Zimebaki siku chache kabla ya kuuaga mwaka 2013, mwaka ambao umekuwa na matukio mengi yaliyoitikisa nchi ya Tanzania, huku mengine yakiipa sifa kubwa.
Historia ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya
itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi ilianza Desemba 31, 2011
wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa, alikiri wazi kuwa sasa
inahitajika Katiba Mpya ili kuendana na wakati wa sasa.
Baadaye Rais Kikwete aliwateua wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na ilianza kazi
yake ya miezi 18, kuanzia Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo iliitoa Juni 4, mwaka huu.
Baada ya kutolewa kwa rasimu hiyo wananchi
walipewa muda wa kuipitia na kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya
wilaya, yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Maoni hayo yalikusanywa na tume hiyo kwa ajili ya
kuyachambua na kutoa rasimu ya pili ya Katiba ambayo inatarajiwa
kutolewa Desemba 30, mwaka huu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kumaliza
kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15, mwaka huu, lakini Rais
Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi na hivyo kuifanya iweze kuendelea na
kazi hadi Desemba 30.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume
hiyo ilikuwa ya pili, kwani mara ya kwanza tume hiyo iliomba kuongezewa
muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu
Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, tume ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku
nyingine 14, Rais Kikwete ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya
60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Kifo cha Dk Sengondo Mvungi
Hatua ya Rais kuiongezea muda Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wa tume hiyo
kujipanga upya baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk
Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika
Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu
wanaotuhumiwa kuwa majambazi, nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.
Ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama
Ni siku mbili za kihistoria ambazo zimeweka rekodi
ya aina yake katika historia ya nchi hii, kuanzia maandalizi ya ujio
wake mpaka alivyowasili nchini Julai 1 na kuondoa Julai 3, mwaka huu.
Shughuli nyingi na barabara kadhaa zilifungwa ili
kutoa nafasi kwa ugeni huo mkubwa uliojumuisha familia yake, wafanyakazi
wa ikulu, walinzi na makachero wa usalama kutoka nchini Marekani.
Katika ziara yake hiyo, Rais aliwekea mkazo
umuhimu ambao Marekani inauweka katika ushirikiano wetu wa kina na
unaoendelea kuimarika na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia
mipango mbalimbali ikiwemo ile ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji
na biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika
kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika.
Ziara ya Rais wa China, Xi Jinping
Ziara hii ilitokea ikiwa ni wiki mbili tangu
achaguliwe Xi Jinping kuwa Rais wa China, ambapo aliichagua Tanzania
kuwa nchi ya kwanza kuitembelea barani Afrika.
Katika ziara hiyo Rais Jinping alikutana na
viongozi mbalimbali nchini, kusaini mikataba ya kidiplomasia 19, ukiwemo
wa ujenzi wa Bandari wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akiwa nchini Rais Jinping alitoa hotuba yake ya
kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo, ambayo iligusia masuala ya
kiuchumi, kisiasa sambamba na kueleza msimamo wa nchi yake kwa Tanzania
na Afrika.
Rais huyo alikutana pia na jumuiya ya watu wa
China na kutembelea makaburi ya wataalamu wa Kichina ambayo yapo Majohe,
Ukonga ambako alitoa heshima zake kwa Wachina waliofariki dunia wakati
wakijenga reli ya Tazara.
Bomu la Arusha
Mei 5, mwaka 2013 ni siku ambayo haitafutika
katika historia ya Tanzania kutokana na tukio la kusikitisha la kutupwa
kwa bomu kanisani, ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine zaidi
ya 60 kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea mbele ya Balozi wa Vatican na
Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo,
Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha, walipokuwa
wakizindua jengo la Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.
Mgogoro wa gesi Mtwara
Maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana
wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, kutoka
mkoani hapo kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyoratibiwa na vyama vya
Chadema,CUF, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT-
Maendeleo, ADC, UDP na DP yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo,
zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya
hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi
asilia inapatikana.
Kufuatia fujo na vurugu zilizotokea katika
maandamano hayo risasi na mabomu yalirindima, hali iliyozua hofu na
tafrani mkoani hapo.
