1.0 UTANGULIZI
Mamlaka
ya Mawasiliano imepokea matokeo ya tathmini ya zoezi la uhamaji toka
mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda kidijiti. Zoezi hili lilifanyika
kwenye miji saba kama ilivyotajwa kwenye taarifa iliyotolewa na
wataalamu wa Chuo kikuu cha Dar e salaam waliofanya tathmini ya Uzimaji
wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya Kwanza.Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifanya kamisheni kwa Chuo Kikuu cha
Dar es salaam kufanya tathmini ya uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika
Awamu ya Kwanza, ikitambua kuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuna
wataalamu wenye uzoefu mkubwa wa kufanya tathmini za aina mbalimbali, na
kwamba uzoefu huo utasaidia sana kuhakikisha kuwa tunapata taarifa ya
uhakika itakayotuwezesha kuboresha zoezi hili kwenye awamu inayofuata.Nachukua
nafasi hii kuwapongeza wataalamu waliohusika katika tathmini hii kwa
weledi wao kwenye kazi hii muhimu kwa taifa letu kulingana na matokeo
yaliyowasilishwa kitaalamu mbele yenu waandishi wa habari leo hii.Tanzania
ni nchi ya kwanza kuzima mtambo ya analojia Barani Afrika. Uamuzi wa
kufanya hivyo, na matokeo yake, umeiletea sifa kubwa nchi yetu kwa jinsi
ambavyo Tanzania ilijipanga na kutekeleza maazimio yaliyofikiwa
kimataifa kwa wakati na weledi mkubwa. Hii imeonyesha wazi jinsi
Serikali ilivyoweza kushirikiana na taasissi zake pamoja na wadau wote
katika kutimiza azma hii iliyoafikiwa kimataifa tangu 2006.Zoezi
la uzimaji mitambo kwa awamu ya kwanza iliyoanza taree 31 disemba 2013
halikuwa rahisi kama wengi wetu tunavyoweza kufikiria, kwani liligusa
nyanja nyingi zikiwemo za kijamii, kibiashara, kiufundi na Kisiasa.
Mamlaka kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano, ilibidi kuzingatia
matakwa ya nyanja zote na wadau mbalimbali bila kuathiri utoaji wa
habari nchini. Inakadiriwa kuwa mpaka kumaliza zoezi hili, mitambo ya
kurushia matangazo kwa mfumo wa analojia isiyopungua 60 itakuwa
imezimwa. Hali hii imefanya Tanzania kuwa nchi ya pekee na kuifanya nchi
yetu kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi nyingi ambazo sasa zimekuwa
zikifika kujifunza hapa nchini.
Uamuzi
wa kufanya mkutano wa nchi za SADC na ule wa nchii za Jumuiya ya Madola
kuhusu Mfumo mpya wa utangazaji wa kidijiti kwa sekta ya utangazaji
hapa nchini hivi karibuni, ni matokeo ya mafanikio makubwa tuliyo yapata
kwenye zoezi hili lililoendeshwa kitaalamu na Serekali yetu kupitia
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
2.0 UPELEKAJI WA MKONGO WA TAIFA KWENYE VITUO VYA KURUSHIA
MATANGAZO
Mamlaka
ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara na Kampuni ya Simu ya TTCL
tuko kwenye mchakato wa kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kurushia
matangazo vinafikiwa na mkongo wa Taifa (Optic fiber cable).
Madhumuni
ya jitihada hizi, ni kuona kuwa mbali na huduma ya msingi ya kurusha
matangazo ya televisheni, vituo vya utangazaji vinatoa huduma za ziada
zipatikanazo kwenye mfumo wa kidijiti. Kwa lugha ya kitaalam ni
“interactive services”. Napenda kuchukua nafasi hii kuvitaka vituo vya
utangazaji vyote nchini kuwa wabunifu na kutumia fursa zilizopo kwenye
teknolojia hii ya kidijiti ili wananchi waweze kuona tofauti kubwa kati
ya mfumo wa zamani wa analojia na huu mpya wa kidijiti.
3.0 UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA AWAMU YA PILI
Baada
ya kupokea matokeo ya tathmini Awamu ya Kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano
inajipanga kuzima mitambo kwa awamu ya pili na ya mwisho. Katika awamu
hii, inategemewa miji 12 itahusika na uzimaji wa mitambo ya analoja.
Lakini kama maafikiano yalivyofanyika awali, uzimaji utafanyika tu pale
ambapo huduma za utangazaji wa kidijiti umefika. Vigezo vyote vitano
tulivyokubaliana na wadau vitahakikishwa kuwa vinatimizwa kabla ya
kuzima mitambo hiyo.
Ni
matarajio ya Mamlaka kuwa wasimikaji wa mitambo ya kidijiti (Multiplex
Operators) wataendelea kwa kasi ufungaji wa mitambo hiyo hasa kwenye
maeneo ambayo mfumo wa analojia unatumika. Mpaka sasa miji mingine 7
inapata huduma ya matangazo ya kidijiti nayo ni Morogoro, Singida,
Tabora, Musoma, Kigoma, Bukoba na Kahama. Mchakato wa kufunga mitambo ya
kidijiti kwenye miji iliyobaki inaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa
vituo vya utangazaji vitatoa ushirikiano mkubwa kama ule tulioupata
kwenye awamu ya kwanza.
Mamlaka
imeyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti hii na
tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale yaliyo nje ya uwezo wetu
tutayafikisha mahali panapohusika kwa utekelezaji zaidi.
Mwisho,
napenda kuwafahamisha kuwa Mamlaka imependekeza rasimu ya ratiba ya
uzimaji mitambo awamu ya pili na ya mwisho itakayotangazwa na Waziri
mwenye dhamana ya sekta ya Mawasiliano hivi karibuni.
Katika
mapendekezo ya Mamlaka, tunakusudia kuanza awamu ya pili katika miji ya
Singida na Tabora mnamo mwishoni wa mwezi Machi 2014. Miji mingine
katika awamu ya pili itakuwa Musoma, Bukoba, Morogoro, Kahama, Iringa,
Songea na Lindi. Awamu ya pili inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi
Oktoba 2014.
Nia
ya Mamlaka ni kuona zoezi hili la uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa
analojia kwenda mfumo wa kidijiti linakamilka katika nchi yetu kabla ya
kufikia ukomo wa matangazo ya analojia kama ilivyoelekezwa na Shirika
la Umoja wa Mataifa linalosimamia Mawasiliano Duniani (ITU) siku ya tarehe 17 Juni 2015.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
19 February 2014
No comments:
Post a Comment