Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla akichangia jambo bungeni siku za hivi karibuni mjini Dodoma. Picha na Maktaba
Dar es Salaam.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla yuko hatarini kuvuliwa
uanachama wa chama hicho, hatua ambayo endapo itachukuliwa itasababisha
apoteze nafasi yake ya ubunge.
Uongozi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nzega mkoani Tabora tayari
umemjadili Dk Kigwangalla katika vikao vyake vya Kamati za Usalama na
Maadili na Kamati ya Siasa, kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni utovu wa
nidhamu wa mbunge huyo.
Habari
zilizolifikia gazeti hili jana jioni zinasema baada ya vikao hivyo
vilivyofanyika Januari 11 mwaka huu, imeazimiwa kuwa suala la Dk
Kigwangalla pamoja na madiwani watano wilayani humo lipelekwe katika
ngazi ya CCM mkoa na baadaye taifa.
Dk
Kigwangalla jana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema: “Hata
mimi nimesikia taarifa hizo, isipokuwa sijapewa taarifa rasmi. Ila
nafahamu kwamba vikao vya chama vilikuwepo na mimi niliitwa ila kama
ambavyo nimeshasema siwezi kuhudhuria”.
Gazeti
hili lilimtafuta Mbunge huyo machachari kutokana na taarifa yake
aliyoitoa kwenye mitandao ya Facebook na Tweeter akieleza kuhusu taarifa
za kuwapo mpango wa kumfukuza uanachama.
Kupitia
mitandao hiyo Dk Kigangwalla aliandika: “Nimepokea taarifa kuwa
madiwani walioungana na wananchi wa Nzega pamoja na mimi kupinga uamuzi
wa Baraza la Madiwani kuzigawa pesa kwenye Kata wameadhibiwa na Kamati
ya Siasa ya Chama Wilaya ya Nzega, bila kusikilizwa na ilhali miongoni
mwa ‘mahakimu’ hawa ni watu waliokuwa wakilalamikiwa na madiwani na
wananchi. “
Mbunge
huyo aliongeza: “Nimepewa taarifa kuwa mapendekezo ya adhabu dhidi
yangu kutoka wilayani kwenda vikao vya juu, ...tena bila kusikilizwa
maana nilitoa udhuru, ni kuwa ninyang’anywe kadi ya uanachama wa CCM.
Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi chama kinavyoendeshwa
Nzega.”
Mbunge
huyo alisema anaamini viongozi wakuu wa CCM wanafuatilia kwa karibu
suala hilo na watachukua hatua stahiki, huku akisema hatahudhuria tena
kikao chochote cha CCM wilayani humo.
“Kama
chama hiki kimefika huku, kwamba kuna watu wana nguvu kuliko chama,
kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa kuwa wana vyeo na mamlaka
ya kufanya hivyo na hakuna wa kuingilia kati na kusema ‘no’, basi sina
haja ya kuendelea kupambana,” aliongeza.
Aliendelea:
“Nimechoka, sintokata rufaa wala sintolalamika tena. Watekeleze hukumu
hiyo. Sintojitetea na sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa,
nimechoka kupambana na watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa
mnyonge, lakini ukabaki na uhai, uzima, heshima na furaha yako”.
Kauli ya CCM Nzega
Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda alikiri Dk Kigwangwalla kujadiliwa
katika vikao vya chama vya wilaya, ikiwamo Kamati ya Siasa.
Alisema
makosa ya Mbunge huyo ambayo yalijadiliwa katika kikao hicho ni kufanya
mkutano wa hadhara na kuwaporomoshea matusi madiwani wenzake ambao
hawakuwa upande wake wakati wakijadili mgawo wa fedha.
Mwenyekiti
huyo alisema CCM baada ya kuona mgogoro huo wa madiwani wake unakua,
kiliamua kuwajadili watuhumiwa na kwamba uamuzi wa kikao hicho ni siri.
Alisema CCM bado inaendelea kumjadili mbunge huyo na kwamba kikao kingine kitafanyika Februari mosi mwaka huu.
Alisema uamuzi wa kikao hicho utapelekwa CCM Mkoa wa Tabora na wao watalijadili na kupeleka mapendekezo yao chama taifa.
Chimbuko la mgogoro
Mgogoro
uliokigawa CCM katika Wilaya ya Nzega, unatokana na tofauti za
kimtazamo kuhusu jinsi ya kutumia fedha Sh2.3 bilioni zilizotolewa na
Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Resolute kama kodi ya huduma kwa
halmashauri ya wilaya hiyo.
Dk
Kigwangalla pamoja na madiwani kadhaa wanapinga kupindishwa kwa azimio
la Baraza la Madiwani ambalo lilielekeza fedha hizo zitumike kuanzisha
Benki ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya
Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd -
NCCCL).
Lengo
la Kampuni ya NCCCL lilikuwa ni kujenga uwezo kwa kuwa na vifaa vya
ujenzi wa barabara za halmashauri na mashine ya uchimbaji wa visima kwa
ajili ya huduma za maji.
Hata
hivyo, wakati utekelezaji wa azimio hilo ukiwa umeanza, Januari 4 mwaka
huu kiliitishwa kikao cha dharura kwa lengo la kubadili maazimio ya
awali.
Zamu
hii madiwani wakiungwa mkono na uongozi wa CCM wa wilaya walikuja na
mpango kwamba fedha hizo zigawanywe kwenye kata, azimio ambalo
linapingwa vikali na baadhi ya madiwani wakiongozwa na mbunge huyo.
Baada
ya azimio jipya kupitishwa, Dk Kigwangalla aliitisha mkutano wa hadhara
na kuwahutumia wananchi na mwishoni mwa mkutano huo wananchi waliazimia
kufungua kesi mahakamani kuzuia kutumika kwa fedha hizo.
Ni
katika mkutano huo ambapo Dk Kigwangalla anadaiwa kuwatusi baadhi ya
madiwani waliokuwa kinyume na yeye, matamshi ambayo yamesababisha
kuanzishwa kwa mchakato wa kumvua uanachama.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment