Wakati kuna joto la vyombo vya habari vya kimataifa kuituhumu Tanzania
kuwa haipambani na ujangili, Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali
imeubaini mtandao unaojumuisha watu 40, akiwemo tajiri maarufu mkoani
Arusha.Akihojiwa juzi jioni na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Rais Kikwete alikanusha taarifa zilizotolewa na gazeti la Sunday Mail
la Uingereza zilizodai Tanzania haijafanya juhudi za kupambana na
ujangili wa meno ya tembo, akisema taarifa hizo ni uzushi na upuuzi
mtupu.“Gazeti
hilo limezungumza na nani, ndiyo maana sitaki kupoteza muda kujadili
upuuzi, achana na mambo hayo. Ndiyo maana tunasema, akutukanaye
hakuchagulii tusi,” alisema Rais Kikwete.Alisema
inashangaza kuona watu wanaozusha taarifa hizo hawaoni jinsi
tulivyofanya jitihada za kutokomeza ujangili, kama operesheni za
tokomeza ujangili na operesheni kipepeo.Kuhusu
majangili 40 ambao wametambuliwa, Rais Kikwete alisema wameutambua
mtandao mkubwa wa majangili unaoongozwa na mfanyabiashara mkubwa wa Arusha Mjini.“Kuna
majangili 40 waliotambuliwa na tumetambua mtandao mzima, pale Arusha
kuna mtu mkubwa alikuwa anaendesha biashara. Kazi ilikuwa ni kutambua
mtandano wote, ule mtandao ni mpana sana,” alisema Rais Kikwete.
Katika
mahojiano hayo, Rais Kikwete alisema, Tanzania ilikuwa ni nchi yenye
tembo wengi zaidi duniani, lakini ujangili ulipokithiri, tembo
walipungua na kufikia 57,000 tu mwaka 1987.
“Mwaka
1989, Taasisi ya Kimataifa ya Cites, walipiga marufuku biashara ya meno
ya tembo duniani na ujangili ulipungua kwa kiasi kikubwa hivyo tembo
waliongezeka na kufikia, 110,000 mwaka 2009,” alisema.
Kikwete ahojiwa CNN
Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa vita dhidi ya ujangili ni tatizo sugu linaloielemea Tanzania.
Wakati
idadi ya tembo ikiendelea kupukutika kila siku, vita dhidi ya ujangili
ilichukua sura mpya mwishoni mwa mwaka jana baada ya operesheni
iliyofahamika kwa jila la Tokomeza Ujangili, kukumbwa na kashfa ya
ukiukwaji wa haki za binadamu na kusababisha mawaziri wanne kujiuzulu.
Mawaziri
waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.
Akizungumza katika kipindi cha Televisheni ya CNN ya Marekani kinachoendeshwa na mtangazaji, Christiane Amanpour, Rais Kikwete alisema vita dhidi ya ujangili ina changamoto kubwa.
“Hizo
ni changamoto tunazokumbana nazo. Baada ya kuona wahifadhi wanaelemewa
na mzigo, niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie na walifanya. Baada ya
kuona polisi wenyewe wanashindwa, tukaweka wanajeshi na hiyo ilikuwa
operesheni tokomeza ili kupambana na majangili,” alisema na kuongeza:
“Wao
walikamata hadi wafugaji na ng’ombe wao. Hapo ndipo kulikuwa na ripoti
za uvunjifu wa haki za binadamu, tukasema hilo halikubaliki. Ndiyo maana
mawaziri wanne waliwajibika na kusimamisha operesheni ili kuangalia
upya.”
Hata hivyo, alisema kuwa operesheni hiyo itaendelea siku za usoni.
