Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka. PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam/Mbeya. Viongozi
wa vyama vya siasa na wanaharakati wa masuala ya ardhi, wamesema
kuzomewa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka ni matokeo ya makosa yanayowafanywa na Serikali
kuwapendelea wawekezaji wa nje na kuwapuuza wananchi.
Kauli
hiyo imekuja siku moja baada ya Profesa Tibaijuka kuzomewa na wananchi
waliokerwa na kitendo cha kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki shamba
la Kapunga, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya lenye ukubwa wa hekta 7,370.
Wananchi
hao walikasirishwa na kitendo cha Profesa Tibaijuka kubadili msimamo
wake awali wa kumpokonya ardhi mwekezaji huyo kwani mara ya kwanza
alishawaeleza viongozi wa vijiji kuwa serikali itawarudishia eneo lao.
Mwekezaji
huyo alitakiwa kumiliki ekari 5,500 lakini serikali ilimmilikisha ekari
nyingine 1,870 ambazo ni mashamba ya wanakijiji.
Mkurugenzi
wa Taasisi ya Haki Ardhi, Yefuz Myenzi alisema hayo ni makosa ya
serikali kuwapa ardhi wawekezaji wa nje bila kutenga ardhi ya
wanavijiji.
“Serikali
inabinafsisha hadi vijiji ambako wananchi wangeweza kulima na kuendesha
maisha yao, unategemea nini wakimwona kiongozi wa serikali ni lazima
watamzomea,” alisema Mnyezi.
Alisema
ubinafsishaji wa ardhi unafanywa na ngazi za juu za taifa bila
kuushirikisha uongozi wa ngazi za vijiji hali inayosababisha vurugu
katika maeneo mengine.
“SiYo
katika Shamba la Kapunga tu, kuna maeneo mengi ambako wawekezaji wa
kigeni wamepewa ardhi lakini wao wanaikodisha kwa wananchi kitendo
ambacho ni kosa,” alisema.
Myenzi
alisema katika maeneo yenye matatizo kama hayo, Rais anatakiwa kutumia
madaraka yake kwa kubadilisha matumizi ya ardhi ili wananchi waweze
kupewa kwa ajili ya kilimo.
Viongozi wengine
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema viongozi wa Serikali
wanawapendelea wawekezaji wa nje na kuwapuuza wanavijiji.
“Migogoro
hii ya ardhi inavyochukiza watu kama kiongozi utakwenda kusuluhisha na
kutoa majibu yasiyowaridhisha wananchi, basi viongozi wataendelea
kuzomewa kama Waziri huyo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema wananchi wanakatishwa tamaa na viongozi wa serikali kuwapendelea wawekezaji.
“Ajira
pekee inayotegemewa vijijini ni kilimo, serikali inabinafsisha hadi
mashamba ya wanavijiji, wamekata tamaa ndiyo maana wanazomea ovyo.
Viongozi hawana nia ya dhati kutatua migogoro iliyopo,” alisema.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu Mkuu wa NCCR -Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema ili
kuondokana na migogoro, wawekezaji wanatakiwa kuwa na vibali vya ardhi
kutoka katika uongozi wa kijiji.
“Wanakijiji ndiyo wenye ardhi, migogoro ya namna hii isingetokea kama wangeshiriki kutoa vibali kwa wawekezaji,” alisema.
DC amtetea Tibaijuka
Mkuu
wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kifu amesema pamoja na kwamba
wananchi wa kijiji cha Kapunga wanataka mgogoro huo umalizike haraka,
lakini anaamini uamuzi wa Profesa Tibaijuka kufanya mazungumzo na
mwekezaji wanayevutana naye utaleta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Profesa
Tibaijuka alisema majuzi kuwa Kampuni ya Kapunga Rice Project inamiliki
kihalali mashamba kwenye eneo hilo na kudai kuwa serikali ndiyo yenye
makosa kwenye mgogoro huo.
Mashamba
hayo mara ya kwanza yalikuwa yanamilikiwa na Kampuni ya Taifa ya Kilimo
(Nafco) lakini yalibinafsishwa na kuchukulikuwa na mwekezaji huyo.
Kifu
alisema pamoja na kwamba wananchi wengine hawakuridhika na uamuzi wa
Waziri lakini anaamini kuwa Profesa Tibaijuka ndiyo yuko sahihi
kuzungumza na wawekezaji ili waliachie eneo hilo kwani hawana makosa.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment