skip to main |
skip to sidebar
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya
kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba
katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja
kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka
za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima,
umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa
na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako
kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili maalumu na la kihistoria.
Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini
waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya
Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze
kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la
Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana
katika historia ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi
yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika
kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa
kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo
bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja,
upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania,
licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako,
au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa.
Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini. Katiba
itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria,
utawala bora na kudhibiti maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo mwisho
kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi
kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga
Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya
Muda na mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu
tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato
unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa
maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi
wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata
nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili
Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao
kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi
201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba
za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum
la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo, kwa Katiba
zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda
Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii,
wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar
na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni
itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura.
Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara
14. Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko
muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa
nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania
kufuatia kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya
kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
2.
Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya
Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
3. Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka
utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo.
Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara
ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na
mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4. Mwaka 1992,
yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa
uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake
katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge
wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge
lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya
kutokuwa na imani.
5. Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
6. Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika
mabadiliko yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi
wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali
kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na
kufanya yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai
yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi
kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti
kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika
mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano,
imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya
Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na
viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati
ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha
mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika
mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania
kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia
riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba,
2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa
kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja
mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya
Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya
itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya
kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya
maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe
6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2
Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na
kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume,
Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili
tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili,
kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa
kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au
HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba
ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine yanayosomwa
na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma.
Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu
ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu.
Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni
yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa demokrasia
imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako
huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia
ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la
kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele
ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa
Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu
351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika,
walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na taasisi
mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa
kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko
yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni
kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa Tanzania,
lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa
wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa
la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume
imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha
Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati
tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu
za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi
kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo
mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili
mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini
mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa
sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi
wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali
zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au
kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung’unikiwa na
watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda
mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia
balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa
katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile
ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya
ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni
kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi
ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya
vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko
inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba
baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane
na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe
kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa
baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo kuhitaji
kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na
nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu
inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa
“Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika
likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha
sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa
upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa
sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana
nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi
kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili
ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu
hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume
la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano
ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika
Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano
inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa
Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala
yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji,
uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika
yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya
Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka
ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia
na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya
Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya
Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na
kuipa Serikali ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni
kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi
washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu muyaondoe
mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala
haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo
yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na
muundo wa Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali
ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika
Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni
lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika
Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua
mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo
yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali.
Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na
kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili
tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli
katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda
sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie baadhi ya dhana na
mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano,
linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge
iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita mfululizo
kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu hawana
tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na
hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande
kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na
kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe
vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha
kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko.
Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa
Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita
mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza
kuugua kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha
Ubunge kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya
mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na
haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa
kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike
ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake.
Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo.
Ni vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili
kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu
hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge.
Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo
hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha
juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania.
Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi
kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge
ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika
kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha
utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu
fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi
ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa
Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa
jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya
kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi
zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao
kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama
chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao
unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge.
Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba
wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo
hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa
wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za
karibu watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa
Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala
mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika
Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali
kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote
katika Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo
mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo
kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu
kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye
uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo
hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa
gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi
iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde
Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu
si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi
zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume
ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia
na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo
mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani
Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika wakati
ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili
tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia
Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika
kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya
Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa
rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo
mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume
katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa
mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo
tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata
kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika?
Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki
katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa
marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa
sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama
zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja
zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote
Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania
waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono
muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara
wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo
huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa
sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu mbili za
Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu
zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo
wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume
imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali
tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi
hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema
kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa
Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi
47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano
hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo
wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.
Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni
wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk.
66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni
kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7
walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni
772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa
Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo
linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu
waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo
hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya
watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia
10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya
Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa
kuhusu kufaa kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu
changamoto nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri
changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar
wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano
kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema
mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa
mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia,
wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya
kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar
kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha,
kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka
mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa
mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande
wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa
Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na
fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya
Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake,
wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili
Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la
Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge lazima zipelekwe kwenye
Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika Zanzibar. Wananchi wa
Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi
Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo Tanzania
Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji wa
mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za
Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi
ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua
ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za
sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu
utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha
Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na
kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na
Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake
yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta
ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia kukuza
maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na
kupendekeza kuwa muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua,
Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo
wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali
mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia
kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya
wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo;
na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa
kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha
amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa
changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una
changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa
na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji
Joseph Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu
alikuwa na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa
gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni
Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo
hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu
kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili
kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza
kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa shughuli za umma
baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera
zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua
mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika na
Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta
tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila
upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea
hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano. Muundo
huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision
making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa.
Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali
pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu
kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili
zisiue Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa
mlolongo huu wa changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha
kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu
bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa
changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini
zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na
Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu
zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake
na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za
Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na
Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi
yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja
yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa
kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia
mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya
Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu.
Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika hatua
nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili wa vyombo vya moto.
6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa
mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu
yafuatayo:
1. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
3. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali
kadhalika, katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015
– 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya
Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa
matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu,
naamini tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali,
napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya
kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa,
ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano
kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala
siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi
yao. La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila
kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu
inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za
Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa
kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na
Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa
Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo
ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili
mpate kujua ukweli na undani wa kila kilichoongezwa na sababu za
kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi
zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
Mambo ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara ya nje na mikopo,
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11
hadi kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea
nchini na kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za
Muungano zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na
taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba
nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha
mabadiliko hayo kufanywa.
Jambo la kwanza kuongezwa, yaani
la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika
tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika
Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo,
kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na
mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali
zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya
Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee
Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya
10 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na
mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo
hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa
Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli,
Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
Tarehe 22
Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi
Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi
asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo
ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa
jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika
Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la
Mitihani la Taifa mwaka 1973.
Mwaka 1984 yalipofanyika
mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya Mambo ya
Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika
Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo
yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17,
Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa
la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama
vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa
Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini
kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na
sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na
mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi
yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa
Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi.
Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni
rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya
siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa
Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo
katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo
muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo
maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za
biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na imethibitika kuwa
Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa ya mchakato huu
sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo tutakayokubaliana kutoka
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na
gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana
tangu wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais
Shein msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka
kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha
Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato
huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka
ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa
kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya “subira yavuta
heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali tunaweza
kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku
hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi.
Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni
suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo
karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi,
pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar
iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na
kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya
kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi
za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna
mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi
kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa
nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha
kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache
kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo
Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa
ufumbuzi tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano
wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya
yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu
inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar
“uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au
taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya
mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya
Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila
ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu
yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo
kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba
ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe
kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande
zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu
mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana budi upewe
nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo yote
sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye
Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu
changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu
na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa
mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa
haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama.
Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani
ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa
washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo
ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na
kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa
shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika wa
fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake
chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi
washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za
Serikali ya Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa
sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo
ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo
wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali
hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au
kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi kwa
Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa
kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini,
kwa sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa
Serikali hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake
hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo
haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha
misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au
chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni
wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya
Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua
hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa
iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa
kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii
ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya
tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa
tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya
kutegemewa na nchi washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate
mfumo huo linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa
Serikali mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa
Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo
ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni
mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na
kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa
hisia za utaifa (nationalistic sentiments) wa zamani kwa nchi
washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya, kwa sababu
ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano,
bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza kupata
ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika
mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi
hayakwami kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa
zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano
utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza
kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio
kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu walioishi pamoja
kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani
Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa
sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa
wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa
ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika, watu hao
watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa
kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili.
Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi
rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki
kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara moja watajikuta maadui.
Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa
kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora
waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma
kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume
imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu
wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar
mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa
Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii
yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza
baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na
kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne,
ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu
utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu,
hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi
ulio sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu
wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo
Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa kweli,
unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi
waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao.
Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta
tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi
kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle
mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini
aliniuliza: “Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza
ya tatu? Si matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo
Serikali tatu si kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila
kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi
mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda,
nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia
Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza,
jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi
yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi
mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito
wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu
sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni
muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu
na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana
kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu
ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache, mtakuwa
na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa
maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa.
Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga
Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake
vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba
itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua
kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa
Baraza la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi
yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa
ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu
sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya
kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka
yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua mliyofikia.
Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo hamna budi
kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa
kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao kwenu.
Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa
kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na
mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya wananchi
wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea
kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia
kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya
Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena katika awamu hii.
Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na Wajumbe wao au na hata
chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa nchi yao. Tutoe hoja
badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna haja ya
kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika kujieleza. Hakuna haja ya
kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au hata kugombana. Ni utovu
wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa
Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na
kujali maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi
yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania
Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo
kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama
vyao au makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta
mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na
kuunganisha mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa
pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa
tayari kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu
mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu
wengine hata kama ni watu usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani.
Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya
hivyo hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya
kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute
namna ya kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute
kushindana, hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi.
Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao.
Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa
kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano,
mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano.
Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za
kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara zaidi
katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize
kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini
tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba
uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya
uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua.
Baada ya kusema maneno yangu mengi hayo,
nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya
kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila la heri na
mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment