Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, January 29, 2014

LIGI KUU YA VODACOM : YANGA 0 - 0 COASTAL

Kikosi cha Young Africans kilichoanza dhidi ya Coastal Union
Young Africans imetoka sare ya bila kufungana (0-0) dhidi ya wenyeji timu ya Coastal Union katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom uliofanyika leo katika dimba la Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kikosi cha Young Africans kilianza mchezo kwa kasi na kulishambulia lango la Coastal Union kwa dakika 15 za mwanzo na kukosa bao la wazi kupitia kwa mshambuliaji wake Saimon Msuva ambaye alichelewa kuunganisha krosi ya David Luhende na mpira huo kuokolewa na mabeki na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Baada ya mashambulizi ya mfululizo Coastal Union waliamka na kusanza kulisakama lango la Young Africans lakini mashmabulizi yao yalikuta yakiishia mikononi mwa mlinda mlango Dida ambaye pia washabiki wa Coastal walianza kumrushia chupa za maji na mawe.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Coastal Union 0 - 0 Young Africans
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi tena kwa Young Africans kulisakama lango la wagosi wa Kaya kwa lengo la kupata bao la mapema lakini ukuta wa Coastal Union uliendelea kusimama imara na kuondoa hatari zote langoni mwao.
Coastal walifanya shambulizi langoni mwa Young Africans kupitia kwa Haruna Moshi "Boban" Lutimba Yayo na Keneth Masumbuko lakiini umakini wa safu ya ulinzi wa Watoto wa jangwani ulikuwa kikwazo kwao kuweza kupata bao.
Dakika za lala salama Young Africans walifanya mashambulizi kupitia kwa Kavumbagu, Msuva, Tegete na Niyonzima lakini bado hawakua na nafasi nzuri ya kumalizia mashambulizi yao na kujikuta yakiwa mikononi mwa mlinda mlango wa Coastal Union Kado
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Coastal Union 0 - 0 Young Africans.
Mchezo wa leo ulikuwa ni wa pili katika mzunguko huu na ikumbukwe pia katika mchezo wa awali timu hizi zilitoka sare ya mabao 1-1 mchezo uliofanyika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kocha mkuu wa Young Africans mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema vijana wamejitahid kucheza vizuri katika mchezo wa leo tofauti na mchezo uliopita, lakini ubovu wa uwanja na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo wa leo yalikuwa yanakela na kuwakatisha tamaa wachezaji wake.
"Tazama wachezaji wangu wamechezewa madhambi mara nyingi na wachezaji wa Coastal Union lakini mwamuzi hajaweza kumuonyesha kadi hata mchezaji mmoja katika mchezo hali iliyopelekea kuwa mchezo wa kibabe na kuumizana" alisema Hans
Mara baada ya mchezo wa leo, Young Africans kesho itarejea jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa jumapili dhidi ya timu ya Mbeya City utakaofanyika uwanja wa Taifa. 
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite, 3.Oscar, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Domayo, 7.Msuva, 8.Niyonzima, 9.Didier, 10.Ngasa/Nizar, 11.Luhende/Tegete
Coastal Union: 1.Kado, 2.Hamad, 3.Banda, 4.Kibacha, 5.Nyosso, 6.Santo, 7.Lyanga, 8.Odula, 9.Yayo,10. Boban, 11.Masumbuko

No comments:

Post a Comment