HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba,
limepitisha rasimu ya Kanuni zitakazotumika kuongoza majadiliano, pamoja
na vifungu ambavyo havikutaja aina ya upigaji kura kama utakuwa wa wazi
au wa siri. Hata hivyo, wakati Bunge likipitisha azimio hilo, baadhi ya
wajumbe wamelaani kitendo cha Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu,
Pandu Ameir Kificho, kuridhia kupitishwa kwa ‘kanuni nusu’ za Bunge kwa
maelezo kuwa jambo hilo halitaleta muafaka.
Wajumbe hao pia wameonya kuwa Bunge
Maalumu la Katiba, linaweza kushindwa kupata muafaka wa njia ya kufanya
uamuzi iwapo wajumbe ndani ya Bunge hilo watang’ang’ania ushabiki na
itikadi za vyama vyao.
Azimio la Kutunga na Kupitishwa kwa
Kanuni hizo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa
Costa Mahalu ambaye alitaka kanuni zipitishwe pamoja na aina ya upigaji
kura kwa ajili ya kupata uamuzi wa Bunge Maalumu unaendelea
kushughulikiwa.
“Suala la upigaji kura, litawekwa katika
kanuni husika baada ya kuamuliwa kama ambavyo Bunge hili maalum litaona
inafaa,” alisema Profesa Mahalu akizungumzia vifungu vya 37 na 38
vinavyoelezea namna ya upigaji kura ambapo kanuni hizo zimeelezea uamuzi
utakaopitishwa kwa upigaji wa kura.
Wakichangia wakati wa kupitishwa kwa
kanuni hizo, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Kanuni nzuri zinakidhi
mahitaji ya kuendesha vizuri Bunge la Katiba. Kanuni zimetuhakikishia
haki na kinga za kila mjumbe na kutakuwa na uhuru bila kushurutishwa au
kupokea maelekezo kutoka kwa yeyote au chombo chochote, naomba
tuzipitishe.”
Naye James Mbatia aliomba vifungu vya 37
na 38 ambavyo havijakamilishwa vichukue muda mfupi vikamilishwe. Kwa
upande wa Idrisa Kitwana Mustafa alisema:
“Mshikamano wetu ndiyo utakaowapa moyo
wananchi walio nje ya Bunge hili. Tukubali kuwa hakuna kazi ya mwanadamu
itakayoridhisha kila mtu na tuchukulie upungufu uliojitokeza kama ni
mambo madogo kwani tuna kazi kubwa mbele yetu”. Panya Ali Abdallah
alisema anaamini tunu ya hekima na busara itatumika katika kupata
Katiba. Shehe Mussa Kundecha alisema:
“Hakuna kazi ya mwanadamu ikakosa kasoro…ni busara kuona watu wakikubaliana kwa yale waliyotofautiana , tuliombee Bunge hili”.
Kwa upande wa Freeman Mbowe wakati anaunga mkono azimio hilo, aliwataka wajumbe washirikiane, kuheshimiana na kuvumiliana.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alilaani
hatua ya Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho,
kukubali kanuni kupitishwa ‘nusu’ kwa sababu ya kuzidiwa nguvu na vyama
vya siasa ambavyo vimesimamia itikadi zao na vinatoa vitisho kwa wabunge
wake wakubaliane na misimamo ya vyama.
“Hii Katiba tunayoenda kuitunga hapa ni
Katiba ya vyama vya siasa na sio Katiba ya wananchi, maana vyama vya
siasa vyote vina misimamo kwenye kuandika Katiba hiyo na ndicho
kinafanya tushindwe hadi kuafikiana ndani ya Bunge hili,” alisema.
Mbunge huyo ambaye jana alisimama
ukumbini kutaka kuzungumza lakini hakupewa nafasi, alidai iwapo jambo
hilo litakwama hapo baadaye, Kificho ndiye wa kulaumiwa maana wiki ijayo
ni wiki ya kufanya uamuzi lakini Kanuni zimekaa kimya.
