Dar
es Salaam. Hali ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya
mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya
mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika tuhuma hizo, Wenje
alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na
Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya vyakula, maji na
vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa serikali mbili.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika
mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka
kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli
tupu.
Hoja ilipoanzia
Wenje, ambaye pia ni mbunge wa
Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani “walilia”
sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha
Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe
wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi
hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa
kama mganga wa jadi.
Ingawa hakumtaja jina, Wenje
alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru
aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.
Kuhusu rushwa, Wenje
alisema:“…Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa
Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika
usiku. Hii haikubaliki.”
Baada ya kauli hiyo ya Wenje,
Profesa Maghembe alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo
Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa Maghembe alikiri
kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa
ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna kundi lipo hapa ambalo
linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula
wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa
anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.
“Kwa sababu hiyo ninaomba kiti
chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje
aniombe radhi,” alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira,
huku kukiwa na sauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.
Makamu mwenyekiti pia alifanya
jitihada za kuwataka wajumbe kuwa wavumilivu, huku akitoa nafasi kwa
Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza kwamba ni tuhuma nzito.
Kawambwa alisema: “Ni kweli
nilikutana nao; ni wajumbe ambao wanatoka kwenye taasisi zinazojihusisha
na masuala ya elimu, lakini mbona wameshafanya mikutano yao mingine
mingi ambayo mimi hawakuniita. Kama mtu akiwa hana hoja bora akae
chini.”
Makamu Mwenyekiti alimtaka
Wenje aombe radhi kutokana na kauli yake, lakini katika hali ya
kushangaza mjumbe huyo alisisitiza kwamba Profesa Maghembe na Dk.
Kawambwa wamekiri.
“Maghembe amekiri aliwaita
wafugaji na wavuvi ndiyo waliokula chakula cha rushwa, pia wapo wengine
walienda kwa Waziri Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi mama mmoja siwezi
kumtaja jina hapa alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa jina lake
mwenyekiti baadaye. Aliambiwa kwamba anatoa siri… hoja iliyojadiliwa
huko ilikuwa ni kwamba msimamo ni wa serikali mbili… rushwa ya chakula,
maji na bahasha walipewa,” alisema Wenje na kusababisha kulipuka kwa
kelele zaidi.
Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.
Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.
Baada ya Wenje kukaa, baadhi
ya wajumbe wa kundi la 201 walichachamaa wakitaka kutetea hadhi yao,
akiwamo mjumbe kutoka kundi la wafugaji, Esther Juma aliyesema
hawatendewi haki kama kundi kusema kwamba walihongwa.
Alisema yeye ana ng’ombe 3,000
na asingeweza kwenda kupokea rushwa ya chakula na kumtaka mbunge huyo
kuwaomba radhi la sivyo asingetoka mlangoni.
Wakati mjadala huo ukiendelea,
mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa ametoka kwa udhuru,
alirejea kimya kimya, na kumtaka Wenje kueleza iwapo anadhani kauli yake
haikuwaudhi baadhi ya wajumbe.
Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta
kutangaza kuwa anapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za
Bunge na uamuzi utakaotolewa atautangaza bungeni.
No comments:
Post a Comment