Uamuzi huo umetolewa na Hakim Ame Msaraka Pinja baada ya kukamilika kusikilizwa kesi hiyo na washitakiwa kuonekana hawana hatia katika mashitaka yaliokuwa yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, mwezi Mei mwaka jana.
Hakimu Pinja amesema kwa kuzingatia mashahidi wanne upande wa mashitaka pamoja na washitakiwa wenyewe waliithibitishia mahakama kwamba katika mkusanyiko wao hawakuwa wakizungumzia mambo ya dini isipokuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema kwa msingi huo washitakiwa hawakuhitaji kuwa na kibali chochote cha kisheria kabla ya kuandaa mkusanyiko huo kwa vile walikuwa wakizungumzia mambo ya Muungano na kwa msingi huo hakuna shitaka linalowatia hatiani na mahakama imetupilia mbali dai hilo.
Amesema baada ya mahakama kupitia jalada la kesi hiyo, imeonekana washitakiwa hawana hatia, “ninawaachia huru kwa sababu kosa waliloshitakiwa halikuhitaji kibali cha Mufti kabla ya kuandaa mkusanyiko huo,” alisema Hakimu Pinja.
Hata hivyo Hakimu huyo alisema upande wa mashitaka wa Serikali kama haujaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo unaweza kukata rufaa mahakama ya mkoa ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa uamuzi huo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Farid Hadiy Ahmed Mussa Juma Issa, Haji Sadif Haji, Suleima Juma Suleiman, Fikirini Mjawaliwa Fikirini na Abdallah Said Ali.
Washitakiwa walifunguliwa mashitaka kwa kufanya mihadhara ya Kiislam bila kibali cha Mufti kinyume cha kifungu cha 6(1)(2) cha kanuni za kuidhinisha na kuratibu mihadhara zinazotengenezwa chini ya kifungu 15(1) ya sheria Namba 9 ya mwaka 2001, kifungu cha 10(1)© na kifungu cha 14(2) ya sheria namba 9 ya mwaka 2001.
Ilidawa bila ya halali, Mei 26 mwaka jana majira ya saa 3:30 huko katika viwanja vya Lumumba wilaya ya Mjini Unguja, washitakaiwa walifanya mihadhara ya Kiislam bila ya kuomba kibali cha Mufti wa Zanzibar.