Serikali imekunjua makucha yake katika kudhibiti ada zinazotozwa katika vyombo vya utoaji elimu chini.
Jana,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alizindua
rasmi mfumo mpya wa ulipaji ada katika vyuo vya elimu ya juu, huku
akisema utasaidia kudhibiti viwango vya ada vinavyotozwa kwa wanafunzi.
Akizindua
mfumo huo jijini Dar es Salaam, Dk. Kawambwa alisema Serikali
imeanzisha mfumo huo unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu katika vyuo
vyote, kwa lengo la kudhibiti ada kulingana na fani zinazotolewa.
"Sasa
natarajia nitapata usingizi wa kueleweka maana kelele za viwango vya ada
zilikuwa ni kubwa, kila chuo kilikuwa na ada yake. Niliulizwa vigezo
vinavyotumika kupanga sikuwa na jibu, lakini sasa nitakuwa na majibu
tena yanayoeleweka," alisema.
Suala la
viwango vya ada katika shule na vyuo binafsi liliwahi kuzungumziwa kwa
kina siku za nyuma, huku Rais Jakaya Kikwete na Waziri Kawambwa
wakinukuliwa kwa nyakati tofauti kutaka taasisi za elimu kupunguza
viwango vya elimu. Aprili 2013 akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama
cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyokuwa vya Serikali
(Tamongsco) uliofanyika mkoani Mbeya, Rais Kikwete alisema: "Elimu ni
huduma muhimu na haki kwa mtoto. Siyo vyema kugeuzwa kuwa biashara ya
kuleta faida kubwa.''
Aliongeza
kuwa Serikali ilikuwa katika mchakato wa kutathmini ada zinazotozwa
vyuoni na sekondari ili kupendekeza viwango halisi vinavyopaswa kutozwa.
Kwa sasa
udadisi wa gazeti hili umebaini kuwa wanafunzi walioanza masomo katika
mwaka wa fedha 2013/2014 wanatozwa ada kuanzia Sh360,000 kwa mwaka hadi
Sh9,900,000.
Kwa
mujibu wa Dk. Kawambwa, mfumo huu ambao baadaye utaendelea hadi shule za
sekondari na msingi, umepatikana kupitia kikosi kazi cha wataalamu
ambacho pamoja na majukumu mengine kilipewa kazi ya kutathmini gharama.
Dk.
Kawambwa alisema moja ya faida ya utaratibu huo mpya ni kudhibiti
taasisi zinazotoza ada kubwa kwa sababu za binafsi ikiwamo biashara.
Mkuu wa
Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Makumira cha Dar es Salaam (Tudarco),
Profesa Uswege Minga alisema endapo gharama hizo zitakuwa sawa, vyuo
binafsi vitaathirika kwa sababu ni gharama kubwa kuendesha chuo kikuu.
No comments:
Post a Comment