kiasi cha faini sh 180,000 wakati mkuu wa mkoa waliomba kiasi hichi kiangaliwe upya ili kuondoa tofauti na mgogoro uliopo.
“Tumeamua kuiachia serikali ya mkoa itusaidia kwani hapa tunaona kabisa tunakufa kisaikolojia hatuna jinsi zaidi ya kujiona tunaiongia kweny umasikini.”alisema.
Mkuu wa mkoa wa Tabora azuru eneo hilo kutafuta suluhu.
Akijibu malalamiko hayo mkuu wa mkoa wa Tabora Fatma Mwassa alisema licha ya yeye mwenyewe kuja kujionea hali hiyo lakini suala hilo ni operesheni ya kitaifa siyo ya kimkoa.
Mwassa alisema anachotaka kufanya ni kuwaombea kwa waziri mwenye dhamana ili waweze kulipa faini stahiki lakini kwa sasa yeye hana maamuzi yoyote.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa aliwashauri wafugaji hao kuwa licha ya adha wanayopata siyo kwamba serikali haiwajali bali wanachotakiwa ni kupunguza mifugo yao ili wasipate changamoto inayowakabili.
“Punguzeni mifugo yenu ni mingi ndiyo maana mnakosa malisho na maji.....siyo lazima uwe na mifugo yote hii mkipunguza mnaweza mkaanzisha biashara nyingine mtakuwa mmeepukika na dha mnayopata.” Aliwaasa.
Naye meneja wa Pori la akiba la Ugala aliyejitambulisha kwa jina moja la Lyimo alimueleza mkuu wa mkoa  kuwa wafugaji hao bado wana nafasi ya kwenda ofisi zao kujadiliana namna ya kumaliza suala hilo.
Hadi kufikia jana jumatatu meneja wa Pori la akiba la Ugala Lyimo aliliambia gazeti hili kuwa faini ya kiasi cha sh 180,000 kiko pale pale hakiepukiki wafugaji wanapaswa kulipia kwani wana kosa.

Na Tabora yetu Blog

No comments:

Post a Comment