Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, February 12, 2014

TWIGA STARS YAAGWA LEO, YAAHIDI USHINDI







 TIMU ya Taifa ya Wanawake inaondoka nchini kesho saa mbili asubuhi kwenda nchini Zambia na ndege ya Kampuni ya Fastjet ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri.

Twiga stars inakabiliwa na mechi ya kwanza ya mchujo dhidi ya Zambia ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika baadaye mwaka huu jijini Windhoek, Namibia.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wachezaji wa Twiga, Mgeni rasmi Katibu wa Kamati ya Olympiki Tanzania, Filbert Bayi alisema kuwa ana imani na timu hiyo kwani ni ina wachezaji ambao wamekaa pamoja kwa muda mrefu.

“Nakumbuka 2011 timu hii ikiwa na baadhi ya wachezaji ninaowaonana hapa ilishiriki kwenye mashindano ya Olympiki Afrika hivyo naamini itafanya vizuri”, alisema Bayi.

Pia Bayi alisema anampongeza kocha Kaijage kwa kazi yake nzuri ya kufundisha na kurejesha heshima kwa Twiga kwani wanaonekana nadhifu kama wanawake.

Naye kocha Kaijage alisema kuwa anashukuru timu yake ipo vizuri kwani imejiandaa vya kutosha hivyo wana uhakika watakwenda kufanya vizuri.

Naye nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili alisema wanaamini watafanya vizuri kulingana na mafunddisho waliyoyapata kwa kocha wao ila dua na sapoti za watanzania zinahitajika ili wafanye vizuri zaidi.

“Sisi tupo vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo huo wa ugenini ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele ila tunawaomba watanzania watupe sapoti na dua zao”, alisema Sophia
Twiga Stars inaondoka na kikosi cha wachezaji 19 na benchi la ufundi lenye watu watano mechi hiyo itakayooanza saa 9 kamili kwa saa za Zambia. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment