Askari wa
wanyamapori katika pori la akiba Ugalla, mkoani Tabora, amejeruhiwa
vibaya akiwa na wenzake wakikabiliana na majangili. Meneja wa pori hilo, Japhary Lyimo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana. Lyimo
alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea wakati timu ya askari kutoka pori
hilo, askari kutoka kikosi maalum cha kupambana na ujangili (KDU),
askari wanakijiji wanaozunguka pori hilo (VGS) na wale wa kampuni ya
uwindaji wa kitalii ya Game Frontiers ambao wanamiliki vitalu viwili vya
uwindaji vya Ugunda na Ugalla vilivyoko kwenye pori hilo wakiwa katika
doria.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,(USIPITWEEEEEEEE)
“Askari
wetu Richard Temu, amevunjika mguu wake wa kushoto baada ya kuteleza na
kutumbukia mtaroni wakati wakifukuzana na majangili,” alifafanua Meneja
huyo kwa njia ya simu.
Alisema siku moja kabla ya tukio hilo, walisikia milio ya risasi kwenye eneo la hifadhi, na hivyo kuamua kufanya msako.
Aliongeza kuwa kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers, ilitoa magari
kusaidia usafiri ikiwa ni pamoja na askari wake ambao hata hivyo, wao
hawaruhusiwi kubeba silaha za moto.
“Pori letu linapakana na makazi ya wakimbizi ya Katumba, na taarifa
tulizo nazo wengi wa majangili hujipanga kutokea huko kwa vile wana
silaha nzito," alisema.
Alifafanua kuwa askari Temu aliyejeruhiwa, alikuwa na wenzake watano,
ambapo yeye alikuwa nyuma yao na kutokana na mvua zinazonyesha hivi
sasa, aliteleza na kutumbukia mtaroni na kuvunjika mguu.
"Tunawashukuru wenzetu wa Game Frontiers kwa msaada wao waliotupatia wa
kumsafirisha kwa ndege hadi Dar es Salaam na sasa anatibiwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili Taasisi ya Mifupa," alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Game Frontiers,
Muhsin Abdallah Sheni, alisema askari wake walikuwa wakishirikiana na
wale wa Idara ya Wanyamapori, KDU na VGS kuwasaka majangili hao na
kampuni yake kama wadau wakuu kwenye sekta ya wanyama pori na uhifadhi
wa wanyama, waliona wanao wajibu mkubwa wa kushirikiana nao katika
kuwasaka majangili hao.
“Sisi tuna vitalu vya uwindaji kwenye pori hili, majangili wametuvamia,
kwa hali hiyo hatuwezi kukaa chini tu na kusubiri, ndiyo maana
tulijitolea magari na vifaa vingine ili kuongeza nguvu kukabiliana na
wahalifu hao.
Aidha, Meneja wa pori hilo, Lyimo, ametoa wito kwa wanakijiji wanaoishi
kuzunguka hifadhi hiyo, kuendelea kutoa ushirikiano kwa Idara ya
Wanyamapori kwa kuwa walinzi namba moja kwani uhifadhi wa wanyamapori ni
faida kwao kutokana na mapato yatokanayo na uwapo wa wanyama hao.
“Kwa mfano, asilimia 25 ya mapato yanayotokana na uwindaji wa kitalii
huenda moja kwa moja kwenye halmashauri na kwa maana nyingine huwasaidia
wanakijiji katika maeneo ya afya na elimu,” alifafanua.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
alifanya ziara kwenye mapori ya akiba Selous na Maswa, ili kuwapa moyo
askari wa wanyamapori kutokana na mazingira magumu wanayokabiliana nayo
katika kuwatunza wanyamapori.
Nyalandu alisema serikali inaandaa utaratibu wa kupeleka muswada bungeni
ili kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania ambayo itakuwa
inajitegemea.
Kwa sasa, askari wa wanyamapori wote wako chini ya Idara ya Wanyamapori,
Wizara ya Maliasili na Utalii na utaratibu wa ajira hufuata misingi ya
utumishi wa umma. Aidha, Nyalandu alisema kwa sasa Idara ya Wanyamapori
ina upungufu wa askari 4,700.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment