Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, March 21, 2014

Jinsi Instagram inavyoyaua matangazo ya radio/TV yanayohusu show/events



Kadri miaka inavyozidi kwenda na teknolojia ya mawasiliano ikiendelea kukua, kuna mambo mengi yamerahisishwa, yamepungua ama yameondolewa kabisa. Kumbuka enzi zile msanii anapotaka kusambaza wimbo wake kwenye redio zote nchini.. Kufanikisha hilo alitakiwa kuzituma kwa njia ya basi, ndege, posta ama kumpa mtu CD atakayeipeleka mpaka pale anapotaka ifike.


Taratibu baada ya watu wengi kuwa na e-mail zao, wasanii wengi wakaanza kuzituma nyimbo zao kwa njia hiyo na kurahisisha mambo. Haikuishia hapo, ongezeko la blogs za burudani likafanya upatikanaji wa nyimbo uwe rahisi zaidi. Bongo5 ikiupata wimbo mpya na kuuweka hulkshare ama soundcloud, kila mtu duniani anaweza kuupata muda wowote anaoutaka.

Huo ni mfano mmoja tu wa jinsi teknolojia ya mawasiliano ilivyoleta mapinduzi.

Kwa leo sitagusia mapinduzi yaliyoletwa na Facebook, Whatsapp na mitandao mingine lakini ningependa kuizungumzia Instagram inayohusika zaidi kwenye makala hii.
Instagram inaendelea kukua kwa kasi na nimewahi kuizungumzia jinsi inavyokiki kwa Bongo. Kwa wasanii na wafanyabiashara kwenye burudani, Instagram kwa sasa imekuwa chombo muhimu kwa kufikisha ujumbe kwa mashabiki au wanunuzi. Kabla ya Instagram na mitandao mingine ya kijamii, kama msanii ana show, ilikuwa ni lazima alipie matangazo redioni kuipromote, kusambaza posters mitaani au kupiga PA. 


Miaka ya hivi karibuni, matangazo ya aina hiyo kwenye redio au TV yamezidi kupungua hasa kwakuwa yana gharama kubwa. Sababu kubwa nyingine ya kupungua, ni kwamba Instagram imeonekana kuwa chombo ‘effective’, kisicho na gharama na kinachowafikia watu wengi na wanaohusika haswaa na mambo hayo.
Utafiti wa haraka haraka unaonesha kuwa watumiaji wengi wa Instagram ni vijana wahudhuriaji wakubwa wa club, show na matamasha ya kulipia. Watu wengi wanaoenda Maisha Club, Bilicanas na kwenye sehemu zingine za burudani za usiku, humiliki smartphones zenye application hiyo. Hiyo ina maana kuwa, banner au tangazo moja la show/event likiwekwa kwenye Instagram na watu 10 wenye followers wengi, ujumbe huwafikia idadi kubwa tena iliyonuiwa (targeted audience) kuliko redioni.
Pamoja na ukweli kwamba matangazo ya redio huwafikia watu wengi zaidi, ukweli ni kwamba matangazo ya show/events husikika kwa watu wasionuiwa kwakuwa wapenzi wa maisha ya usiku (night life) si wasikilizaji wazuri wa redio labda kama wakiwa kwenye magari. Lakini watu hao huzishika simu zao na kutembelea kwenye mitandao ya kijamii karibu muda wote.
Hicho ndio wasanii na waandaji wa show siku hizi wamekuwa wakifanya na Instagram ndio imekuwa sehemu mahsusi kwa hilo. Ndio maana siku hizi ukiingia Instagram utakutana na picha nyingi zinazotangaza ujio wa single mpya, msanii kuwa na show sehemu, uzinduzi wa kitu fulani, ujio wa bidhaa mpya kwa wenye maduka na mambo mengine. Wasanii wengi kwa sasa wamekuwa wakitumia tu Instagram kutangaza events zao na hufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Siri ni kuwa, ujumbe huo huwafikia wahusika, kuliko kama wangetumia redio peke yake.
Kinachofanyika sasa ni kwamba, msanii akiwa na show yake, huwaomba washkaji zake au wasanii wenzie kumsaidia kuweka poster yake kwenye kurasa zao. Poster hiyo ikiwekwa na mastaa 10 ambao kwa wastani kila mtu ana followers, 30,000.. unaweza kupata picha ya jinsi ujumbe huo unavyoweza kuwafikia watu wengi na kwa njia rahisi na ya uhakika.
Poster hiyo inaweza kuwa ‘effective’ kuliko hata tangazo la redio. Hii ni kwasababu mtu anaweza kusikia tangazo la redio akiwa na shughuli nyingine na hivyo kushindwa kupata details zote za mahali, kiingilio ama siku ya tukio.
Lakini kwa mtu anayeona poster kwenye Instagram, ni rahisi kuchukua muda mzuri kufahamu kila kitu kwa ufasaha.
Hii ina maana kuwa, kuwa na followers wengi kwenye Instagram kwa msanii ama muandaji wa show, ni sawa na kuwa na mtaji muhimu anaohitaji kuuheshimu. Kwa Diamond ambaye sasa ana takriban followers 90,000, ni rahisi mno kuandaa kitu kitakachofanikiwa kwa kutumia promo ya Instagram na mitandao mingine ya kijamii.
Hivyo, Instagram ni zaidi ya kupost ‘selfies’. Instagram ni hazina.



No comments:

Post a Comment