Wakati
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwasili mjini Dodoma, Ofisi ya
Bunge imetangaza kuandaa utaratibu wa malazi kwa wajumbe hao katika
hoteli mbalimbali mjini humo.Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge na Katibu wa
Baraza la Wawakilishi, jumla ya hoteli 27 zimeainishwa kuwapokea wajumbe
hao 640 ambao wanatarajiwa kuwapo mjini Dodoma kwa muda wa miezi
mitatu.
Pamoja na
utaratibu wa malazi, taarifa hiyo pia iliagiza wajumbe hao kuwasili
wakiwa na nakala halisi za vitambulisho vitakavyotumika kwa ajili ya
usajili.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa usajili utafanyika leo na kesho kwenye Ofisi za
Bunge, ambapo zoezi hilo litajumuisha ujazaji wa fomu, upigaji picha za
vitambulisho sambamba na kukabidhiwa vitendea kazi.
Baada ya
zoezi hilo Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi watakutana
na wajumbe kwa ajili ya kutoa maelekezo ya awali yanayohusiana na
utaratibu wa ukaaji, jiografia ya viwanja vya Bunge na huduma za
utawala.
Kikao cha
kwanza cha mkutano huo kitafanyika Jumanne ijayo, ambapo pamoja na
masuala mengine kitahusisha uchaguzi wa mwenyekiti wa muda
atakayesimamia upitishwaji wa kanuni na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge
hilo.
Wiki
iliyopita Ikulu ilitangaza majina ya wajumbe 201, yaliyoteuliwa na Rais
Jakaya Kikwete kushiriki katika uchambuzi wa Rasimu ya Pili ya Katiba na
kutengeneza Katiba Mpya.
Mbali ya wajumbe wa Bunge la Katiba, pia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wako Dodoma wakiendelea na vikao vyao.
Mji wafurika wageni
Kutokana
na kuwapo kwa ugeni huo, Mji wa Dodoma umefurika wageni wakiwamo wajumbe
wa Bunge la Katiba na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC)
huku, maeneo mengi yakionekana kufanyiwa usafi.
Hata
hivyo, wageni wengi walionekana kuingia jana na baadhi ya watumishi wa
hoteli hizo walikiri kuwasajili baadhi ya wageni, ambao wapo katika
orodha hiyo.
Gazeti
hili jana lilishuhudia kukiwa na maandalizi ya mwisho kwa ajili ya
mapokezi hayo, huku baadhi ya maeneo yakiendelea kukarabatiwa ikiwamo
kupaka rangi.
No comments:
Post a Comment