Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, April 8, 2014

Tamko la awali la CHADEMA kupinga uchaguzi mdogo wa Chalinze


CHADEMA logo
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinatoa tamko la awali kwa umma kuhusu ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia uchaguzi, zilizofanyika kwenye mchakato wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Chalinze, ambao umehitimishwa Aprili 6, mwaka huu, kwa wapiga kura wa jimbo hili kupiga kura;

Ukiukwaji huo ni kama ifuatavyo;

  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza wapiga kura wapya kinyume cha sheria
Kinyume kabisa na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 15(5), kinachosema; 

“Kwa madhumuni ya kifungu hiki, Tume itapitia upya daftari la kudumu la taifa la wapiga kura mara mbili kati ya kipindi kinachoanza mara baada ya uchaguzi mkuu na tarehe inayofuatia siku ya uteuzi,”

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekiuka kifungu hiki cha sheria kwa kufanya kile wanachoita wao ni ‘uhakiki wa mwaka 2014’ wa daftari ambao wanadai lengo lake lilikuwa ni kupunguza idadi ya wapiga kura waliokufa au kuhama au kuandikishwa mara mbili, lakini badala ya wapiga kura kupungua, uhakiki huo uliofanywa na tume bila kushirikisha wala kuwataarifu wananchi wa Jimbo la Chalinze, umeongeza idadi ya wapiga kura wapya katika jimbo hili kwenye uchaguzi huu mdogo.

Vile vile, kutokana na kitendo hicho cha NEC kuongeza idadi ya wapiga kura wapya kwenye daftari kimesababisha kuongezeka kwa vituo vya kupigia kura tofauti na ilivyokuwa mwaka 2010, ambapo Jimbo la Chalinze lilikuw ana jumla ya vituo 286 na sasa vimekuwa 288.
  • Kutangaza matokeo kinyume cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi
Msimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, katika kufanya majumuisho ya kura, alienda kinyume cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kwa kutangaza matokeo ya jumla bila kufanyika majumuisho ya kituo kimoja baada ya kingine, kama sheria inavyomtaka.

Kitendo hicho kilikuwa kinyume na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu 80(3), kinachosema;

“Baada ya taarifa zote za matokeo na masanduku ya kura yaliyo na karatasi za kura za uchaguzi wa bunge kupokelewa kutoka vituo vya kupigia kura katika jimbo, Msimamizi wa Uchaguzi, baada ya kuamua uhalali wa kura zozote zenye mgogoro na kabla ya kujumlisha kura hizo, atatangaza kwa sauti matokeo ya kila kituo cha kupigia kura katika jimbo kimoja baada ya kingine.”

Badala yake, Msimamizi wa Uchaguzi alitangaza matokeo ya jumla kwa kila kata, bila kufanyika kwa majumuisho kama sheria inavyotaka, jambo ambalo linapelekea matokeo yaliyotangazwa kutokuwa halali kisheria, huku yakitofautiana na matokeo tuliyonayo kwa mujibu wa fomu za matokeo.
  • Matumizi ya rasilimali za umma kuibeba CCM na mgombea wake
Tangu mwanzo wa kampeni CCM, kinyume cha sheria zinazosimamia uchaguzi, wametumia rasilimali za umma kumfanyia kampeni mgombe wao, kushawishi na kuelekeza wapiga kura.

Kuna mifano mingi katika suala hili; upo ushahidi unaonesha kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa akifika jimboni hapa kwa kutumia magari ya serikali na watumishi wa umma, ambapo alihusika kufanya kampeni za ‘mtu kwa mtu’.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Ally Mohamed Shein, ambaye alikuja Chalinze kwenye mkutano wa ufungaji wa kampeni za chama chake huko Miono, naye alitumia rasilimali za umma, k.m; magari na watumishi (wakiwemo kutoka vyombo vya ulinzi na usalama), waliokuwa kwenye msafara wake, kufanya kampeni za chama cha siasa, kushawishi na kuelekeza wapiga kura, kinyume kabisa na sheria na taratibu za uchaguzi.

Mama Salma Kikwete ambaye ni kiongozi mwandamizi wa CCM, kwa muda takriban wote wa kampeni alikuwa akitumia rasilimali za umma kama vile magari (yaliyokuwa na namba za ikulu) na watumishi, kufanya kampeni za kumnadi mgombea wa chama chake.
  • CCM kufanya kampeni siku ya uchaguzi
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alifanya kampeni siku ya kupiga kura, akiwa kwenye kituo cha kupigia kura, ambapo alinukuliwa na na kutangaazwa moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari, akisema yeye amempigia kura mgombea wa CCM.

Kitendo hicho cha Rais Kikwete ambacho kililenga kufanya kampeni, kushawishi na kuelekeza wapiga kura, ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 104 (1), ambacho kinasema;

“Hakuna mtu atakayefanya mkutano siku ya kupiga kura au; ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo…kuonesha upendeleo au nembo nyingine inayoonesha kuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi.”

Kifungu cha 104 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kinasema;
“Mtu yeyote atakwenda kinyume na kifungu hiki, atakuwa amefanya kosa…”
  • Vishawishi vya rushwa kwa ajili ya kujitoa
Kinyume na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 91B, ambacho kinasema; “Mtu yeyote atakayemshawishi au kumsababisha mtu mwingine kujitoa kuwa mgombea katika uchaguzi kwa kupewa malipo, ukuwadi wa malipo au ahadi ya malipo na mtu yeyote….atakuwa amefanya kosa la rushwa na iwapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo kisichozidi miaka mitano,” mgombea wa CCM aliwatumia makuwadi wake kumshawishi mgombea wa CHADEMA ajitoe kwa ahadi ya kupatiwa cheo atakachokuwa tayari, kati ya ukuu wa mkoa au wilaya, mahali popote nchini.

Imetolewa leo Bagamoyo, Aprili 7, 2014 na;
John Mrema
Mkuu wa Operesheni ya Uchaguzi Mdogo-Chalinze

BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGIIIII

No comments:

Post a Comment