Nguvu
ya madaraka na uwezo wa madaraka yenyewe yamefanya watu wengi kufanya
vitu vingi ili angalau aonekane anastahili kuwepo kwenye hayo madaraka.
Wiki hii sizungumzii viongozi wa serikali, vyama na mashirika bali ni
katika maisha ya kawaida ambayo sisi wengine tupo huko kwa wingi wetu.
Kwa tafsiri rahisi ni uwezo anaopewa mtu juu ya jambo fulani yeye
kulisimamia au kusimamia kitengo fulani cha watu fulani ndipo tunaposema
mtu huyu ana madaraka ya kitu fulani.
Ukifuatilia
kwa makini uroho wa madaraka hauko huko juu tu, bali hata huku mtaani
mambo yanaendelea hivyo hivyo. Sikujua kuna watu wanatamani wawe ndo
wenyeviti wa harusi, wasipowekwa utalijua kasheshe lake, inabidi waanze
kwa kusema unajua huyu mwenyekiti hana uzoefu kabisa na nina wasiwasi
kama ana hekima. Nikajaribu kuwaza je tatizo ni mwenyekiti au tatizo ni
wewe? Upo kwenye kamati kwa ajili ya kusaidiana na huyo mwenyekiti ili
mfanikishe hiyo harusi. Kwani kwenye harusi zaidi ya michango na kujua
harusi itafanyikia wapi, je wewe utakuja na ubunifu gani mpya watu
wasioujua? Je kwanini huwezi kuthamini na kuheshimu watu wengine wakiwa
juu yako? Inawezekana watu hawakuamini au hauna mvuto wa kuwaongoza
katika hiyo kamati, unachotakiwa ni kujishusha na kuruhusu wakati
mwingine uongozwe ili uweze kujifunza.
Je
una ajenda gani ya siri kwenye hayo madaraka unayoyataka? Unajua ni
rahisi kuwasema viongozi wa juu kuwaona kuwa ni waroho. Utagundua kila
mtu ni mroho wa madaraka ila kiwango cha uroho kimetofautiana. Labda
ukichukua uenyekiti wa maandalizi ya harusi, itabidi uipigie chepuo
biashara yako au kamisheni ya mapambo , ukumbi, vinywaji na hata usafiri
na video shooting? Je agenda yako ni nini?
Agenda
yako ndio itakufanya ung’ang’anie uongozi au usiung’ang’anie uongozi.
Kama una mpango wa kusaidia kwa roho safi ni vizuri zaidi. Ila kama ni
kwa ajili ya umaarufu na kuleta mivutano isiyo ya kawaida, ninakushauri
kaa pembeni. Kama una mpango wa kusaidia hata usipokuwa mwenyekiti au
ngazi yeyote , bado unaweza kusaidia na mchango wako utafaa sana.
Jifunze kujitolea hata kama hujapewa cheo.
Kumbuka,
mwoaji na mwolewaji ndio wanajua wanachokitaka , hivyo kila jambo
lazima liende kulingana na hao wanaofanya mkae kikao. Ingawa kuna mambo
yamekuwa yakiendelea ambapo watu wengine ndo wanaosema harusi iweje, ni
kana kwamba vitu ambavyo havikufanyika katika maisha yao wanataka
vifanyike kwenye maisha ya wengine. Kama ya kwako ulidunda,
usilazimishie kwa wengine, kila mtu ana kitu anachokipenda kitokee
kwenye maisha yake hivyo waruhusu kama inawezekana wao ndo waamue kitu
wanachokihitaji. Wewe ni kuwasaidia wafike pale wanapotakiwa kufika,
sizungumzii utamaduni ninazungumzia kwamba mwisho wa siku kumbukumbu ni
kwa ajili ya hao wawili nyinyi ni mashahidi tu.
Ni mwendelezo wa kuelewa kabla ya kufanya jambo au kutekeleza jambo.
No comments:
Post a Comment