Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, April 23, 2014

AJALI YAUA MAHABUSU WANNE NA ASKARI


Mahabusu  wanne na askari Magereza, Sajenti Peter Mabuma, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongana na lori na kupinduka katika Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Wakati mahabusu na askari hao wakikumbwa na masaibu hayo, idadi ya abiria waliokufa kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya Luhuye, iliyotokea juzi, katika Kijiji cha Yitwimila, Wilaya ya Busega, mkoani  Simiyu, imeongezeka kutoka 12 hadi 17 baada ya majeruhi watano kufariki asubuhi katika hospitali ya Rufaa Bugando, mkoani Mwanza.

Mahabusu waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Juma Mohamed (19), Faraja Msahamu (40), Alex Athumani (23) na Hamis Juma (38).

Askari Magereza aliyefariki dunia alikuwa akiwasindikiza mahabusu hao kutoka katika Mahakama ya Mwanzo Kimanzichana, kuwapeleka katika gereza la Keko, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ulrichi Matei, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana, majira ya saa 6.00 mchana.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari lililokuwa limewabeba mahabusu hao, ambalo ni mali ya Jeshi la Magereza, lenye namba za usajili MT 0038, kuligonga lori hilo na kupinduka. 

Gari lililowabeba mahabusu lilikuwa likiendeshwa na Koplo Zawadi Makupa (41). Lilikuwa likitokea katika Mahakama ya Kimanzichana.

Kamanda Matei alisema lori hilo lenye namba za usajili T446 CJS lilikumbwa na mkasa huo wakati likiwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara katika Kijiji cha Kinene Mwalusembe, wilayani humo.


 
Alisema mahabusu wote pamoja na askari huyo walifariki dunia katika eneo la tukio na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Francis Mwanisi, alithibitisha maiti kuhifadhiwa katika hospitali hiyo na kwamba, hali ya askari aliyejeruhiwa katika ajali hiyo ni mbaya.

Alisema askari huyo amepata majeraha makubwa kichwani na kwenye mikono yote miwili na kwamba, kwa hali hiyo wamepanga kumhamishia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.

WALIOKUFA KATIKA AJALI SIMIYU WAFIKIA 17
Idadi ya abiria waliokufa kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya Luhuye katika Wilaya ya Busega, mkoani  Simiyu juzi imeongezeka kutoka 12 hadi 17.

Baadhi ya marehemu, akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Waadiventista Wasabato (SDA) Wilaya ya Kahama, mkoanim Shinyanga, wametambuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema wawili kati yao, walifariki  juzi jioni wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando.

Hata hivyo, Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linamshikilia mmiliki wa basi hilo, Masalu Jackson (37)mkazi wa eneo la Majengo mapya, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara,  kwa ajili ya upelelezi wa kipolisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, baadhi ya maiti na majeruhi bado hawajatambuliwa hadi kufikia jana jioni.

Aliwataja maiti waliotambuliwa kuwa ni Mchungaji huyo wa SDA, Thomas Mwita (40), naAfisa Elimu wa Shule Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mkoa wa Shinyanga, Wangwe Maurice ( 30), ambao walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu.

Aliwataja wengine,  ambao pia walikuwa  wakitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu  kuwa ni Mahemba Chacha (42), mkazi  wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, Rahma  Kibera (32) mkazi wa Bugalika, jijini Mwanza, Alex  Masatu (42).

Ingawa hakutaja majina, Kamanda Mkumbo alisema majeruhi tisa waliokuwa   wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Magu wametambuliwa na kwamba, wawili kati yao,  hali zao ni mbaya.

“Majeruhi 33 waliofikishwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya matibabu, bado  wamelazwa. Wengine wawili, Esther Moris (18) mkazi wa Sirari, wilayani Tarime, mkoani Mara na Rose Wilson (21) mkazi wa Igoma, jijini Mwanza walifariki jana jioni  baada ya kuwa nimetoa taarifa za awali kwa vyombo vya habari,” alisema.

Aliwataja wengine waliokufa jana wakati wakitibiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando  kuwa ni Sheta Msongoma (58), mkazi wa Nassa, Jimbo la Busega, mkoani Simiyu na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Baraka Alex.

“Tusaidiane kutoa wito kwa watu wa mbali wajitokeze kwa wingi katika hospitali hizi mbili; Magu na Bugando ili wawatambue ndugu zao,”  alisema Kamanda Mkumbo.

KIKWETE ATUMA RAMBIRAMBI
Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, kufuatia vifo vya watu 17 waliopoteza maisha yao katika ajali ya basi hilo.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa ajali za barabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa imetokea katika kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba kabla ya kupinduka.”

“Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.

Naungana nao katika kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke peponi roho za marehemu, alisema Rais Kikwete.”

Pia Rais Kikwete ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Imeandikwa na Yasmine Protace (Mkuranga) na Juma Ng’oko na Berensi Alikadi (Simiyu).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment