
Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
SHIRIKISHO
la soka Tanzania, TFF limemuajiri katibu mkuu wa zamani wa Yanga,
Selestin Mwesigwa kuwa katibu mkuu mpya wa shirikisho hilo.
Rais
wa TFF, Jamal Malinzi imesema kuwa, Mwesigwa alizaliwa mwaka 1970, ana
digrii ya masuala ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na
diploma ya mafunzo ya sheria.
Malinzi
aliongeza kuwa Mwesigwa amefanya kozi kadhaa za masuala ya utawala
ndani na nje ya nchi zikiwemo kozi za utawala wa mpira zilizotolewa na
FIFA.
Rais
huyo alisema Ajira yake ya mwisho ya Mwesigwa ilikuwa Ukatibu mkuu wa
klabu ya Yanga ya Dar es salaam, hivyo ana uzoefu mkubwa wa masuala ya
uongozi ikizingatiwa amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ikiwemo
Plan International.
Aidha,
Malinzi alisisitiza kuwa Mwesigwa alipokuwa katibu mkuu wa Yanga
alishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Bodi ya Ligi kuu na
ule wa Yanga kuingia udhamini na kampuni ya bia ya TBL, hivyo amekidhi
vigezo vya kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya TFF.
TFF pia imemuajiri katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF.
Rais
Malinzi alisema Mtawala ana Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na Shahada ya Uzamili ya uongozi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha
ESAMI.
Rais
aliongeza kuwa Mtawala ambaye ajira yake ya mwisho ilikuwa Ukatibu mkuu
wa Simba Sc , Klabu mwanachama wa TFF, ana uzoefu ambao utasaidia sana
kukabili changamoto mbalimbali za vyama wanachama wa TFF.
Aidha
Rais alisema uzoefu wake na ujuzi wa masuala ya sheria utasaidia
kutatua masuala mbalimbali ya kisheria na kikatiba ndani ya shirikisho
hilo.
Nafasi
ya Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF imeachwa wazi kufuatia waombaji wote
walioomba wa ndani na nje ya nchi kutokidhi vigezo, hivyo kamati ya
utendaji imeagiza nafasi hii itangazwe upya na wale walioomba mara ya
kwanza wasiombe tena.
Rais Malinzi alisema Bwana Idd Mshangama atakaimu nafasi hii kwa sasa mpaka mtu mwingine atakapopatikana.
Pia
nafasi ya Mkurugenzi wa ufundi imebaki wazi baada ya waombaji wote
kutokidhi vigezo, hivyo Bwana Salum Madadi atakaimu nafasi hiyo na Rais
Malinzi ameagiza itangazwe tena na walioomba wasiombe tena.
Nafasi nyingine iliyobaki wazi ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, hivyo itatangazwa tena na kwasasa Bwana Danny Msangi atakaimu.
Afisa habari wa TFF ataendelea kuwa Bwana Boniface Wambura Mgoyo.
Rais
Malinzi alisema ajira zote zitaanza rasmi januari Mosi mwakani na
anawatakia kazi njema, huku akiwa na imani kubwa kuwa watasukuma mbele
gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu.
Katika hatua nyingine, TFF imeteua wajumbe wa kamati ya uchaguzi na kamati ya Rufani ya Uchaguzi na kamati ya soka la ufukweni.
Kamati
ya uchaguzi inaundwa na Mwenyekiti, Wakili Melchesedek Lutema, Makamu
wake, Wakili Walter Chipeta na Wajumbe Hamidu Mahmoud Omar, Jeremiah
John Wambura na Hassan Dalali.
Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF itakuwa chini ya Mwenyekiti , Wakili
Julius Lugaziya, Makamu wake, Wakili Mwita Mwaisaka na Wajumbe Juma
Abeid Khamis, Rashid Dilunga na Masoud Issangu.
Na
kamati ya Soka la Ufukweni itakuwa chini ya Mwenyekiti Ahmed Mgoyi,
makamu mwenyekiti, Shafii Dauda na Wajumbe Deo Lucas, Juma Mgunda,
Boniphace Pawasa, Joseph Kanakamfumu na John Mwansasu.