Sakata la Sheikh Ponda
Tukio la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya ya
Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda ilikuwa miongoni mwa habari
zilizoibua mjadala mzito huku kukiwepo na hali ya sintofahamu kama
kiongozi alijeruhiwa kwa risasi au kitu chenye ncha kali.
Mkasa huo wa aina yake ulitokea Agosti 10, mwaka
huu majira ya saa 12: 15 za jioni eneo la Barabara ya Tumbaku karibu na
Fire, mkoani Morogoro mara baada ya kumalizika kwa Kongamano la Kiislamu
lililofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata
ya Saba Saba.
Baada ya tukio hilo, uvumi ulisambaa maeneo
mbalimbali nchini ukidai kuwa Shekhe Ponda amepigwa risasi na polisi na
kufariki dunia.
Kuporomoka kwa ghorofa
Ilikuwa ni asubuhi ya Machi 29 ambapo jengo la
ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika Mtaa wa Indira Gandhi jijini
Dar es Salaam, liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 36 na wengine
kadhaa kufunikwa na kifusi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo kulizua huzuni,
taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio
kutaka kufahamu nini kimetokea hali iliyosababisha kusimama kwa shughuli
mbalimbali katikati ya jiji.
Matukio ya tindikali
Mwaka 2013 kumekuwa na matukio mengi wa watu kumwagiwa tindikali hususan upande wa Zanzibar, ambapo matukio kadhaa yaliripotiwa.
Mwaka 2013 kumekuwa na matukio mengi wa watu kumwagiwa tindikali hususan upande wa Zanzibar, ambapo matukio kadhaa yaliripotiwa.
Julai 19 mwaka huu Said Mohamed Saad ambaye ni
Mkurugenzi wa Home Shopping Center alimwagiwa tindikali na mtu
asiyefahamika kisha kutokomea na kumuacha bilionea huyo katika maumivu
makali.
Saad alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya
matibabu lakini ilishindikana kutokana na madhara makubwa aliyoyapata
kutokana na tindikali hiyo hali iliyosababishwa kupelekwa Ujerumani kwa
matibabu zaidi.
Matukio mengine yalitokea Zanzibar kuhusisha raia
wawili wa Uingereza, Kate Gee na Kirstie Trup waliomwagiwa tindikali,
eneo la Mji Mkongwe na Padri wa Parokia ya Machui, Anselmo Mwang’amba .
Siku chache baada ya tukio hilo lilitia doa nchi
ya Tanzania katika ramani ya kimataifa, jeshi la Polisi upande wa
Zanzibar lilitangaza kukamata lita 29 za tindikali.
Mauaji ya kutumia silaha
Mwaka huu pia kulikithiri kwa mauaji ya kinyama
kwa kutumia silaha ambapo watu kadhaa walijikuta wakipoteza maisha na
wengine kujeruhiwa, kutokana na vitendo hivyo vilivyoonekana kushika
kasi nchini.
Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya Padri wa
Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili, Evarist Mushi ambaye alipigwa
risasi na watu wasiofahamika asubuhi ya Februari 17 mwaka huu.
Mauaji mengine yalitokea Agosti 7 kwa
mfanyabiashara maarufu wa madini Erasto Msuya kuuawa kwa kupigwa risasi
wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Msuya alikuwa anamiliki vitegauchumi
kadhaa na kuaminika kama mfanyabiashara aliyekuwa akiongoza kwa utajiri
Mirerani aliuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20.
Tukio lingine la mauaji lillilotokea Oktoba 13
eneo la Kibamba ambalo kwa kiasi kikubwa lilihusishwa na ugomvi wa
kimapenzi ambapo Mtangazaji wa Kituo cha ITV, Ufoo Saro alijeruhiwa kwa
risasi huku mama yake mzazi akipoteza maisha kutokana na shambulio
lililofanywa na mzazi mwenzie aliyejulikana kama Anthery Mushi.
Operesheni Tokomeza
Operesheni hii iliyolenga kupambana na vitendo
vya ujangili dhidi ya wanyamapori ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu
katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na mbuga za wanyama huku
ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa
Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) na Idara ya Wanyamapori. Mawaziri wanne waliopoteza
nafasi zao kufuatia operesheni hiyo, nao ni Balozi Khamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii), Dk David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Dk Emmanuel
Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).
No comments:
Post a Comment