Akifafanua zaidi jinsi Serikali ilivyochukua hatua, Rais Kikwete alisema:
“Wakati
wa uhuru Tanzania ilikuwa na tembo 350,000… Mwaka 1987 walibaki
55,000…Juhudi za kupambana na ujangili zimeanza muda mrefu. Tangu mwaka
1989 kulikuwa na Operesheni Uhai na tulifanikiwa, kwani mwaka 2009 idadi
ya tembo ilifikia 110,000,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mwaka
2010 kulizuka aina nyingine ya ujangili na hii ni ya upuuzi kabisa. Kwa
mfano katika pori moja kulikuwa na tembo 30,000 na wote walikwisha… Ni
jambo gumu sana.”
Ili
kuendeleza mapambano hayo, Rais Kikwete pia amezitaka nchi
zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika ili ziweze kupambana.
“Wito
wangu na viongozi wengine wa Afrika ni kwamba, kwanza ili kupambana
katika vita hii, lazima kuwe na rasilimali watu, kuajiri askari wa
wanyamapori na wapewe mafunzo,” alisema na kuongeza:
“Nchi
zilizoendelea kama Uingereza na Marekani watatusaidia katika mafunzo na
vifaa, silaha, uangalizi na vyovyote vile watakavyojitolea.”
Alipoulizwa kuhusu upigaji marufuku kama ilivyofanywa na Marekani, Rais Kikwete alisema ipo dhamira ya kufanya hivyo.
“Tunazo
zaidi ya tani 112 za meno ya tembo na tunafikiria hilo. Tulikuwa na
wazo la kuomba kibali cha kuyauza, lakini tumeghairi huu siyo wakati
wake. Kwa sababu ingekuwa ni kufungua mlango wa biashara hiyo,”
“Wito
wangu ni kupiga marufuku biashara hiyo. Kama hakutakuwa na mahitaji ya
meno ya tembo hakutakuwa na sababu ya kuua tembo. Hivyo wataishi
salama.”
Alipoulizwa
kuhusu utajiri wa rasilimali wakiwemo wanyamapori, gesi na madini, Rais
Kikwete alikiri kuwa haziwanufaini Watanzania licha ya takwimu za
uchumi kuongezaka.
“Uchumi
wa Tanzania unakuwa kwa asilimia saba kwa mwaka, lakini ukuaji huo ni
kwenye sekta za mawasiliano, uchukuzi na viwanda. Kwa hiyo mtu mtaani
anajiuliza, au sijasikia vizuri, anafikiria mbona bado ni maskini,
hakuna umeme, maji huduma za afya.
“Wakati
uchumi unakua hivyo, uondoaji wa umaskini unakua kwa asilimia mbili na
tathmini yetu kwa hii asilimia saba inachangiwa na sekta za mawasiliano,
usafirishaji na viwanda.”
Awali mtangazaji Amanpour alinukuu baruapepe ya Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la ‘Car washer’ (muosha magari) akisema:
“Watu
pekee wanaofaidika na ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa gesi ni viongozi
wa Serikali huku wananchi wengi wakiogelea kwenye umaskini.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alikanusha:
“Kusema kwamba tunapata zaidi ya Dola 100,000 ni upotoshaji. Hata hivyo, nasema wazo hilo ni zuri..,” alisema na kuongeza:
“Sekta
inayoajiri watu wengi ni kilimo na inakua kwa asilimia nne. Sasa kama
kilimo kitakua haraka kama sekta nyingine basi tutaendelea. Jinsi ya
kufikia hapo ndiyo tunafanyia kazi, ndiyo mchango wangu,” alisisitiza.
Kuhusu haki za mashoga, Rais Kikwete alionyesha kusita kukubaliana na hoja hiyo kwa Tanzania:
“Itachukua muda kwa watu wetu kukubali mila za Magharibi. Siwezi kusema sasa kwamba niko tayari… haiwezi kutokea kwa sasa.
“Haiwezi
kutokea Tanzania … Nakumbuka wakati fulani Waziri Mkuu wa Uingereza,
David Cameron aliwahi kuibua jambo hilo na lilileta malumbano mengi.
