TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete wiki hii atahudhuria mikutano miwili mikubwa ya kimataifa
ukiwamo wa kujadili amani na usalama Barani Afrika kwa mwaliko wa Rais
Francois Hollande wa Ufaransa.
Kwa mikutano miwili ya kwanza, washiriki walikuwa ni marais wa nchi za
Afrika zilizokuwa makoloni ya Ufaransa lakini mwaka 1976 zilialikwa nchi
zinazozungumza lugha ya Kireno katika Afrika kama watazamaji tu.
Mwaka 1981 jina na madhumuni ya mkutano huo yalibadilika na ukaanza
kuitwa The Conference of Heads of States and Government of Africa and
France na mwaka 1996 mkutano huo ulifunguliwa kwa nchi zote za Afrika
bila kujali zinazungumza lugha gani. Awali mkutano huo ulikuwa
unafanyika kila baada ya miaka miwili, sasa ni kila baada ya miaka
mitatu.
Kama ilivyokuwa mkutano uliopita uliofanyika mwaka 2010 mjini Nice,
Ufaransa, mada kuu ya Mkutano huo ni kujadili amani na usalama katika
Bara la Afrika vikiwemo vita ndani ya nchi mbalimbali, uharamia kwenye
bahari, biashara ya dawa za kulevya, ugaidi na ujambazi wa vikundi na
jinsi mambo hayo yanavyoathiri Afrika na Ufaransa.
Aidha, Mkutano huo utajadili mada nyingine mbili ambazo ni Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Rais Kikwete na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Hollande watakuwa
Wenyeviti-Wenza wa kikao kitakachojadili madhara ya Mabadiliko ya Tabia
Nchi. Rais Kikwete atakuwa Mwenyekiti-Mwenza wa kikao hicho katika
nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa
Afrika (AU)Juu ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).
Rais Kikwete anatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake matokeo ya Mkutano
wa COP19/CMP9 uliofanyika karibuni mjini Warsaw, Poland kujadili suala
zima la Madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mkutano mwingine mkubwa ambao Rais Kikwete atahudhuria ni ule wa marais
wa Afrika utakaojadili jinsi ya Jumuiya ya Kimataifa inavyoweza
kushirikiana kukomesha ujangili na biashara haramu ya pembe za tembo na
faru.
Katika Mkutano huo utakaofanyika Hoteli ya de la Marine, Rais Kikwete
aanatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake kuhusu hatua ambazo
zinachukuliwa na Serikali yake kukabiliana na ujangili nchini chini ya
Operesheni Tokomeza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Desemba, 2013

No comments:
Post a Comment