Dodoma.Spika
wa Bunge, Anne Makinda jana alipigilia msumari sakata la wabunge
kuchukua posho bila kuzifanyia kazi stahiki kwa kuwaamuru wazirudishe.
Spika alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati akitoa mwongozo ulioombwa na
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde akitaka ufafanuzi wa
hatua ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Erasto Zambi kutumia Bunge
kujitetea kuhusu tuhuma za kuchukua posho za safari bila kusafiri.
Alisema Zambi ni mbunge ,pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya na
Kamishna wa Bunge anayefahamu taratibu za safari zinazoeleza kuwa
kuchukua fedha bila kwenda safari ni makosa.
Silinde wakati akiomba mwongozo huo alimtuhumu Zambi kuwa alichukua
kiasi cha Sh13 milioni za posho ya safari ya Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) na nyingine kwa ajili ya safari ya shughuli za michezo
lakini hakusafiri.
“Mtu anapozungumza kwa kutumia Bunge lako kujitetea kwa kukiuka
taratibu, inaruhusiwa?” alihoji Silinde, ambaye pia ni Waziri kivuli wa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
Kabla ya Silinde kusimama na kuomba mwongozo, Zambi alikuwa amepewa
fursa na Spika ya kuchangia taarifa za Kamati za Bunge za Nishati na
Madini na Miundombinu zilizowasilishwa juzi.
“Jana (juzi) kulitokea maneno maneno fulani hapa bungeni. Alisimama
ndugu Silinde akasema Zambi kala hela hakusafiri,” alisema lakini kabla
hajamalizia kuzungumza Spika alimkatiza... “Naomba hilo uliache
unapoteza muda na haliwasaidii wananchi, changia mambo mengine muhimu,”
alisema Spika Makinda huku wabunge wengi ndani ya Ukumbi wa Bunge
wakipiga makofi.
Hata hivyo, Zambi aliendelea kusisitiza kuwa taswira inayokwenda kwa
wananchi ni mbaya na wameanza kumpigia simu kuwa ameiba fedha na kusema
hilo ni jambo baya analostahili kulisemea.
Alisema utaratibu uko wazi kama hujasafiri unarudisha fedha na kusema...
“Ningekuwa kiongozi wa ajabu sana kama ningekwenda Dubai na Uingereza
na kutokwenda ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutoka
chama kinachotawala.”
Baada ya kueleza hayo, Spika alisimama na kusema: “Waheshimiwa wabunge
nimesema kama mlichukua pesa bila safari, mnarudisha si basi…. Wote
kabisa ninawajua na ninalifanyia kazi. Wote waliochukua pesa warudishe
ndiyo utaratibu wa Serikali na ndivyo inavyotakiwa. Wote watarudisha.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao aliwataka wabunge kutumia
kikao cha kupeana taarifa cha wabunge wote kuzungumza kama kuna tatizo
lolote badala ya kuumbuana ndani ya Bunge.
Moto wa posho hizo ulikolea juzi pale Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM),
Mwigulu Nchemba alipoomba mwongozo wa Spika akitaka kujua hatua ya
mbunge aliyechukua fedha na kwenda safari binafsi. Nchemba alisoma
ujumbe wa simu uliokuwa ukionyesha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani,
Freeman Mbowe alikatisha safari ya Mbunge wa Viti maalumu (Chadema),
Joyce Mukya.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,PIA BOFYA HAYO MATANGAZO UNAYOYAONA KUJIFUNZA VITU VINGI(USIPITWEEEEEEEE)
No comments:
Post a Comment