Wakati huo pia kulikuwa na ziara ya Mwanamfalme, Prince Charles. Kwa
hiyo hilo bado,” alisema Rais Kikwete.
Nyalandu
Serikali
imeacha nia yake ya awali ya kuwasilisha ombi la kukubaliwa kuuza akiba
ya pembe za ndovu katika chombo cha kimataifa kinachosimamia biashara
ya wanyapori (CITES), ikiwa ni hatua ya kuunga mkono vita dhidi ya
biashara haramu ya meno ya tembo.
Msimamo
huo ulitolewa juzi jijini London, Uingereza na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu wakati wa mkutano wa kimataifa unaojadili namna
ya kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori duniani (Conference on
Illegal Wildlife Trade).
Akiwasiliana
na Mwananchi kwa njia ya mtandao jana, Meneja Uhusiano wa Shirika la
Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alimkariri Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akisema uamuzi huo umefikiwa baada
ya kutia saini makubaliano ya kushiriki harakati za taasisi ya Hillary
Clinton ya Clinton Global Initiative inayopigania kupiga marufuku kwa
biashara ya meno ya tembo.
Waziri
Nyalandu alitumia mkutano huo kuelezea juhudi na mafanikio ya Tanzania
katika vita dhidi ya ujangali ambapo alisema hadi mwishoni mwa mwaka
jana zaidi ya watuhumiwa 320 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Jumuiya
ya Ulaya (EU), Bara la Asia (China) na Afrika walitiwa mbaroni kwa
kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.
“Katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tani 19.7 za meno ya tembo
zilikamatwa katika maeneo mbalimbali duniani kati ya hizo, tani 15.2
zilikamatwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na vyombo mbalimbali
ikiwemo Jumuiya ya Kimataifa,” Shelutete alimkariri Waziri Nyalandu
akiueleza mkutano huo.
Alisema
Serikali itafanya sensa kubwa katika hifadhi na mapori ya akiba nchini
kubaini idadi kamili ya tembo waliopo huku akibainisha kuwa hadi sasa,
utafiti unaonyesha kuwa tembo walioko ndani ya maeneo ya hifadhi wako
salama zaidi kulinganisha na walioko nje ya hifadhi.
Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti imetajwa kama moja ya hifadhi salama kwa tembo
barani Afrika baada ya kufanikiwa kudhibiti idadi ya tembo wanaouawa
kutoka watatu kwa mwezi hadi sifuri katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita.Mwaka
jana, Serikali ilifanya sensa ya tembo katika mifumo wa ya kiikolojia
ya Selou-Mikumi na Ruaha-Rungwa na kubaini kuwa katika ikolojia ya
Selou-Mikumi, idadi ya tembo katika mfumo wa ikolojia ya Selou-Mikumi
imepungua kutoka 38,975 mwaka 2009 hadi 13, 084 mwaka jana, huku katika
mfumo wa kiikolojia wa Rwaha-Rungwa wakipungua kutoka 31,625 hadi
20,000.Rais
Jakaya Kikwete anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo
ulioitishwa na Serikali ya Uingereza na kuhudhuriwa na washiriki kutoka
zaidi ya nchi 47 duniani pamoja na mashirika 13 ya kimataifa.
Pamoja
na mambo mengine, mkutano huo unajadili jinsi ya kuimarisha usimamizi
wa sheria, mchango wa mfumo mzima wa sheria za jinai katika kukabiliana
na biashara haramu ya Wanyamapori.
Mengine
ni jinsi ya kupunguza mahitaji ya bidhaa zitokanazo na wananyamapori,
maendeleo endelevu kwa jamii zilizoathiriwa na biashara haramu ya
wanyamapori na mikakati ya kuwanusuru wanyama kama tembo, faru, tiger na
makundi mengine ya wanyama wanaolengwa na wawindaji haramu kutokana na
thamani ya pembe na ngozi zao.
-MWANANCHI–
No comments:
Post a Comment