Alisema kwa mara ya kwanza Tanzania
itapata Katiba ya vitisho kutokana na vyama vikubwa vya CCM, Chadema na
CUF kuwalazimisha wabunge wake kuwa na msimamo katika suala ambalo
linahusu masuala ya wananchi na sio ya vyama hivyo.
“Watanzania wapo wengi hawana vyama,
lakini hivi vyama vya siasa vimeng’ang’ana kuwatisha wajumbe wake
wasiende kinyume na misimamo ya vyama hivyo, hii sio haki hata kidogo,
tunachoandika hapa ni Katiba ya wananchi sio ya vyama,” alisema mbunge
huyo.
Alionya kuwa wabunge wengi kwenye vyama
vya siasa ni waoga hasa wa viti maalumu, maana wanaamini kuwa wakienda
nje ya misimamo ya vyama vyao, watafukuzwa na hawatapata ubunge tofauti
na wabunge wa majimbo.
Mbunge wa Muhambwe Felix Mkosamali,
alisema hata wajumbe ambao wamepitisha Kanuni hizo watajilaumu kwa vile
vikao vya Bunge haviwezi kuanza bila kuafikiana namna ya kufanya uamuzi.
Mkosamali ambaye awali alimlalamikia
Kificho kwa kutompa nafasi ya kuzungumza, licha ya kusimama mara nyingi,
badala yake Mwenyekiti huyo wa muda alikuwa anaruhusu wajumbe
aliowataka.
“Toka nimefika hapa sijapewa nafasi ya
kuzungumza, nimesimama mara kwa mara; lakini Mwenyekiti haniruhusu kwa
vile tu anafahamu msimamo wangu ni kupinga kanuni hizi kupitishwa nusu,”
alisema Mkosamali.
Alipoulizwa iweje apinge suala hilo
wakati Mwenyekiti wake wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisimama
kuunga mkono na kuwasihi wajumbe wote kuunga mkono suala hilo, alisema
Mbatia ana uamuzi wake katika Bunge la Katiba.
“Kwa maoni yangu, Mbatia amekosea kuunga
mkono suala hilo, huo ni mtazamo wangu maana hapa hakuna mbunge wa
chama bali sote sisi ni wajumbe, hakuna mnadhimu wa chama hapa,” alisema
Mkosamali.
Alisema katika Bunge Maalumu la Katiba,
mambo yote yanahitaji maridhiano hivyo haipendezi Mwenyekiti kupendelea
baadhi ya watu. Alisema anamsubiri Mwenyekiti atakayechaguliwa ili
awasilishe maoni yake.
Mchungaji Christopher Mtikila kwa upande
wake alisema alipinga kupitishwa kwa azimio hilo la kuazimia Kanuni za
Bunge Maalumu kwa vile limepitishwa kwa hila na akashangaa wajumbe
wengine kutoka kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunga
mkono kanuni hizo.
Mtikila alisema suala la kanuni hizo
kutokuwa na namna ya kupiga kura, linaonesha dhahiri kuwa wajumbe hawana
nia ya dhati ya kutunga Katiba mpya kwa vile suala hilo litarudishwa
kwa wajumbe hao lipate uamuzi.
Alisema kuliahirisha ni kutoa fursa kwa
baadhi ya watu kuwarubuni baadhi ya wajumbe ili waweze kubadilisha
misimamo yao na wanapoenda kupiga kuwa wapigie kundi ambalo
linang’ang’ania kura ya wazi.
“Ndio maana wameliweka kiporo suala hili
wanataka tukirudi hapa tuwe tumepowa na watunywe vizuri kama uji wa
ulevi,” alisema Mtikila.
Mbatia kwa upande wake alisema wiki tatu
zilikuwa ngumu kwa wajumbe, lakini akasema kwenye Katiba ili jambo
lipite ni lazima lipate maridhiano hivyo kitendo cha kupitisha kanuni
hizo kunatoa fursa ya mambo mengine kuendelea na baadaye warudi kufanya
uamuzi.
“Dola linaundwa kwa njia ya maridhiano
na ndio hatua tuliyofikia sasa, wahenga wanatuasa pambana wakati
mnazungumza, kisheria kanuni hizi ziko sahihi,” alisema Mbatia.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment