RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Jakaya Mrisho Kikwete ameipa klabu ya Simba Sh 30 milioni kwa ajili ya
kukomboa hati yao ya kiwanja cha Bunju B, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
aliwaambia wanachama wa klabu hiyo jana Jumapili katika mkutano wa
wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar es
Salaam.
Rage alisema kwamba Rais Kikwete ametoa
fedha hizo baada ya kufurahishwa na umoja ulionyeshwa na baadhi ya
wanachama wa Simba waliojitolea kwenda katika uwanja huo kwa siku za
karibuni na kufyeka majani na kuonyesha kuwa wanauhitaji.
Rage alisema alikutana na Rais Kikwete
saa 2 asubuhi jana Jumapili kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Simba
na kumtakia heri katika mkutano huo huku pia akitoa hundi ya Sh 30
milioni kwa ajili ya uwanja huo.
“Asubuhi leo saa 2 nilipata bahati ya
kukutana na Rais Kikwete na kututakia heri katika mkutano wetu na kama
unavyojua kulikuwa na matatizo ya kupata hati ya ardhi kule Bunju,
tulikuwa tunadaiwa Sh 85 milioni, tulitoa milioni 50 hivyo nikamuomba
Rais aingilie kati jambo hili ili kuweza kupata hati mapema na kuanza
ujenzi.”
“Rais akanikabidhi hundi ya milioni 30
kama mchango wake kwetu, amedhihirisha ni mwanamichezo na mpenzi wa timu
zote, kutokana na jambo hilo naamini mambo yatakwenda vizuri na zile
siku 100 alizotoa katibu wa Simba kuwa baadhi ya vitu vitakuwa
vimekamilika basi vitakamilika kweli maana hadi kufikia siku hizo
tutakuwa hata na sehemu ya kufanyia mazoezi timu yetu,” alisema Rage.
Aliongeza: “Kikubwa alichofurahishwa ni
juhudi za wanachama kwenda kule na kuonyesha uhitaji wa uwanja na ndio
maana akaamua kutoa fedha hizo ili kuhakikisha tunapata hati ya ardhi na
kuanza ujenzi mara moja.”
SOURCE: MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment