MTOTO AZRA VUYO JACK SASA ANAMIAKA 2 NA BADO ANAENDELEA KUKULIA MAHABUSU |
MTOTO AZRA VUYO JACK 2 AKIWA NA MWANDISHI WETU JOSEPH MWAISANGO NJE YA MAHAKAMA WAKATI KESI YA WAZAZI WAKE IKIENDELEA KUSIKILIZWA |
BABA NA MAMA AZRA WAKIWA NA MTOTO WAO WAKISUBIRI KUINGIA MAHAKAMANI HII PICHA NI YA MIAKA MIWILI ILIYOPITA |
MTOTO AZRA VUYO JACK AKIWA AMELALA HAPA ALIKUWA NA MIEZI 5 |
TAASISI zinazohusika na haki za binadamu,
ukatili wa kijinsia pamoja na Haki za watoto zimeombwa kuingilia kati suala la
watoto wanaopata mateso magerezani kutokana na wazazi wao kutumikia adhabu.
Mwito huo umetolewa na baadhi ya wananchi
kufuatia kuwepo kwa watoto waliozaliwa Gerezani lakini hakuna hatua
zilizochukuliwa za kuwatoa nje ya gereza watoto hao na badala yake wanaendelea
kukulia humo.
Baadhi ya watoto waliozaliwa gerezani na
kuendelea kuishi humo ni pamoja na Azra Vuyo Jack(2) ambaye ni mtoto wa
Anastazia Cloete (29) raia wa Afrika kusini aliyekamatwa miaka miwili iliyopita
akituhumiwa kukutwa na madawa ya kulevya.
Tangu kujifungua kwa mwanamke huyo hakuna
juhudi zozote zilizofanywa na mamlaka zinazohusika za kumnusuru mtoto Azra(2)
kutokana na adhabu anayoitumikia mzazi wake na kumkumba yeye ambapo baadhi ya
wasamaria wema wameendelea kujitolea kupeleka chakula.
Emily Mwaituka mmoja wa wasamaria wema
anayejitolea kumlea mtoto huyo kwa kupeleka maziwa na chakula amesema
anachoshangaa ni mateso anayoyapata mtoto huyo kwa kuishi gerezani wakati
taasisi na vituo vya kulelea watoto vipo.
Amesema kinachomshangaza ni hata Ubalozi
wa Afrika kusini hapa nchini kukaa kimya na kushindwa kushughulikia suala la
kumtoa mtoto gerezani hadi anafikisha miaka miwili huku bado kukiwa hakuna
dalili za kumtoa.
Ameongeza kuwa ni vema angeruhusiwa
kumlea nyumbani kwake badala ya kumwacha kuendelea kuishi gerezani ambako
kutamwathiri mtoto huyo kisaikolojia kutokana na maisha yagerezani.
Amesema mtoto huyo angewasubiri wazazi
wake nje ya gereza wakati kesi yao inayoendelea kusikilizwa katika Mahakama kuu
kanda ya Mbeya kwa kulelewa na wasamaria wema kama Serikali imeshindwa
kumsaidia.
Mbali na mtoto huyo mwingine ni mtoto wa
Wilvina Mkandara ambaye alijifungua mtoto akiwa gerezani baada ya kuhukumiwa
kwenda jela miaka 30 kutokana na kukutwa na hatia ambapo mtoto wake hadi sasa
anaumri wa miezi sita.
Hata hivyo ni watoto wengi wanaozaliwa
Gerezani pindi wazazi wao wakiwa wanatumikia adhabu kwa mujibu wa Sheria, Swali
je Sheria zinasemaje kuhusu mtoto ambaye hana hatia kuendelea kuishi gerezani
hata kama anapata huduma zote za msingi?
Haki za Watoto, Unicef, na Taasisi za Dini mpo wapi
kufuatilia na kujua ni watoto wangapi wanaathirika kisaikolojia kwa kutumikia
adhabu za wazazi wao magerezani na kuchukua hatua stahiki za kuwanusuru na hali
hiyo?
Aidha baadhi ya wadau wamekiomba Chama
cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania(TAMWA) ambao wamekuwa mstari wa mbele
kutoa elimu kwa jamii kuepuka ukatili wa kijinsia na watoto kuingilia kati
suala hilo.
Wamesema ni bora taasisi hiyo
ikalishughulikia suala hilo mapema kabla ya watoto hawajaathirika na uwepo wao
ndani ya magereza kutokana na kukosa baadhi ya huduma kama michezo na watoto
wenzie na haki ya kusoma.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment