Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, February 15, 2014

YANGA YAFUZU HATUA YA PILI, YAICHAPA KOMOROZINE de DOMONI 5 -2, NGASA APIGA HAT-TRICK


Mrisho Ngasa akipokea zawadi ya mpira kutoka kwa mwamuzi wa mchezo wa leo kutoka Sychelles Allister Barra wa kufuatia kufunga mabao matatu (hat-trick)
Wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika timu ya Young Africans leo imeweza kufuzu raundi ya pili ya mashindano hayo kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya wenyeji timu ya Komorozine de Domoni katika mchezo uliofanyika jioni ya leo katika dimba la Uwanja wa Sheikh Said Ibrahim Mitsamihuli.
Ikicheza mbele ya Balozi wa Tanzania nchini Comoro Bw. Chabaka Kilumanga Young Africans imefanikiwa kufuzu hatua ya pili ya Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 12- 2, kufutaia ushindi wa mabao 7-0 katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es salaam huku Mrisho Ngasa akifunga "Hat-trick" katika michezo yote miwili.
Komorozine de Domoni ikicheza mbele ya Gavana wa jimbo lao la Anjuani iliuanza mchezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema ili kuwapa nguvu washangiliaji wao amabo walikuja kuipa sapoti timu hiyo.
Hamis Kiiza aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 13 ya mchezo kufuatia kuitumia vizuri krosi ya mlinzi wa kushoto Oscar Joshua aliyepanda kuongeza nguvu mashambulizi na pasi yake kumkuta Kiiza ambaye aliukwamisha mpira wavuni bila ajizi.
Dakika ya 22 ya mchezo, Mrisho Ngasa aliwainua mashabiki wa Young Africans vitini kufuatia kuifungia timu yake bao la pili kufuatia migongeo mizuri ya Haruna Niyonzima na Didier Kavumbagu.
Saimon Msuva aliipatia Young Africans bao tatu kufuatia kufanya shambulizi langoni mwa timu ya Komorozine de Domoni baada ya pasi za viungo Athuman idd, Haruna Niyonzima na Mrisho Ngasa kumkuta mfungaji ambaye hakufanya makosa.
Dakika ya 41 ya mchezo makosa ya mpira ulioptezwa na Hamis Kiziza yaliwapelekea Komorozine de Domoni kijipatia bao la kwanza baada ya mshmabuliaji wao kumtoka Oscar Joshua na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika, Komorozine de Domoni 1 - 3 Young Africans.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Young Africans iliwaingiza Frank Domayo, Hassan Dilunga na Said Bahanuzi waliochukua nafasi za Athuman Idd, Saimon Msuva na Didier Kavumbagu mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi.
Dakika ya 77 Korozine de Domoni walijipatia bao la pili kufuatia makosa ya kiungo Hassan Dilunga baada ya mpira alipoteza kunaswa na msahmbuliaji wa Komorozine na kuwazidi ujanja walinzi wa Young Africans na kuukwamisha mpira wavuni.
Mrisho Ngasa aliipatia Young Africans bao la nne dakika ya 87 ya mchezo kufuatia Said Bahanuzi kuwatoka walinzi wa Komorozine na kupiga krosi iliyomkuta Ngasa na kuukwamisha mpira wavuni kwa kifua.
Dakika ya 90 ya mchezo Mrisho Ngasa aliendelea kuwapa furaha tena washabiki wa Young Africans waliojitokeza uwanjani leo kuishangilia timu yao baada ya kuipatia timu yake bao la tano na la ushindi kwa kichwa baada ya kuitendea vyema krosi ya kiungo Haruna Niyonzima.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Komorozine de Domoni 2 - 5 Young Africans.
Mara baada ya mchezo mwamuzi wa mchezo wa leo Allister Barra alimkabidhi mpira mshambuliaji Mrisho Ngasa kufuatia kufunga mabao 3 peke yake (hat-trick) katika mchezo wa leo.
Baadhi ya watanzania walijitokeza kuishangilia timu yao ya Young Africans wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Chibaka Kilumanga  walifurahishwa na ushindi huo na kusema wamefarijika na timu yao kwa kushinda mchezo wa leo na kusema wanaitakia kila la kheri katika michezo inayofuata.
Kesho mchana Msafara wa Young Africans umealikwa chakula cha mchana nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro Bw.Ckibaka Kilumanaga  na siku ya jumatatu kikosi kitaanza safari ya kurejea nchini majira ya saa 6 mchana kwa shirika la ndege Precision Air.
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite, 3.Oscar, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Chuji/Dilunga, 7.Msuva/Domayo, 8.Niyonzima, 9.Didier/Bahanuzi, 10.Ngasa, Kiiza

No comments:

Post a Comment