Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana ameangukia pua baada
ya Bunge kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele
vya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi
wa habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Kadhalika
Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana na wabunge wengine kukataa
mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika kwa Serikali kupeleka
bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari, badala ya kutoa ahadi
zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa
kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi
wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani
ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi
kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
"Sitegemei
magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya taifa. Walio wangu watanikataa na
wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa ajili ya taifa sitamwangukia mtu
yeyote miguuni," alisema Werema, kauli ambayo iliwachefua wabunge.
Hata
hivyo, jana baada ya Spika kuwahoji wabunge na kukataa mapendekezo ya
Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka hivyo alisimama na kutaka
Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu hicho.
"Mheshimiwa
Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi
naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,"
alisema Werema.
Hata
hivyo, Spika alikataa na kusema: "Kama kuna eneo ambalo tumefanyia utani
Serikali ni katika eneo hili, naomba Serikali mtuletee muswada bungeni
siyo porojo za maneno."
Katika
marekebisho hayo, Serikali ilikuwa ikipendekeza katika sheria hiyo
mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na
hatia ya kuandika habari za uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi
kiasi kisichozidi Sh5 milioni.
Hata
hivyo, wakati Bunge lilipoketi kama kamati wabunge walikataa kupitisha
marekebisho hayo ambayo yalikuwa sehemu ya Muswada wa Marekebisho ya
Sheria mbalimbali wa mwaka 2013, wakisisitiza kwamba Serikali ipeleke
bungeni muswada wa sheria ya habari.
Moto wa wabunge
Moto wa
wabunge hao uliwashwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM),
ambaye alipendekeza sehemu ya nane ya muswada iliyokuwa na vipengele vya
39, 40 na 41 iondolewe ili kuishinikiza Serikali kupeleka bungeni
sheria nzima inayohusu vyombo vya habari.
Mbunge
huyo alisema kuwa sehemu hiyo na vipengele vyake kama vingepitishwa
vingeifanya Serikali kuwa kimya na kushindwa kupeleka bungeni Muswada wa
Sheria ya Vyombo vya Habari kama ilivyoahidi kwa muda mrefu.
"Mimi
nimekuwa mbunge hapa huu mwaka wa nane, lakini kila siku Serikali
imekuwa na kigugumizi cha kuleta muswada huo. Kila mara tunaambiwa kuwa
utaletwa, lakini hauletwi sasa mpango wa kuleta vitu nusu-nusu haufai,"
alisema Selukamba.
Mbunge
huyo alilalamika kuwa baadhi ya viongozi walishapendekeza kuwa watu wote
wanaopigia kelele sheria hiyo waangaliwe hati zao za kusafiria kwa
madai kuwa zinatia shaka jambo alilosema kuwa yuko tayari kufanya hivyo
ilimradi ahakikishe anasimamia kweli.
Jenista Mhagama
Baada ya
Serukamba kutoa hoja hiyo, wabunge wengi walisimama kumuunga mkono ndipo
akapewa nafasi ya kuchangia Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama ambaye
pia alisisitiza kwamba lazima sheria ya vyombo vya habari ifikishwe
bungeni.
Mhagama
alisema kutokana na kigugumizi cha Serikali, tayari kuna gharama ambazo
zimekuwa zikijitokeza ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za
Jamii kutumwa India kwa ajili kujifunza mambo mbalimbali yanayoendana na
sheria hiyo, lakini bado hata hivyo haijasaidia kitu.
Mhagama
na Serukamba tangu wakati mjadala wa sheria ulipoanza juzi walisisitiza
kuunga mkono kuletwa kwa sheria ya vyombo vya habari. Serukamba alisema
akichangia muswada huo alihoji: "Kuna nini hapa? Maana hii tabia ya
kuchomoa vipande vipande na kutuletea hapa haina tija."
"Tukatae
vipengele hivi, nawaomba wabunge wenzangu mniunge mkono katika hili na
ikiwa tutavikataa vipengele hivi Serikali italeta sheria nzima hapa,
mimi sina tatizo na adhabu hata ingekuwa mara tatu, lakini tuleteeni
sheria nzima, mnaogopa nini?" alihoji Serukamba.
Mhagama
yeye alisema kwa muda mrefu wadau wa vyombo vya habari wamelalamikia
kuwapo kwa sheria hiyo itakayolinda tasnia ya habari, lakini Serikali
mara zote imekuwa ikipiga danadana.
