Wananchi
wa Dumila mkoani Morogoro wakitumia uzoefu wao wa kuogelea kujinusuru
na mafuriko yaliyotokea jana na kuhatarisha maisha ya watu wengi ikiwa
ni pamoja na kuharibu madaraja. Picha na Lilian Lucas
Morogoro. Mafuriko
makubwa yametokea katika Kata ya Dumila, Kilosa mkoani Morogoro na
kusababisha mamia ya watu kupoteza makazi huku daraja la Mto Mkundi
linaloziunganisha Wilaya za Kilosa na Mvomero likivunjika.
Mafuriko
hayo yalisababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha jana alfajiri na
kusababisha maafa makubwa yakiwamo kuharibiwa kwa makazi ya watu,
majengo ya Serikali zikiwamo shule, vyuo na mahakama.
Habari
zinasema mafuriko hayo pia yalichangiwa na mvua kubwa iliyoanza
kunyesha usiku wa kuamkia jana katika sehemu za milima iliyopo Kilosa na
Mvomero, hivyo Mto Mkundi kushindwa kuhimili maji hayo.
Mashuhuda
walisema waliona maiti ya mtu ikielea kwenye maji yaliyokuwa yakipita
kwa kasi, tukio ambalo lilithibitishwa na Diwani wa Kata ya Magole, Juma
Rajabu Chewe. Chewe alisema maiti hiyo ilionekana ikielea eneo la
Mateteni na kwamba taarifa zilitolewa polisi ili aopolewe. Hadi jana
jioni idadi ya watu walioathiriwa na maafa ilikuwa bado haijafahamika.
Maji
yasambaa kwenye vijiji mbalimbali vinavyozunguka mto huo na
kuwalazimisha baadhi ya watu kulazimika kujiokoa kwa kupanda kwenye paa
za nyumba zao huku wengine wakikwea juu ya miti.
Baadhi
ya watu walikutwa na mafuriko hayo mashambani na walipozidiwa na nguvu
ya maji walijiokoa kwa kushikilia vitu mbalimbali ikiwamo miti, huku
baadhi yao wakipoteza nguo walizokuwa wamevaa walipokuwa kwenye harakati
za kujiokoa.
Polisi
waliofika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji walilazimika kuomba helikopta
kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar es Salaam ili kuwaokoa watu
waliokuwa kwenye paa za nyumba na kwenye miti iliyokuwa imezungukwa na
maji.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitaka kuwapo kwa uvumilivu wakati
Serikali ikiendelea na taratibu za kuwaokoa walioko juu ya miti na kutoa
misaada kwa walioathirika.
Alisema
kuwa kutokana na hali kuwa mbaya, ofisi yake ililazimika kuomba
helikopta kwa ajili ya kuongeza nguvu ya juhudi za uokoaji.
Taharuki kubwa
Mafuriko
hayo yalizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutawanyika ovyo wakiwa
hawajui cha kufanya, kutokana na nyumba zao kuharibiwa na mali zao
hususan mazao yakisombwa na maji.
Hali
ilikuwa mbaya zaidi kwa kina mama wakiwa na watoto ambao walionekana
katika makundi wakiomba msaada baada ya kukimbia makazi yao, huku wengi
wakiwa wamelowa kutokana na kunyeshewa.
Mwanamke
aliyejitambulisha kwa jina la Zahra Maulid alisema wanapata taabu na
watoto kwani hawajui watakula nini baada ya mazao yao ukiwamo mpunga,
mahindi na alizeti kusombwa na maji.
“Hapa
hata hatujui tutaishi vipi maana vyakula vyetu vyote vimesombwa na
maji, tunachoomba Serikali itupatie msaada wa haraka na mpaka sasa
hatujui mlo wetu wa leo na hata wengine hawana makazi,”alisema Zahra.
Habari
zaidi kutoka Dumila zilisema, madarasa ya Shule ya Msingi Magole, nayo
yalifunikwa na maji na wanafunzi waliokuwamo walijiokoa kupita
madirishani.
Majengo
ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Dakawa, Chuo cha Veta Dakawa na
Mahakama ya Mwanzo Dakawa nayo yaliharibiwa na mafuriko hayo.
Wanafunzi
wa Sekondari ya Dakawa walikuwa nje ya mabweni wakisubiri maji kukauka.
Majalada ya kesi mbalimbali katika Mahakama ya Mwanzo Dumila yalilowa
maji, huku tope zito likionekana ndani ya chumba cha mahakama hiyo.
Mafuriko
hayo pia yalisababisha kusombwa kwa nguzo za umeme na kufungwa kwa
barabara nyingine kadhaa kutokana na miti mikubwa kukatika na kutanda
katika barabarani hizo.
Pia vituo 11 vya treni vilivyoko mkoani Morogoro vimeathirika kutokana na mafuriko baada ya kusombwa na maji.
Magari yakwama
Magari
zaidi ya 5,000 yaliyokuwa yakitokea Dar es Salaam, Tanga na Pwani
kuelekea Bara na yale yaliyokuwa yakitokea Bara kwenda Dar es Salaam
yalikwama huku, mengine yakigeuza na kurejea yalikotoka.
Abiria
aliyekuwa katika moja ya mabasi yaliyokwama, Godfrey Wambura
alilalamikia kukosekana kwa huduma za kijamii katika eneo hilo na kwamba
bidhaa muhimu zilikuwa zimeanza kuuzwa kwa bei ghali. Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye alifika mapema kwenye eneo hilo,
alishauri magari yaliyotokea yanatokea upande wa barabara kurudi Dodoma
na kwenda Iringa kwa ajili ya kuja Dar es Salaam.
Meneja
wa Wakala wa Barabara (Tanroads) wa Mkoa wa Morogoro, Doroth Mtanga
alisema haifahamiki ni hasara gani iliyotokana na kuvunjika kwa daraja
hilo.
Wakati
huohuo, jana Serikali ilitangaza kufunga Barabara ya Morogoro – Dodoma
kuanzia jana, na kuwashauri wale wenye safari za lazima kutumia barabara
mbadala kwani eneo la Dumila halipitiki.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi
aliliambia gazeti hili jana jioni kuwa: “Magari yanayoendelea kutumia
barabara hiyo yanaweza kusababisha maafa zaidi maana eneo hilo
halipitiki, lakini kibaya zaidi Kijiji cha Dumila ni kidogo, hakiwezi
kuhimili idadi ya watu wote waliokwama na watakaokwama.”
Aliongeza:
“Magari yanayotoka Dar es Salaam yapitie Chalinze – Arusha – Babati -
Singida – Mwanza na yale yanayotoka Mbeya yatumie Barabara ya Iringa –
Dodoma – Arusha – Kondoa kuelekea Arusha au Mwanza.”
Alisema
mafundi wameanza kazi ya kurejesha hali ya kawaida katika daraja
lililobomoka na kwamba barabara hiyo imefungwa kuanzia jana na
itaendelea kufungwa leo, huku akiwashauri madereva wa magari yaliyoko
katika eneo hilo waondoke na kurejea yalikotoka.
Kuhusu
waliopatwa na maafa, waziri huyo alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera ilikuwa eneo
la tukio kufanya tathmini ya maafa hayo.
“Hapa
kwetu tumekusanya mahitaji ya chakula, mablanketi, mahema na vyote
hivyo vinaondoka jioni hii (jana) kwa gari la jeshi kwenda eneo la
maafa,” alisema Lukuvi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment