WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA AWALI KUHUSIANA NA TUKIO LILILOTOKEA MALINYI MKOANI MOROGORO.
Mnamo
tarehe 18/12/2013 majira ya saa tatu asubuhi katika kata ya Malinyi,
tarafa ya Malinyi, wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, kundi la watu
kutoka maeneo mbalimbali kijijini hapo walivamia kituo cha Polisi
Malinyi kwa lengo la kutaka kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa 4 waliokuwa
wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji.
Katika
jitihada za kuhami kituo, askari polisi walitoa tahadhali mbalimbali za
kuwataka wananchi hao watawanyike ikiwemo kupiga mabomu ya machozi,
lakini wananchi hao waliendelea kukaidi amri hiyo. Katika purukushani
hizo za askari kutetea kituo na wavamizi kuendelea kuharibu mali za
kituo ikiwemo kukichoma moto, wananchi 3 walipoteza maisha na wengine 3
walijeruhiwa.
Kufuatia
tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, ametuma
timu maalumu ikiongozwa na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo (CP)
Paul Chagonja kutoka Makao Makuu ya Polisi kwenda kuongeza nguvu
katika Operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na tukio
hilo, ili wafikishwe katika mkondo wa sheria haraka.
Jeshi
la Polisi linalaani vikali tukio hilo linaloashiria vitendo vya
vurugu na uvunjifu wa amani, tukio ambalo limesababisha vifo na majeruhi
pamoja na kujenga hofu miongoni mwa jamii.
Aidha, IGP Mwema ametoa wito kwa
wananchi wa mkoa wa Morogoro hususani wilaya ya Ulanga kata ya Malinyi,
kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wakati
uchunguzi ukiendelea, mtu yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao
anaombwa kutoa taarifa kwenye namba ya simu ifuatayo 0754 78 55 57 au
katika kituo chochote cha Polisi, ili wahalifu hao waweze kukamatwa na
kufikishwa mahakamani.
Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.


No comments:
Post a Comment