"Kwa nini
Serikali inachelewa kuwasilisha muswada wa sheria bungeni? Hebu sasa
tukae na wadau tukubaliane mambo ya msingi, tuwe na sheria ili kuinusuru
tasnia ya habari, sheria itasaidia kuwadhibiti makanjanja, wapo watu
wanaoidhalilisha tasnia ya habari bila sababu za msingi," alisema.
Taarifa
ya Serikali iliyotolewa bungeni jana ilisema Muswada wa Vyombo vya
Habari uko tayari na kwamba wakati wowote unaweza kupelekwa bungeni kwa
ajili ya kupitishwa kuwa sheria.
Wabunge wengine
Vipengele
hivyo vilipingwa na wabunge wengi tangu mwanzo, akianza Waziri Kivuli
wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
(Chadema) pamoja na Wabunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya na Martha
Mlata (CCM).
Tundu Lissu
Katika
maoni ya Kambi ya Upinzani, Lissu alisema mapendekezo ya marekebisho ya
Sheria ya Magazeti hayana msingi kwa sababu; hakuna ushahidi wowote
kwamba adhabu zilizoko katika vifungu vya 36(1) na 37(1)(b)
zinazopendekezwa kuongezwa zimeshindwa kudhibiti makosa ya uchochezi.
"Tangu
sheria hiyo ilipotungwa miaka zaidi ya 37 iliyopita, hakuna mwandishi wa
habari au mchapishaji wa gazeti lolote ambaye amewahi kufikishwa
mahakamani na kupatikana na hatia ya makosa hayo. Badala ya kuwapeleka
wakosaji mahakamani, Serikali imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na
kutisha waandishi habari," alisema Lissu na kuongeza:
"Hii peke
yake inathibitisha hoja kwamba sheria ilitungwa kwa malengo ya kisiasa
ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa Serikali na watawala na si kuzuia
makosa ya jinai".
Bulaya
Bulaya
kwa upande wake alisema, Serikali inafanya makosa makubwa kwa kutaka
kuwaadhibu waandishi wa habari, pasipo kujenga msingi imara wa uandishi
wenyewe kama taaluma katika nchi.
"Kwa nini
Serikali inawaza adhabu kali tu? Kuongeza faini kutoka Sh15,000 hadi
Sh5 milioni, hapo kuna nini, lazima tujiulize maana kwa kufanya hivi
tunawaumiza waandishi wa habari ambao wengi wao hawana uwezo wa kulipa
hizo fedha,"alisema Bulaya na kuongeza:
"Sheria
nzima ikiletwa hapa, tutakuwa na uwezo wa kuangalia mambo mengi yakiwamo
masilahi ya waandishi wa habari, lakini pia kuwabana watu ambao
hawataki kutoa habari ila wanasubiri waandikwe ndipo wajitokeze
kulalamika."
Mlata
Naye
Martha Mlata katika mchango wake alisema wanasiasa ndio wamekuwa
wakiwatumia waandishi wa habari na kwamba faini iliyowekwa na Serikali
ni mbaya kwani ni mzigo kwa waandishi wa habari.
"Na sisi
wanasiasa tuache kuwatumia waandishi wa habari na ninyi waandishi wa
habari msikubali kutumiwa na wanasiasa, tukitaka kuwatumia mkatae na
mfanye kazi kwa kumwogopa Mungu kila mtu kwa dini yake," alisema Mlata.
Walioishabikia sheria
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi
Chana na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) walishabikia
kuwapo kwa adhabu kali kwa waandishi wa habari, kwa maelezo kwamba
wamekuwa wakitumiwa kuwachafua watu.
Chana
alisema: "Katika malengo ya Serikali ilipoleta marekebisho haya
wametuambia kwamba malengo yake ni kuongeza adhabu ili kulinda matumizi
ya lugha ya matusi, makosa haya yanajumuisha matumizi ya lugha za
uchochezi zinazoweza kusababisha machafuko katika jamii.
"Ni
ukweli kila Mtanzania anafahamu kuwa magazeti yetu kuna wakati
yanatumika na kikundi fulani, kuwabeba kikundi fulani au mtu fulani na
kuangamiza mtu fulani au kikundi fulani.
Aliliomba
Bunge litoe majibu pale magazeti yanapomdhalilisha mtu kwa kuandika
jambo ambalo halina ushahidi wa kimahakama. "Nawauliza wahariri, pale
magazeti yanapotumika kuchochea ndivyo sivyo tufanyaje? Je, huo ndio
uhuru wa habari?" alihoji.
Nchemba
kwa upande wake alisema hakuna haja ya kusubiri sheria mpya na kwamba
kusubiri kunaweza kutoa mwanya kwa vyombo vya habari kuitumbukiza nchi
kwenye machafuko.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment