Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais Jakaya
Kikwete ameteua mabalozi wapya watatu kujaza nafasi zilizoachwa wazi na
mabalozi waliostaafu kwa mujibu wa sheria na mwingine kushika Idara ya
Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule ilisema Rais Kikwete
amemteua Dora Msechu kuwa Balozi wa Tanzania Sweden kuchukua nafasi ya
Balozi Mohamed Mzale ambaye amestaafu.
Hadi uteuzi huo, Balozi Msechu alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika wizara hiyo.
Pia amemteua Luteni Jenerali Wynjones Kisamba kuwa
Balozi wa Tanzania Urusi. Kabla ya uteuzi huo, Jenerali Kisamba
anayekwenda kuchukua nafasi ya Balozi Jaka Mwambi, alikuwa Mkuu wa
Utendaji Kivita na Mafunzo, Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania.
Rais pia amemteua Joseph Edward Sokoine kuwa
Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi huo, Sokoine
alikuwa Ofisa Mambo ya Nje Mkuu na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa
Tanzania, Canada.CHANZO MWANAINCHI


No comments:
Post a Comment