Zitto Zuberi Kabwe
Kesi
ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Zitto Kabwe dhidi ya chama chake hicho inatarajiwa kuanza
kutajwa leo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alifungua kesi hiyo dhidi ya
Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, akiiomba
mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa
anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa,
itakaposikilizwa.
Katika
kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia aliiomba mahakama hiyo imwamuru
Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za Kikao cha Kamati
Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya chama
na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake
kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kesi
hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji John Utamwa imepangwa kuanza kutajwa
leo kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa rasmi.
Tayari mahakama imeshatoa amri ya zuio la muda kwa Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Uamuzi huo ulitolewa Januari 7 na Jaji Utamwa, kutokana na maombi ya Zitto, kupitia kwa Wakili wake Albert Msando.
Awali
mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na
Mkurugenzi wake wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala
walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la
muda.
Katika
uamuzi wake, Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa
maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
No comments:
Post a Comment