SIMBA imepanga kuongeza kiungo mkabaji, beki wa kati na mshambuliaji kwenye dirisha dogo la usajili ingawa pia imedai itaangalia kwa jicho la tatu nafasi ya kipa inayoonekana kusuasua.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema nafasi hizo ndizo zimeonekana zina mianya.
Julio, ambaye kikosi chake kina wachezaji 26 alisema wanahitaji kujipanga upya na watawasilisha mapendekezo yao kwa uongozi.
“Tumesuasua katika baadhi ya mechi na nafasi
ambazo tunaweza kuongeza dirisha dogo ni mshambuliaji mmoja, beki wa
kati na kiungo mkabaji ingawa pia tutaangalia nafasi ya kipa, nayo
tunaweza kuongeza nguvu kwani pia inasuasua,” alisema Julio, ambaye
habari za ndani zinadai huenda naye akatolewa kwenye benchi la ufundi la
timu hiyo.
Simba ilifanya vizuri katika mechi kadhaa za
mzunguko wa kwanza ingawa ilikuja kupepesuka na kutoka kileleni ikagota
nafasi ya nne.
Hata hivyo Julio alitetea uamuzi wao wa kuwapeleka
wachezaji walioshuka viwango kwenda timu ya vijana baada ya baadhi ya
mashabiki na wanachama kuponda mfumo huo.
“Hatuwezi kuacha jambo hilo, litaendelea hivyo hivyo hata kama hawataki, kwani ndiyo funzo la wachezaji wasiotaka kujituma.
Mchezaji ukishindwa kuonyesha kiwango unaenda timu
B ili upandishe kiwango chako na ukipelekwa kule wale waliobaki timu
kubwa lazima nao watajituma zaidi,”alisema Julio, ambaye ni mchezaji wa
zamani wa Simba.CHANZO MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment