Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, February 25, 2014

WATU SABA WAFARIKI DUNIA MKOANI IRINGA

 
Watu saba wamefariki dunia katika matukio sita tofauti mkoani Iringa likiwemo la watoto wawili kufariki wakiwa wanaogelea kwenye dimbwi la maji lililopo kijiji cha Mkungugu tarafa ya Isimani.

Akizungumza  ofisini kwake kaimu kamanda wa polisi Mkoani Iringa Mratibu mwandamizi Peter Kakamba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 23 februari majira ya saa 12:30 jioni.

Kaimu Kakamba aliwataja watoto hao ni Nestory Luhala(8)  ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili pamoja na Junior Luhala(5).

Tukio lingine mwanafunzi wa miaka 14 ajulikanaye kwa jina la Iginasi Ngalembule mkazi wa Isuka  kata ya Mtitu wilayani Kilolo afariki dunia baada ya kupigwa na radi.

Kaimu Kakamba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 22 februari majira ya saa 11 kamili jioni.

Na katika tukio lingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Benny Kaguo(21) mkazi wa Viwengi afariki dunia wakati akiwa anasubiri kupatiwa matibabu katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Kaimu Kakamba alithibitisha tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 21 februari majira ya saa 2:30 usiku na kusema marehemu alijeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika baada ya kuhusishwa kwa wizi wa nyanya.

Watu waliohusika na tukio hilo la kumpiga marehemu wanatafutwa na polisi.

Aidha tukio lingine JESHI la polisi mkoani Iringa linamshikilia Yoktani Kikula(24) dereva wa Scania na mkazi wa Ipogoro kwa kosa la kusababisha kifo cha Kennedy Kisoma(8) mwanafunzi wa Idegenda.

Kaimu Kakamba alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 20 februari majira ya saa 10 kamili alasiri ambapo dereva huyo alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T.655 CKC aina ya Scania ambapo chanzo cha kifo hicho ni baada ya mwanafunzi huyo kudandia gari hilo bila dereva kufahamu na hatimaye kudondoka ghafla na kufariki papo hapo.

Mtu mmoja mwendesha pikipiki aliyefahamika kwa jina Gohan Luhwango(22) afariki dunia baada ya kugongana uso kwa uso na gari aina ya Nissan patrol.

Kaimu Kakamba alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 21 februari majira ya saa 10 kamili maeneo ya kijiji cha Boma la Ng’ombe barabara ya Kilolo-boma.

Kakamba alisema marehemu alikuwa akiendesha pikipiki aina na namba bado hazijafahamika ambapo aligongana na gari lenye namba za usajiri T.167 APH mali ya Dolphin Safari iliyokuwa ikiendeshwa na Steven Joseph(45) na kufariki papo hapo.

Mbali na matukio hayo ya vifo pia kaimu Kakamba alisema jeshi la polisi mkoani hapa linamshikilia Sigfried Mapunda(51) mkazi wa mkimbizi kwa kosa la kumgonga Rosemary Mbilinyi(42) mkazi wa Kibwabwa na kumsababishia kifo papo hapo.

Kakamba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 23 februari majira ya saa 2:25 usiku katika barabara kuu ya Iringa – Mbeya na kulitaja gari hilo ni aina ya Isuzu fuso lenye namba za usajili T.679 ABS.
 
NA DIANA BISANGAO WA MATUKIO DAIMA.COM, IRINGA
 

No comments:

Post a Comment